Mkoa Unaojiendesha wa Tibet uko katika nyanda za juu za Qinghai-Tibet, kaskazini magharibi mwa China, ambapo ni nyanda za juu kabisa duniani. Mahekalu yenye kuta nyeupe na paa nyekundu, waumini wanaosujudu kila baada ya hatua huku wakiomba dua na kujongelea mahekalu ni mandhari pekee ya Kitibet isiyoonekana sehemu nyingine duniani.
Shughuli za dini kubwa au ndogo zinafanyika kila siku katika kila hekalu.
Wafuasi wa Dini ya Buddha ya Kitibet wanaona Hekalu la Jokhang ni mahali patakatifu. Miaka 1,300 iliyopita mfalme wa Dola ya Tubo, yaani Tibet ya leo, Songtsam Gambo alijenga hekalu hili kwa mujibu wa usanifu wa mkewe Wencheng, binti wa mfalme wa Enzi ya Tang, na kuweka ndani ya hekalu hilo sanamu ya mwanzilishi wa dini ya Buddha, Sakyamuni, iliyopakwa rangi ya dhahabu aliyoleta mkewe kutoka Enzi ya Tang.
Mwandishi wetu aliona kwamba ndani na nje ya Hekalu la Jokhyang walikuweko waumini wengi ambao walikuwa wanatandaza karatasi sakafuni wakajilaza mwili mzima juu yake na kunyoosha mikono mbele, kisha wakainuka na kuanza tena kutoka mikono ilipofikia. Sauti pekee iliyosikika ndani ya hekalu hilo ilikuwa ya karatasi.
Miongoni mwa waumini wako watawa wa kiume waliovaa majoho ya rangi majano au nyekundu, na pia wako waumini raia. Zhoma ni mtawa wa kike kutoka Mkoa wa Sichuan, jirani na Tibet, naye alimwambia mwandishi wetu kwamba ana umri wa miaka 25, na mwaka huu ni mwaka wake wa 7 tangu awe mtawa. Alisema "Nimekuwa hapa Lhasa miezi 6 sasa, na nimesujudu kwa muda wa mwezi mmoja na siku 25 katika hekalu hili. Katika muda wote huo kila siku alasiri nasujudu mara 600."
Katika mji wa Lhasa, popote ulipo ama barabarani au vichochoroni lakini hukosi kuwaona waumini wakiomba dua kwa kunong'ona. Ukitembea nyumbani kwa Watibet utaona shubaka ya kuwekea sanamu za Buddha na chumba maalumu cha kusomea msahafu.
Ukitaka kuelewa vilivyo dini ya Buddha ya Kitibet ni bora ufike Lhasa katika sikukuu za dini. Sikukuu za dini ni nyingi mwaka mzima. Kwa mfano, Sikukuu ya Ibada Kubwa, Sikukuu ya Taa za Siagi, Siku ya Kufukuza Mashetani na Sikukuu ya Mtindi. "Sikukuu ya Mtindi" inatokana na dhehebu kuu la Gelugpa la dini ya Buddha ya Kitibet kuweka amri ya kutoruhusu watawa kutoka nje ya hekalu. Siku wanaporuhusiwa kutoka, watawa wote walishuka milimani kwa furaha na kuburudika na maziwa yaliyoganda.
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, kwenye ibada kubwa ilioneshwa picha ya Sakyamuni iliyochorwa katika kitambaa chenye urefu wa mita 31 na upana wa mita 41. Waumini zaidi ya elfu kumi kutoka nchini na nchi za nje walistaajabia picha hiyo. Hii ilikuwa ni zawadi kwa ajili ya kusherehekea maadhimisho ya miaka 13 ya kiongozi wa dini ya Buddha ya Kitibet, ambapo katika muda wa siku tano kiongozi huyo aliwatakia baraka waumini elfu 30 kwa kuwagusa utosini.
Athari kubwa ya kidini pia inatokana na mahekalu mengi huko Tibet. Kuhusu namna ya kuhifadhi mahekalu hayo, naibu mwenyekiti wa tawi la Shirikisho la Waumini wa Dini ya Buddha Ce Molin alisema: "Zipo sehemu 1,400 za kufanyia shughuli za dini huko Tibet na watawa karibu 46,000. Serikali ilitumia pesa nyingi ili kukarabati mahekalu yaliyoharibika. Katika muda wa miaka 20 iliyopita serikali ilitenga yuan milioni 400 ili kuhakikisha sehemu ya ibada na utawa.
Mwandishi wetu alishangaa kutogundua mahekalu yaliyokarabatiwa. Kuhusu hayo mzee mmoja mtawa alimweleza kuwa, "Mwaka 1991 serikali ilitenga pesa yuan milioni tatu kukarabati Hekalu la Jokhang, ukarabati huu ni mkubwa katika miaka 300 iliyopita, mradi wa ukarabati ulichukua miaka mitatu na miezi sita, ukarabati ulifuata kanuni za kukarabati majengo ya zamani yawe kama ya zamani bila kubadilisha sura yake ya awali, kwa hiyo mwandishi wetu hakuweza kugundua mahekalu kama ni mapya.
Mtawa huyo aliyosema "bila kubadilisha sura ya awali" na "majengo ya zamani yakarabatiwe kama ya zamani"ndio kanuni muhimu katika ukarabati wa majengo ya kihistoria.
Kuhusu kuamini dini kwa hiari na hifadhi ya mahekalu huko Tibet, balozi mdogo wa Nepal huko Lhasa Bw. Sanker Prathan Panpy alisema, "Nikiwa Mnepal nimeona kwamba ama Kasri ya Potala au mahekalu yote yamehifadhiwa kwa makini mjini Lahsa. Serikali ya China imetenga fedha nyingi kutunza mahekalu na kuyafanya kumbukumbu hizo ziendelee miaka hadi miaka. Kwa kuona hayo mliyofanya nafurahi."
Si muda mrefu uliopita serikali ya China kwa mara nyingine tena imetenga fedha yuan milioni 300 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya Kasri ya Potala, mradi huo utachukua muda wa miaka mitano.
Idhaa Ya Kiswahili
|