Sura ya Mto Changjiang katika sehemu ya Magenge Matatu, ambapo maji yanakwenda haraka sana.
Changjiang ni mto mkubwa wa kwanza hapa nchini China. Katika sehemu ya mwanzo ya mto huo, kuna sehemu ambayo huitwa mto Chuanjiang, ambao ni maarufu kwa hatari kwa vile una kina kifupi na umwembamba. Hapo awali, usafiri wa boti katika mto huo ulikuwa mgumu sana na kubidi kusaidiwa na wafanyakazi maalumu, ambao walibeba kamba mabegani wakivuta boti ziliposafiri kwa kukata maji, na kuzisukuma ziliposafiri kwa kufuata mkondo. Kazi hiyo ilihitaji ushirikiano mkubwa wa wafanyakazi, la sivyo boti zingeweza kuzama na wafanyakazi hao pia kupoteza maisha. Kwa hivyo walikuwa wanafanya kazi kuzisaidia boti huku wakiimba nyimbo zenye mahadhi maalumu, nyimbo hizo zimepewa jina la "Haozi".
Hivi sasa, hawepo tena watu wanaovuta boti wala nyimbo za Haozi, bali hadithi hizo zimehifadhiwa kwenye kumbukumbu, na watu wanaojua kuimba Haozi wapo wachache sana. Mzee Chen Banggui mwenye umri wa miaka 87 ni mmojawapo. Alisema "Nilipokuwa na umri wa miaka 13, kutokana na umaskini pamoja na wazazi wangu wote kufariki dunia, nilifanya kazi ya kuvuta boti. Kazi hiyo ilikuwa nzito na ngumu sana, hata hivyo napenda kuimba Haozi."
Mwendo wa maji katika Mto Chuanjiang hubadilika sana, na kulingana na hali tofauti za mwendo wa maji, nyimbo za Haozi pia hubadilika. Nyimbo hizo zilikuwa zikibadilika miongoni mwa watu waliovuta boti kizazi baada ya kizazi, sasa kuna aina 26 za Haozi ambazo zimehifadhiwa pamoja na maneno ya nyimbo hizo yasiyohesabika. Maneno hayo yametungwa na wafanyakazi wenyewe wakieleza hisia zao za furaha, hasira na uchungu.
Mwaka 1949, Jamhuri ya watu wa China ilipoasisiwa, serikali ilitenga fedha kuboresha usafiri wa mto Chuanjiang, na kuanzia hapo kazi hatari za kuvuta na kusukuma boti zimekuwa zikifanywa na mashine, kwa hivyo ikaleta mabadiliko katika maisha ya wafanyakazi waliovuta boti. Bw. Chen Banggui alipata ajira katika Kampuni ya Kivuko ya mji wa Chongqing, ambapo maisha yake yalianza kuboreshwa.
Ingawa ameacha kazi hatari za kuvuta boti, lakini nyimbo za Haozi alizokuwa akiziimba wakati wa kazi hakuzisahau na zikawa sehemu ya maisha yake. Bw. Chen alifundishwa kusoma na kuandika. Baada ya kukusanya na kusahihisha nyimbo hizo, alianza kuimba Haozi kwenye jukwaa. Katika miaka ya 50 na 60 ya karne iliyopita, akiwa msanii wa umma(fork artist), aliwahi kufanya maonyesho ya nyimbo za Haozi katika mji mkuu Beijing, ambapo viognzoi wa China wa wakati huo, marehemu Mao Zedong na Zhou Enlai walimpokea Bw. Chen. Mwaka 1987, alifanya onyesho nje ya China na kuimba nyimbo za Haozi mbele ya wageni.
Mwaka 1987, Bw. Chen aliimba nyimbo za Haozi kwenye maonyesho ya muziki ya umma zinazohusu mito mikubwa ulimwenguni, yaliyofanyika nchini Ufaransa. Wakati huo, alikuwa na umri wa miaka 71, na onyesho lake lilivutia watu wengi.
Hivi sasa, mzee huyo amestaafu kwa miaka mingi. Anaishi kwa raha na watoto na majukuu zake. Hata hivyo, hawezi kusahau nyimbo za Haozi. Alieleza kuwa, hivi sasa hakuna haja kwa waendesha boti kupambana na sehemu hatari za Mto Chuanjiang, lakini anaona masikitiko ya kiasi kwa vile hakuna tena nyimbo za Haozi.
Hata hivyo, si mzee Chen peke yake anayependa nyimbo za Haozi, bali pia familia yake nzima. Mjukuu wa mzee Chen, anayeitwa Xiong Yan, sasa anasoma katika chuo kikuu mjini Beijing. Bibi Xiong Yan alisema kuwa, kila ifikapo sikukuu, familia hiyo yenye watu zaidi ya 20 huungana, ambapo mzee Chen anapenda kuimba nyimbo za Haozi pamoja na watoto na wajukuu wake. Msichana huyo alieleza jinsi anavyopenda nyimbo hizo na masikitiko yake. "Kuna kitu kimoja nasikitika sana, kwamba katika familia yangu, hakuna mtu hata mmoja anayeweza kurithi nyimbo za babu. Tatizo kuu ni kwamba, hatukushuhudia maisha magumu ya watu waliovuta boti. Kwa hivyo, ni vigumu kupata moyo wa nyimbo hizo. Huenda kwa siku za baadaye, hatuna chaguo lingine bali kuhifadhi nyimbo za Haozi kwenye rekodi."
Ingawa mzee Chen mwenyewe ana matumaini makubwa kwamb, moyo wa nyimbo hizo utaweza kuendelea, anatambua kuwa, maisha ya hapo awali yametoweka kabisa, na bila maisha hayo, mwimbaji hawezi kuimba nyimbo za Haozi kama walivyokuwa wafanyakazi waliovuta boti.
Mradi wa magenge matatu umezinduliwa miaka 10 iliyopita, ambao ni mradi mkubwa wa hifadhi ya maji unaojengwa katika Mto Changjiang, mto mkubwa wa kwanza nchini China. Mradi wa magenge matatu ni mkubwa kuliko yote duniani, una uwezo wa kudhibiti mafuriko ya maji, kuboresha usafiri wa meli katika mto Changjiang na kuzalisha umeme.
Ingawa amezeeka sana, mzee Chen anafuatilia ujenzi wa mradi huo. Katika miaka hii, hakuacha utungaji wa maneno ya nyimbo za Haozi. Na mwaka huu, wakati bwawa la mradi wa magenge matatu lilipoanza kulimbikiza maji, alitunga wimbo kwa kusherehekea tukio hilo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-01-15
|