Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-01-22 21:03:48    
Chakula cha Jiaozi cha kichina

cri

   JIAOZI

     "Jiaozi" ni chakula kama sambusa ndogo. Mtu akisema "jiaozi" ni sehemu ya utamaduni wa China, anakuwa hajatia chumvi hata kidogo. Chakula hicho cha kiasili kikiandaliwa nyumbani kinaashiria muungano wa familia, na kikiandaliwa kuwakaribisha wageni kinaashiria ukarimu na heshima ya wenyeji kwa wageni. Kama wageni wa ng'ambo wakifika nchini China na kurudi makwao bila kuwahi kula "jiaozi", basi watachekwa na kusemwa kuwa walikwenda bure nchini China.

    Kwa kifupi, "jiaozi" ni chakula kama sambusa ndogo kilichotengenezwa kwa kijazo na sehemu ya nje ya unga wa ngano, na kinapikwa kwa kutoswa katika maji yanayochemka. Zamani "jiaozi" kilikuwa ni chakula cha sikukuu na hasa katika mkesha wa mwaka mpya wa Kichina.

    Kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanyika ili kutayarisha "jiaozi". Kwanza ni kutengeneza kijazo. Kwa kawaida kijazo kina mchanganyiko wa nyama na mboga, lakini kwa wakati mwingine huwa na kijazo cha nyama peke yake au mboga. Wakati wa kutayarisha kijazo, kazi kubwa ni kukatakata nyama na mboga kwa kiasi kinachotakiwa na kuchanganya viungo. Wakati wa kukatakata, kisu kinapopigapiga mbao kinatoa mlio, na mlio wake hubadilika kadiri kisu kinapopiga kwa nguvu tofauti. Watu hupenda mlio huo wa katakata za kutayarisha kijazo zisikike mbali na kwa muda mrefu zaidi, kwani mlio huo ukiwa wa muda mrefu zaidi unaashiria kutayarishwa kwa "jiaozi" nyingi zaidi na maisha yanawawia mema.

    Baada ya kutayarisha kijazo kazi inayofuata ni kufunga kijazo, "jaozi" hutengenezwa kwa umbo dogo kama mwezi, na sehemu yake ya nje hufungwa kwa vidole gumba na shahada. Vijijini, "jiaozi" hufungwa kwa kutia alama kama mashuke ya ngano zikiashiria mavuno mazuri.

    Baada ya "jiaozi" kuwa tayari, kazi inayofuata ni kuzitosa katika maji yanayochemka, na kukoroga koroga pole pole ili zisigandamane kwenye sufuria. Wakati inapochemka hutiwa maji baridi kidogo mara tatu na baada ya dakika ishirini hivi "jiaozi" zinakuwa tayari.

    Kabla ya kula, bakuli la kwanza hupaliliwa kwa ajili ya mababu kama ni tambiko, bakuli la pili hupakuliwa kwa ajili ya miungu wanaowaamini na kuomba dua. Baada ya yote hayo ndipo jamaa wanapoanza kula, na baada ya kumaliza kula ni bora kubakiza "jiaozi" kadhaa shufwa, ikiwa ni ishara ya ziada kila mwaka.

    Katika mkesha wa mwaka mpya, "jiaozi" ni chakula cha lazima, jamaa wanaofanya kazi katika sehemu nyingine ama wafanyabiashara au wanafunzi, wote hurudi nyumbani wakijiunga na wazazi wao. Wanatayarisha "jiaozi" kwa pamoja na kula pamoja, hukuk familia nzima ikifurahia sikukuu.

    Lakini hivi sasa baadhi ya desturi zimebadilika. Katika zama hizi, vijana wa mijini hawatengenezi "jiaozi" bali wananunua kutoka dukani au moja kwa moja wanakwenda kula hotelini.

Idhaa ya Kiswahili 2004-01-22