Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2003-12-04 15:06:23    
Mradi Wa Kupeleka Gesi Sehemu ya Mashariki Kutoka Sehemu ya Magharibu Nchini China

cri
    Mradi unaojengwa hivi sasa wa kupeleka gesi sehemu ya mashariki kutoka sehemu ya magharibi, ni mradi wa njia ndefu kabisa ya kusafirisha gesi kwa mabomba nchini China. Njia hiyo yenye urefu wa kiasi cha kilomita 4,000 inapeleka rasilimali nyingi ya gesi kutoka sehemu ya magharibi kwenda sehemu ya mashariki yenye upungufu wa nishati. Tangu kuanzishwa ujenzi wake, mradi huo wa kupeleka gesi umepata ushirikiano mkubwa kutoka sekta mbalimbali husika za China. Hivi sasa ujenzi wa mradi huo unaendelezwa vizuri.

    Mradi wa kupeleka gesi ya sehemu ya magharibi kwenye sehemu ya mashariki ni mradi moja mkubwa wa nishati katika harakati ya ustawishaji wa sehemu ya magharibi ya China. Ujenzi wa mradi huo ulizinduliwa tarehe 4 mwezi Julai mwaka 2002 ukiwa na sehemu tatu za uchimbaji, usafirishaji na matumizi ya gesi ya asili ambapo zimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa idara mbalimbali za serikali kutokana na ukubwa wa mradi huo. Kutatuliwa kwa haraka kwa matatizo mbalimbali yanayotokea katika ujenzi wa mradi, kumehakikisha ujenzi kuendelea vizuri.

    Kufuatana na matakwa ya mradi wa kupeleka gesi ya sehemu ya magharibi upande wa sehemu ya mashariki, wizara ya ardhi na maliasili ilimaliza haraka majadiliano na kutoa uthibisho wa kuwepo kwa rasilimali ya gesi ya asili. Hivi sasa, imehakikishwa kwamba kiasi cha gesi iliyoko katika viwanja kadhaa vilivyoko kando ya njia ya kusafirisha gesi kimefikia mita za ujazo trillion 1.86, na uwezo wa kutoa gesi ya asili kwenye viwanja hivyo utafikia mita za ujazo bilioni 100 hivi ifikapo mwaka 2020.

    Eneo la ardhi inayotumika katika ujenzi wa mradi wa usafirishaji wa gesi ni kiasi cha hekta elfu 22. Ili kuhakikisha kwamba ujenzi wa mradi unaanza kwa kufuata mpango uliowekwa, wizara ya ardhi na rasilimali ya asili iliweka kigezo cha fidia cha namna moja kwa ardhi inayochukuliwa na kutumiwa katika ujenzi. Mkuu wa idara ya mpango wa wizara ya ardhi na rasilimali ya asili, Bw. Pan Wen-can alisema kuwa hivi sasa mabomba yaliyokwisha tandikwa yamezidi kilomita elfu 3 ambapo maslahi ya wakulima waliochukuliwa ardhi yamelindwa. Alisema,

    "Matumizi ya ardhi katika ujenzi wa mradi yanahusiana moja kwa moja na maslahi ya wananchi walioko kando ya njia ya usafirishaji wa gesi. Kabla ya ujenzi wa mradi kuanza, tulishauriana na idara na wananchi ambao ardhi yao itatumika kwa muda na kuafikiana nao kwenye mapatano; baada ya kumalizika kwa ujenzi wa mradi, watarejeshewa ardhi yao yenye hali kama ya hapo awali. "

    Suala la uhifadhi wa mazingira ya asili katika ujenzi wa mradi wa usafirishaji wa gesi ya sehemu ya magharibi kwenda sehemu ya mashariki pia ni lenye matatizo mengi. Njia hiyo inapita kwenye sehemu nyingi za jangwa, nyanda za juu, mbuga, mashamba na ardhi zenye majimaji za mikoa na miji zaidi ya kumi. Kabla ya ujenzi wa mradi kuzinduliwa, shirika la uhifadhi wa mazingira ya asili la taifa lilikamilisha utaratibu wa ukaguzi na kuidhinisha taarifa kuhusu athari kwa mazingira ya asili na limeagiza kwamba maeneo ya ujenzi yawekwe wazi katika njia yote ya ujenzi yenye kilomita zaidi ya 4,000 na kupiga marufuku magari na mitambo ya kazi kwenda nje ya maeneo ya kazi, ili yasije yakakanyaga na kuharibu miti na majani. Kutokana na maelezo ya mkuu wa idara ya usimamizi ya shirika la taifa la uhifadhi wa mazingira ya asili Bw. Zhu Xing-xiang ni kwamba kuna maeneo 24 ya hifadhi ya mazingira ya asili kandokando ya njia ya mabomba. Idara za ujenzi zimefanya marekebisho mara nyingi juu ya mpango wa ujenzi ili kupunguza kadiri iwezavyo athari na uharibifu kwa maeneo hayo ya hifadhi ya mazingira ya asili. Alisema,

 " Katika sehemu ya ujenzi mkoani Xinjiang, wameongeza urefu wa njia ya mabomba kwa kilomita 35 kwa ajili ili kuyakwepa maeneo ya hifadhi ya mazingira ya asili; katika maeneo ya hifadhi yaliyoko katika jangwa, wamehifadhi ipasavyo mahali pa kunyweshea maji wanyama na kadhalika, Ili kupunguza athari ya ujenzi kwa maeneo ya hifadhi ya mazingira ya asili."

     Usalama wa viwanja vya mafuta ya petroli na gesi ya asili ni suala lingine kubwa linaloukabili ujenzi wa mradi wa usafirishaji wa gesi. Naibu Kiongozi wa idara ya usalama ya wizara ya usalama ya China Bw. Yang Qi alisema kuwa, wizara ya usalama pia imechukua hatua za usalama ili kuhakikisha kwamba ujenzi wa mradi wa usafirishaji wa gesi unaendelezwa bila matatizo yoyote. Alisema,

     "Shughuli za kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa gesi ni za mfumo mzima wa idara ya usalama, ambazo zinapaswa kutoa adhabu kubwa kwa uharibifu dhidi ya ujenzi wa mradi, kutatua haraka masuala yote yanayokwamisha ujenzi wa mradi, kufanya utafiti juu ya vitisho vyovyote vinavyoukabili mradi ili kuhakikisha kwamba ujenzi wa mradi huo unaendelezwa bila matatizo."

     Licha ya ushirikiano na msaada uliotolewa na idara zote husika za China katika utafiti wa rasilimali, utandikaji wa mabomba ya usafirishaji wa gesi na uhifadhi wa mazingira ya asili, wizara husika za China pia zilifanya shughuli nyingi katika soko la matumizi ya gesi ya asili katika sehemu ya mashariki.

    Kutokana na ushirikiano kutoka pande mbalimbali, ujenzi wa mradi wa usafirishaji wa gesi umepata mafanikio makubwa, njia ya mabomba ya upelekaji wa gesi yenye urefu wa kilomita 1,500 kutoka mkoa wa Shanxi hadi Shanghai umekamilishwa, na idara husika zimekamilisha maandalizi ya kutoa gesi kwa mji wa Shanghai tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2004.