Mhamiaji mmoja alikuwa akitizama magenge matatu kabla ya kuaga maskani yake ya miaka mingi.
Kwa maoni ya mzee He xueming mwenye umri wa miaka 50, maisha yake ya hivi sasa ni mazuri zaidi kuliko alivyotarajia. Mhamiaji huyo alieleza kuwa, maisha yake yamebadilika sana baada ya kuhamishiwa katika nyumba mpya.
Akisimama mbele ya nyumba yake yenye orofa mbili, Mzee He aliongea na mwandishi wetu wa habari. Alisema kuwa, familia yake ilihamishwa mwaka 1999, ambapo mwanzoni aliona huzuni kwa kuwa, alikuwa ameagana na marafiki zake. Lakini watu wote walioishi katika wilaya yake walikuwa wamehamishwa, na marafiki zake walikwenda mkoa wa Jiangxi na mji wa Shanghai. Hivi sasa, anawapigia simu mara kwa mara.
Familia ya mzee He ina watu watano, ambao walikuwa wanaishi katika wilaya iliyopo katika kitongoji cha mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China. Wilaya hiyo ipo karibu sana na mto Changjiang, na hapo mwanzoni kila mto huo ulipofurika, maji yalifunika shamba dogo la familia hiyo. Kwa vile, familia hiyo ilikuwa inashindwa kujitosheleza kwa chakula na mavazi kwa kutegemea shamba hilo dogo peke yake, ilikuwa inambidi mzee He afanye biashara ndogo ya kuuza mayai na kufanya vibarua.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya China iliamua kujenga mradi wa maji wa magenge matatu. Wilaya waliyoishi mzee He na familia yake ilikuwa katika eneo la bwawa. Kwa hivyo, kuanzia hapo, mzee He na wenzake walianza kufanya matayarisho ya kuhama. Miaka minne iliyopita, familia yake na familia nyingine zaidi ya 100 zilihamishiwa katika wilaya ya Youxi, mjini Jiangjin, kilomita 400 mbali na maskani yao ya zamani. Wilaya hiyo ya Youxi vile vile ipo kando ya mto Changjiang, lakini kuna eneo kubwa la mashamba na watu wachache, na wilaya hiyo ni maarufu kwa uzalishaji wa machungwa nchini China. Baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa bwawa la magenge matatu, maji hayatafika kiwango cha kuimeza wilaya hiyo.
Hata hivyo, ilichukua muda kwa familia ya mzee He kuzoea maisha katika nyumba mpya. Akikumbusha siku zile, mke wa Bw. He, Mama Qiu Heping alisema, "Mwanzoni nilipolima mashamba na kupanda michungwa, mikono yangu iliumia na kutokea malengelenge, nililia kwa mara kadhaa. Nilisema, si wazo zuri la kuja hapa, tungehamishwa mjini ambako tusingelima mashambani."
Lakini familia hiyo ikazoea maisha mapya kwa haraka. Kwa kutumia misaada ya serikali ya dola za kimarekani zaidi ya elfu 10, walijenga nyumba ya orofa mbili yenye eneo la mita 300 za mraba, ambayo ukubwa wake ni mara tatu ya nyumba waliyoishi hapo mwanzoni. Mbali na hayo, katika shamba la karibu nusu hekta walilopewa na serikali, walianza kupanda mpunga na michungwa. Serikali pia iliwapelekea mafundi kuwafundisha teknolojia za kilimo na mifugo. Mzee He anafurahia sana maofisa wa serikali ya wilaya na mafundi, akisema, "Wanatusaidia sana sisi wahamiaji. Wanakuja kututembelea mara kwa mara, wakituuliza kuhusu hali ya kiuchumi, hali ya makazi yetu na hali ya miti ya michungwa. Kwa nini wanatufuatilia namna hii? Hawafurahii hali duni ya maisha yetu, na wanataka familia zote zipate pesa. Wanatusaidia kweli. Wanachoka sana wakitembeatembea huku na huko."
Sasa ni miaka minne imepita. Bw. He na mke wake wanafurahia maisha katika maskani yao mpya. Mwaka 2002, chini ya msaada wa mafundi, Bw. He alinunua miti 400 ya machungwa ya aina mpya. Hivi sasa, familia hiyo inapata dola za kimarekani karibu elfu 3 kwa mwaka kwa kutegemea machungwa peke yake.
Hivi sasa, Bw. He na mke wake pia wanatembelea majirani mara kwa mara, wakiongea sana. Mzee He alisema kuwa, amepata marafiki wengi wapya. "Mwanzoni, niliwakumbuka sana marafiki zangu wa miaka mingi, lakini sasa siwafikirii sana, na sasa inanibidi kuwafikiria marafiki mapya."
Mzee He alieleza kuwa, anapenda kupumzika nyumbani baada ya kazi za siku nzima, ambapo anatizama televisheni akinywa chai.
Ingawa maisha yao yameboreshwa sana, lakini mzee He na mke wake wana upweke kiasi. Wao wana watoto watatu, ambao wote wameondoka kutoka kwenye familia na kwenda kujiendeleza katika miji mingine. Miaka mitatu iliyopita, mtoto wao mkubwa na mke wake walikwenda Shenzhen, ambao ni mji mkubwa wenye ustawi ulipo kusini mwa China, ambapo wanaendesha saloon moja ya kutengeneza nywele. Binti pekee wa familia hiyo pia anafanya kazi katika kampuni moja ya makazi mjini Shenzhen, na mwaka jana, mtoto wao mdogo alijiunga na jeshi. Mzee He alisema kuwa, amepata pesa kwa hiyo, hawezi kusahau kutoa mchango kwa taifa.
Familia hiyo yenye watu watano hivi sasa imebakiwa na mzee He na mke wake. Wanasema, wanafuatilia sana maendeleo ya watoto wao. Na watoto wao pia wanawaandikia barua, kuwapigia simu na kuwatumia fedha mara kwa mara. Mtoto wao mkubwa anataka wazee hao waende mjini Shenzhen kuishi pamoja nao. Lakini mzee He ana maoni yake mwenyewe. "Mji mkubwa si mzuri, ambapo nakaa nyumbani siku zote, siwezi kuwatembelea majirani, naona, nitaumwa nikiishi mjini kwa muda mrefu. Napendelea vijiji, ambapo hewa ni safi sana, natembea kila ninapokwenda. Napanda vizuri miti ya machungwa, na kuchuma pesa nyingi. Je, unaona maisha ya vijijini ni safi au la?"
Mwezi Juni, mwaka 2003, bwawa la magenge matatu lilijaa maji. Idara ya uhamiaji iliwaalika mzee He na wahamiaji wengi warudi maskani yao ya zamani, wakashuhudia magenge matatu mapya. Mzee He alieleza kuwa, alikuwa anasisimka sana mpaka kulia. "Makazi ya zamani yamezama kwenye maji, na mto umekuwa mpana sana, ambapo mto una sura ya kupendezwa na mpana, na maji yanaonekana yamesimama, si kama mwanzoni ambapo maji yalikwenda haraka sana. Sasa likawa kama ziwa tulivu."
Mzee He alisema, sasa ndoto yake kubwa ni kutunza barabara miti ya machungwa. Na mke wake Mama Qiu pia alieleza matumaini yake ya kuwafuga vizuri nguruwe wake. Hivi sasa, hawafikirii tena maisha ya mwanzoni, kwa vile, yaliyopita yamepita kabisa, na maisha mapya yameanza.
Idhaa ya Kiswahili 2004-01-08
|