Panda ni aina ya wanyama ambao wapo katika hatari ya kutoweka kabisa. Wanyama hawa wanapatikana nchini China peke yake. Mji wa Yaan ulioko mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China, ni miongoni mwa sehemu ambazo wapo wanyama hao wenye sura ya kupendeza. Miaka miwili iliyopita, China ilitenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa makao makubwa kabisa duniani ya kuwahifadhi panda katika sehemu iitwayo Bifengxia, huko Yaan. Makao makuu hayo yanawavutia watu wanao wapenda panda na wachunguzi wa panda duniani kote. Hivi karibuni, mwandishi wetu wa habari alitembelea makao makuu hayo, na sasa nakuleteeni makala inayohusu utunzaji wa wanyama hao.
Panda ni maarufu kama hazina ya taifa ya China ni aina ya wanyama ambao wapo katika hatari ya kutoweka kabisa. Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa, kuna panda wapatao elfu 1 tu duniani, na wengi wao wanaishi milimani kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa China, ambapo kuna misitu ya mianzi ambayo ni chakula kikuu cha panda pamoja na maji mengi.
Mwanzoni panda walikuwa wanakula nyama, lakini baada ya mabadiliko ya mamilioni ya miaka, hivi sasa wanakula aina zote za vyakula. Katika miaka ya 100 ya hivi karibuni, panda wamekuwa wakikabiliwa na hatari ya kutoweka kabisa kwa vile, uwezo wao wa kuzaliana umepungua, miti ya mianzi ambayo ni chakula chao kikuu imepungua na mazingira ya mahali wanapoishi yameharibika.
Katika miongo kadhaa iliyopita, panda wamekuwa wakipendwa sana na watu wa nchi mbalimbali duniani. Serikali ya china imekuwa ikiwachukulia kama ni zawadi kubwa, imewazawadia au kukopesha kwa nchi na sehemu zaidi ya 20. China inawajibika kuwatunza panda.
Ofisa wa mji wa Yaan Bw. Li Guobin alisema kuwa, tishio kubwa kwa panda ni tatizo la kuzaa. "Katika mambo ya kuwahifadhi panda, kuna matatizo kadhaa magumu, na miongoni mwa matatizo hayo, ugumu wa kuzaliana ni tatizo kubwa zaidi likifuatiwa na tatizo la chakula kwa panda. Panda mama akizaa kitoto, si rahisi kukilea. Panda mtoto anapozaliwa anakuwa mdogo sana, uzito wake unakuwa ni kati ya gram 90 hadi 100 tu, ni vigumu sana kumtunza."
Bw. Li alifafanua kuwa, kutokana na utafiti wa wataalamu wa panda, asilimia 80 ya majike ya panda hayana uwezo wa kuzaa, huku asilimia 90 ya madume hayana uwezo wa kuzaa. Kwa hiyo, kuwafanya panda wazaliane kwa mbinu za binadamu ni suala gumu la utafiti.
Tokea miaka ya 60 ya karne iliyopita, China ilianza majaribio ya kuzalisha panda kwa mbinu za binadamu. Katika muda mrefu, wafanyakazi walikuwa wana uwezo wa kuvilea kwa mafanikio vitoto vya panda 10 hivi kwa mwaka. Katika miaka ya hivi karibuni, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka. Mwaka 2003, China ilifanikiwa kuvilea vitoto vya panda vipatavyo 16. Kwa upande wa utafiti kuhusu chakula cha panda, China pia imepata maendeleo.
Ili kutafiti na kuinua kiwango cha mafanikio ya kuzaliana kwa panda kwa kutumia mbinu za kibinadamu, China ilijenga makao makuu ya kuwatunza panda mwaka 2001 katika sehemu ya Bifengxia, huko Yaan.
Makao makuu hayo huchukua hekta karibu 500, yapo mlimani ambapo kuna maji mengi na mimea mingi. Ndani ya makao makuu hayo, kuna eneo la kuzaliana kwa panda, eneo la panda wadogo, hospitali ya panda, na taasisi. Kwenye hospitali ya panda kumewekwa zana za kisasa. Zimepandwa aina 7 mpaka 8 za mianzi ambayo ni chakula wanachopendelea zaidi panda. Kila panda ana chumba chake chenye kiyoyozi na maji safi, na nje ya vyumba, kuna ua wenye eneo la mita elfu 2 mpaka 3 za mraba.
Naibu mkurugenzi wa makao makuu hayo Bw. Tang Chunxiang alieleza kuwa, "Tunajitahidi kuyajenga makao makuu yetu yawe miongoni mwa makao makuu mazuri kabisa nchini China katika maeneo ya kinga na tiba za maradhi ya wanyama, afya zao, uokoaji wao, pamoja na maeneo ya mafunzo kwa watu, upashanaji wa data na uingizaji wa zana mbalimbali. Kwa upande mwingine, tunafanya mfuatano wa utafiti katika taaluma ya viumbe, vitendo vya panda n.k."
Hivi sasa, kuna wafanyakazi zaidi ya 20 katika makao makuu hayo, ambao wanawatunza panda zaidi ya 10, kuwafuatilia na kurekodi mienendo yao. Bw. Xu Erxing aliyemaliza masomo katika chuo kikuu cha kilimo cha Sichuan amefanya kazi katika makao makuu kwa miaka miwili. Anaweza kufahamu hali ya afya ya panda kutokana na kinyesi chake.
"Ninaandaa chakula kwa panda kila siku, na kuwafuatilia hali zao, kama vile wamekula vipi, wamepumzika vipi, vitendo vyao na vinyesi vyao. Kwa mfano, iwapo panda moja akihara, kuna sababu mbili kuu, moja ni maradhi ya tumbo, na nyingine ni kula chakula kingi kuliko mahitaji yake."
Bw. Xu alisema kuwa, anajivunia sana kazi yake inayohusiana na panda. Kila anapowafuga panda, anajisikia kama panda wanamwona kama rafiki, huwa anataka kuwagusa na kuwabusu. Baadhi ya nyakati, anawafikiria sana panda baada ya kazi, unapoingia usiku, anasafiri kwa baiskeli yake kwa nusu saa kwenda kwenye makazi ya panda ili kuwaangalia.
Katika shughuli za kuwahifadhi panda, si kama tu ni wajibu wa wafanyakazi wa makao makuu hayo, bali pia wanavijiji wanaokaa karibu na makao hayo wanafanya hivyo kwa hiari. Mwanakijiji Bw. Lin Genchang alisema, "Panda ni muhimu sana katika maisha yetu, na kila mtu wa sehemu hiyo anafahamu kuwa anatakiwa kuwatunza na kuwahifadhi panda. Na misituni, ni mwiko kuvuta sigara."
Mwanakijiji huyo alisema kuwa, ama mlimani ama barabarani, wakiwakuta panda walioumia au wenye njaa, wanavijiji huwasaidia kwa hiari, au kutoa ripoti kwa idara ya uhifadhi wa wanyama ya sehemu hiyo.
Wageni wengi waliotembelea makao makuu hayo wanayasifu sana. Bibi Anna Babajanyan kutoka Armenia aliyatembelea makao makuu hayo mara tatu. Alieleza kufurahishwa na kazi ya huko. "Watu wa huko wanawatunza vizuri panda, na watu wengi wakiwemo wanafunzi wanasafiri kwenda huko ili kuwaangalia panda. Wafanyakazi wa makao hayo wanatuambia kuwa, inatubidi kufuata utaratibu, kwa mfano, huwezi kutoa sauti kubwa wala kuwadhuru panda, vile vile kuna miiko mingine. Naona ni jambo la kusisimua kuwaangalia panda katika makao hayo."
Idhaa ya Kiswahili 2004-02-12
|