Wachina wanachagua bidhaa kwa ajili ya Sikukuu ya Spring.
Tarehe 22, Januari ni siku ya kawaida kama siku nyingine katika nchi za Afrika, lakini kama mungekuwa nchini China au kama mnakaa katika mahali ambapo kuna Wachina, mtaona shamrashamra kubwa ajabu. Kumbe, siku hiyo ni mwaka mpya wa Kichina, kwa maneno ya Kichina, ni Sikukuu ya Spring.
Kwa mujibu wa kalenda ya Kichina, siku hiyo ni tarehe mosi, Januari. Na kwa Wachina wote popote walipo duniani, iwe wale wanaokaa nchini China, au wale wanaoishi ng'ambo, Sikukuu ya Spring ni sikukuu muhimu kuliko nyingine yote katika mwaka mzima. Mbali na hayo, sio Wachina peke yao ambao wanasherehekea Sikukuu ya Spring, bali pia watu wa nchi nyingine za Asia, zikiwemo Korea ya Kusini, Japan, Viet Nam, Singapore n.k..
Je,jinsi Wachina wanavyosherehekea sikukuu hiyo kubwa?
Kwa mujibu wa historia, Wachina walianza kusherehekea Sikukuu ya Spring tokea miaka elfu nne iliyopita. China ni nchi iliyopo nusu ya kasakzini ya ikweta, na tofauti na nchi za Afrika ya Mashariki na ya Kati, nchini China kuna majira manne kwa mwaka, na Spring ndiyo ni majira ya kwanza katika mwaka. Na tokea mwanzo China ni nchi ya kilimo, na majira Spring ni wakati ambapo wakulima wanaandaa mbegu. Kwa hiyo, Wachina wanauchukulia mwanzo wa majira ya Spring kuwa ni mwanzo wa mwaka mpya, na kuupa mwaka mpya huo jina kama Sikukuu ya Spring.
Tunaweza kulinganisha Sikukuu ya Spring na Sikukuu ya Krismasi katika nchi za magharibi na Sikuku ya Idd el Fitr kwa Waisalamu, kwa vile zina uzito unaofanana.
Kwa mgeni anayetoka nchi za Afrika au nchi za magharibi, utashangaa sana kuona tofauti zilizopo katika mwezi Desemba wa kalenda ya kimataifa kwa China na nchi nyingine za mashariki ya mbali. Ukiwa barani Afrika ambako waumini wa dini ya kikristo na Waislamu ni wengi, mwezi wa Desemba ni mwezi wenye pilikapilika nyingi. Kwa wakristo huo ni mwezi wa maandalizi ya sherehe ya Sikukuu ya Krismasi, na Waislamu huwa katika shamrashamra za Sikuku ya Idd el Fitr. Hata baada ya sikukuu hizi mbili za kidini, watu wote bila kujali dini zao hujumuika pamoja na kusherekea kuukaribisha mwaka mpya yaani tarehe mosi Januari kwa kalenda ya kimataifa.
Lakini, hali hii ni tofauti na hali iliyopo nchini China na nchi nyingine za mashariki ya mbali.
Nchini China, katika mwezi Desemba shughuli zote za kiuchumi na kijamii huendelea kama kawaida. Utaratibu katika ofisi za serikali, mashule na hata biashara huendelea kama kawaida.
Wapo baadhi ya Wachina wanaosherehekea sikukuu hizo za Krismasi na Idd el Fitri, kwa vile, wapo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo, ukubwa wa sherehe hizo hauwezi kulingana na ule wa sherehe za Sikukuu ya Spring, ambayo pia ni siku za muungano wa familia.
Tukichukua mfano wa mwezi wa Desemba, mwaka 2003, kulikuwepo hali fulani ya kusherekea sikukuu ya Krismasi, japo sio kwa kiwango kikubwa. Maduka yalikuwa yakiuza bidhaa mbalimbali zinazohusiana na sikukuu hiyo, kulikuwa na miti ya Krismasi na baadhi ya vibandiko vyenye ya kutakia kheri ya krismas na mwaka mpya, na baadhi ya watu walisherekea sikukuu hiyo wakiwaunga mkono wageni wachache kutoka nchi mbalimbali na wachina wakristo wanaosherekea sikukuu hizi.
Hata wakati wa mwaka mpya wa kalenda ya kimataifa, unaweza kuona sherehe zenyewe si kubwa nchini China.
Ukiwa mgeni utajiuliza, kama watu wa nchi hii hawasherekei sana sikukuu hizi, basi kwao sikukuu kubwa ni ipi, na wanasherekea vipi siku hiyo? Kumbe, sikukuu kubwa kabisa kwa Wachina ni mwaka mpya wa Kichina, wakati mwingine inaitwa sikukuu ya majira ya spring. Siku hii inaweza kuwa mwishoni mwa mwezi wa Januari au mwanzoni mwa mwezi Februari kutegemeana na kalenda ya kichina.
Wiki kadhaa kabla ya kufika siku yenyewe, pilikapilika zinaonesha kabisa kuwa sikukuu kubwa inakaribia. Mitaa mbalimbali imepambwa kwa maua na mapambo mengine yenye rangi nyekundu, hata ukiingia katika mikahawa na katika ofisi za serikali mapambo yanayohusiana na sikukuu hiyo yatakufanya utambue kuwa siku muhimu imekaribia.
Hata hivyo, Sikukuu hiyo pia huleta tatizo la usafiri, kwani Sikukuu ya Spring ni siku ya muungano wa familia, na watu wanaofanya kazi nje wanarudi nyumbani kabla ya mkesha wa sikukuu hiyo. Kwa hiyo, kabla ya Sikukuu ya Spring, katika kipindi cha muda mfupi kumekuwa na msongamano mkubwa wa watu wanaotaka kusafiri kwenda sehemu mbalimbali na kufanya bei za tiketi kupanda au hata kuwabidi watu kusubiri kwa muda hadi nafasi kwenye vyombo vya usafiri ipatikane.
Na kabla ya mkesha wa sikukuu watu nyumbani wanakuwa na pilikapilika nyingi. Kwani katika siku hiyo wanakula chakula cha jioni kwa pamoja nyumbani, ambapo sisi Wachina tunaita chakula hicho cha jioni kuwa chakula cha muungano.
Mbali na chakula, katika mkesha wa Sikukuu ya Spring, mila nyingine muhimu ni watu kuusubiri mwaka mpya hadi saa 6 usiku, kengele za mwaka mpya zinapogongwa. Na baadhi ya watu, hasa watoto, vijana na watu wa makamo hawalali kabisa usiku kucha.
Watoto nao wanaofurahia sana sikukuu hiyo, kwa vile, wanaweza kupata zawadi kutoka wazazi, zawadi zenyewe kwa kawaida ni pesa. Na katika mila ya Wachina, watu hulipua fataki kusherehekea sikukuu hiyo. Chanzo cha mila hiyo kongwe ni kufukuza bahati mbaya. Lakini hivi sasa mila hiyo imepigwa marufuku na serikali katika miji mingi mikubwa, kama vile Beijing, kwa sababu, kila mwaka kunakuwa na watu wengi, hasa watoto wanaojeruhiwa na fatatki, mbali na hayo, fataki pia zinaleta uchafuzi mbaya.
Basi, katika siku ya kwanza ya mwaka mpya kwa kalenda ya Kichina, je kwa kawaida watu wa China wanafanya nini?
Kuanzia siku hiyo, watu wanavaa nguo mpya wanatembeleana na kusalimiana. Siku hizi, si lazima watu kwenda maskani kwa marafiki kuwasalimia, bali wanaweza kuwasalimia kwa simu, e-mail, na hata ujumbe wa simu za mikono.
Hivi sasa, watu wa China wanapumzika kwa siku saba wakati wa Sikukuu ya Spring, yaani kutoka tarehe mosi, Januari katika kalenda ya Kichina mpaka siku ya saba, kwa mwaka huu ni kuanzia leo mpaka tarehe 28. Lakini kwa kweli, kutokana na mila za Wachina, sherehe za Sikukuu ya Sping huendelea kutoka siku saba kabla ya leo mpaka siku 15 baada ya leo, kwa jumla ni muda wa wiki tatu hivi.
Pamoja na kupumzika, kuungana na familia, kutembeleana kati ya jamaa na marafiki, hivi sasa Wachina wengi wanapenda kutalii katika mapumziko ya siku saba ya Sikukuu ya Spring. Kwa vile, hivi sasa ni majira ya siku za baridi katika sehemu kubwa nchini China, kwa hiyo, watu wengi wanapendelea kusafiri katika nchi za nje. Mwezi Desemba, mwaka jana, China na nchi 8 za Afrika, zikiwemo Tanzania na Kenya, zilisaini mikataba ya utalii. Kwa maoni yangu, wakati wa mapumziko ya Sikukuu ya Spring ndio majira mazuri katika nchi za Afrika ya Mashariki, kwa hiyo, hakika watakuwepo Wachina wengi zaidi na zaidi watakaosafiri kwenda barani Afrika siku za baadaye katika mapumziko ya Sikukuu ya Spring.
Idhaa ya Kiswahili 2004-01-22
|