Mti wa Loquat wenye matunda.
Mkoa wa Sichuan uliopo kusini magharibi mwa China ni mkoa wa pili kwa idadi kubwa ya watu, na pia unajulikana sana kwa shughuli za kilimo. Katika muda mrefu uliopita, mkoa wa Sichuan ulikuwa unakabiliwa na tatizo la kuwa na idadi kubwa ya wanavijiji na eneo dogo la mashamba. Ili kuongeza ufanisi wa mashamba yake, katika miaka ya karibuni Sichuan imetekeleza mkakati unaoitwa "kusitawisha kilimo kwa sayansi na elimu", ukiwa ni juhudi za kuendeleza kilimo chenye umaalumu na kuboresha maisha ya wakulima. Leo hii, hebu twende mkoani Sichuan, China, tushuhudie maisha ya wakulima wa huko. Karibuni.
Katika kijiji cha Meiman, mtaa wa Long Quanyi, ulioko kwenye kitongoji cha Chengdu, mji mkuu wa mkoa wa Sichuan, yuko mzee You Kailong mwenye umri wa miaka 67 mwaka huu, ambaye anakaa chini ya mti wa loquat ndani ya ua wa nyumba yake. Loquat ni aina ya miti inayozaa matunda matamu yenye rangi ya manjano, matunda yake yanapendwa sana na watu kutokana na utamu wake. Mzee You anatuambia kuwa, anauza matunda hayo mengi kwa mwaka, pamoja na mapato yaliyopatikana katika shughuli za utalii ambazo zimeendelezwa kutokana na miti ya loquat, familia yake inapata mapato ya jumla ya Yuan za Renminbi elfu 60 hadi 70, sawa na dola za kimarekani elfu 7.3 hadi 8.5. Akizungumzia maisha ya hivi sasa, mzee huyo anaongea akiwa na majivuno. "Kutokana na kupanda miti ya matunda, tumemudu ujenzi wa nyumba mpya, tuna zana za umeme za aina mbalimbali nyumbani. Kwa mfano katika familia yangu, tuna friji, televisheni na pikipiki, vitu hivyo vyote ni ghali sana, lakini tunayo pesa."
Mkuu wa kijiji cha Meiman Bw. You Jiang alifahamisha kuwa, kijiji hicho kipo milimani. Mwanzoni watu wa huko walitegemea kilimo cha nafaka, na walikuwa maskini. Hivi sasa, familia zote zipatao 530 za kijiji hicho zinashughulika na upandaji wa miti ya loquat. Aidha, wakulima wanapanda mazao ya nafaka na mazao mengine yenye thamani kubwa. Pamoja na mapato ya utalii, wastani wa pato la mwanakijiji kwa mwaka limezidi Yuan za Renminbi elfu 4, ambazo ni sawa na dola za kimarekani 500.
Hata hivyo, kada huyo ameeleza kuwa, mwazoni ilikuwa ni vigumu sana kuwashawishi wanakijiji wapande miti ya loquat badala la nafaka. "Labda ni kutokana na kuwa, wenzangu walizoea umaskini, hawataki mabadiliko. Waliona kuwa, wasipopanda mazao mengine badala ya nafaka, watakabiliwa na njaa. Kwa hiyo, mwanzoni ilikuwa ni vigumu sana kwa kuwashawishi wapunguze maeneo ya mashamba ya mazao ya chakula, na kupanda miti ya matunda."
Lakini kuboreshwa kwa miundo ya uzalishaji ni mwekeleo mkuu usiopingika. Mtaa huo wa Long Quanyi una watu wengi lakini una eneo dogo la mashamba, ambapo kwa wastani kila mtu ana shamba lenye hekta 0.05 tu, na kwa kutegemea kilimo cha mazao ya nafaka, wastani wa pato la mwanavijiji kwa mwaka ulikuwa ni Yuan za Renminbi mia 6 hivi, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani 73 tu.
Kutokana na hali kama hii, mwaka 1987 serikali ya mtaa huo iliweka mkakati wa kuendeleza upandaji wa miti ya matunda. Katika miaka mitatu iliyofuata, vituo 7 vya miti ya matunda vilijengwa ambavyo huzalisha matunda ya aina mbalimbali yenye thamani kubwa, ikiwemo mizabibu, madete na loquat.
Matunda ya Loquat yanayopendeza.
Naibu mkuu wa idara ya maendeleo ya kilimo ya mtaa wa Long Quanyi Bw. Luo Yucheng alisema kuwa, mwanzoni, ili kuwahamasisha wakulima wapande miti ya matunda, watumishi wa idara yake walitembelea vijiji vingi kueneza habari hiyo kwa wakulima. Mbali na hayo, serikali ya mtaa ilitoa sera nafuu kwa wakulima. Kwa mfano, iwapo wakulima wakihama na hawawezi kuhama pamoja na miti ya matunda, serikali inawafidia kiasi ambacho kinalingana na mavuno ya miti yake ya miaka mitatu. Serikali pia iliruhusu kuwa, watoto wa wakulima wanaweza kurithi miti ya matunda.
Mkuu wa kijiji cha Meiman Bw. You Jiang alisema kuwa, loquat ni matunda yenye thamani kubwa ya kiuchumi, na hivi sasa mavuno kutoka kwenye miti yake katika hekta moja kwa mwaka yanauzwa kwa Yuan za Renminbi laki moja na elfu 50, ambazo ni sawa na dola za kimarekani elfu 18.8. Aidha, kila sehemu ya miti ya loquat ina manufaa yake. Kwa mfano, majani yake yanaweza kutumika kwa kutengeneza dawa; matunda yake, pamoja na utamu wake, yanasaidia kupunguza homa mwilini na kunufaisha mapafu. Kwa hiyo, hivi sasa wakulima wengi wanapenda kupanda miti ya loquat.
Ili kuinua kiwango cha mavuno ya matunda ya loquat, inabidi kutegemea mbinu za kisayansi. Naibu mkuu wa Idara ya kilimo ya mkoa wa Sichuan Bw. Zhao Xueqian alisema kuwa, mkakati wa kustawisha kilimo kwa sayansi na elimu unatekelezwa mkoani kote, akisema, "Kila mwaka wakati wa msimu wa kilimo, serikali ya mkoa wa Sichuan inawatuma mafundi wapatao elfu moja kutembelea vijijini. Mafundi hao wa kiwango cha juu wanatoka taasisi za kilimo na mijini, wanawasaidia mafundi elfu 10 wa wilayani, wakiwafundisha wakulima vijijini, ambapo wanashirikiana wakiwafundisha wakulima uso kwa uso ujuzi wa kupanda na kutunza miti ya matunda."
Bibi Zeng Xiuying sasa anatunza miti ya loguat kwa mbinu za kisayansi. "Mwanzoni sikufahamu kabisa namna ya kutunza miti ya loguat, ambapo nilijifunza mwenyewe na kupata uzoefu hatua kwa hatua, na mapato pia yalikuwa makubwa mwaka hadi mwaka. Ni mafundi waliokuja walitusaidia, walituhamasisha na kutufundisha namna ya kutunza miti hiyo, na walitupa mbinu zote."
Mkuu wa kijiji cha Meiman Bw. You Jiang alieleza kuwa, kutokana na matunda ya loquat kuwa maarufu kwa utamu na manufaa kwa afya, wakazi wengi wa mijini wanakuja vijijini kuyanunua, na pia wanawatembelea wakulima nyumbani kwao, kula chakula pamoja nao, na kutalii vijijini. Kwa hiyo, utalii umeendelezwa vijijini.
"Walaji wanaona kuwa, hali ya hewa na mazingira vijijini ni nzuri. Wanawatembelea wakulima nyumbani na kula chakula kinachoandaliwa na wakulima. Ukitaka kupumzika, bora uende vijijini. Hivi sasa, shughuli za utalii zimeendelezwa sana katika kijiji chetu, ambapo kuna familia 120 za wakulima zinazowapokea watalii, na wanavijiji zaidi ya 500 wanashughulikia utalii. Kwa kutegemea utalii peke yake, mapato ya wakulima yamefikia fedha za Renminbi Yuan milioni 3 kila mwaka, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani laki 3 na elfu 66."
Hivi sasa, kwa kutegemea kilimo cha matunda na nafaka na shughuli za utalii, wakulima wengi katika mtaa wa Long Quanyi wamepata pesa. Katika kijiji cha Meiman, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, nyumba zenye orofa moja au mbili zinaonekana kila mahali, na nyumba hizo zimejengwa kwa ustadi na kupendeza sana. Wakulima walisema kuwa, katika siku za mwanzoni, walikuwa hawana uwezo wa kupata chakula cha kutosha, sembuse kujenga nyumba nzuri na kuzipamba.
Idhaa ya Kiswahili 2004-02-19
|