Hivi sasa watu wengi wameacha kutumia simu za mkononi za aina ya zamani, na kuanza kutumia simu za mkononi za aina mpya zinazoweza kupiga picha ambazo zinauzwa sana madukani. Lakini mkondo huo wa matumizi ya simu hizo umeleta changamoto kubwa kwa haki ya watu ya kuhifadhi sura zao, hatua ambayo imezifanya nchi nyingi duniani kuweka vizuizi vingi kwa matumizi ya simu za aina hiyo.
Simu zinazoweza kupiga picha ziligunduliwa miaka miwili iliyopita na zilikuwa kubwa na ghali. Lakini katika muda wa miaka miwili hiyo iliyopita, simu za aina hiyo zimekuwa ndogo, kiasi cha kuweza kulingana na zile za kawaida, tena bei zake zimekuwa chini, hivyo simu za aina hiyo zinanunuliwa na watu wengi siku hadi siku.
Taarifa moja iliyotolewa na kampuni moja inayofanya utafiti wa masoko nchini Marekani inasema kuwa mauzo ya simu za mkononi duniani yaliendelea kuongezeka mwaka 2003 na kukisiwa kufikia milioni 460. Mauzo makubwa ya simu za mkononi yalitokana na sababu mbili muhimu, ya kwanza ni kwamba simu za mkononi za bei rahisi ziliuzwa kwa wingi, ya pili ni kwamba watu wengi walibadilisha simu za mkononi kwa simu za aina mpya zinazoweza kupiga picha.
Lakini, kuongezeka kwa simu za mkononi zinazoweza kupiga picha kumekuwa tishio kwa haki ya watu ya kuhifadhi siri zao, hususan katika baadhi ya sehemu za umma kama vile vyumba vya kubadilishia nguo na klabu za kujenga mwili. Hivi sasa, kuna picha nyingi zilizopigwa kwenye sehemu za umma bila wenyewe kujua zikiwemo za klabu za kujenga mwili, migahawa na hata kwenye vyoo vya mitaani. Baadhi ya majarida ya wachezaji nyota na tovuti za nchi za magharibi zinawahamasisha wasomaji kupiga picha za wachezaji nyota wakati wanapoonekana kwenye sehemu za umma, na kuzipeleka kwenye majarida au tovuti.
Baadhi ya nchi zimetambua uzito wa tatizo hilo na zimeweka vizuizi kwa kamera hizo zinazofichika. Nchini Japan, simu za mkononi zinazoweza kupiga picha haziruhusiwi kutumika katika klabu za kujenga mwili na ofisi za idara za serikali; nchini Uingereza wateja wenye simu zinazoweza kupiga picha wanakatazwa kuingia katika klabu za kujenga mwili na kumbi za dansi za usiku. Serikali ya Italia imeweka vizuizi na kukataza watu kutumia simu zinazoweza kupiga picha; nchini Australia, wanasiasa wanajitahidi kusihi kupitishwa kwa mswada mpya wa sheria inayokataza kuwa na simu zinazoweza kupiga picha mashuleni; nchi nyingi za mashariki ya kati zinanuia kutunga sheria kuzuia matumizi ya simu za aina hiyo.
Lakini, wakati huo huo wafanyabiashara wanajitahidi sana kutangaza sifa za simu zinazoweza kupiga picha. Kampuni ya Nokia ambayo imechukua theluthi moja ya soko la simu za mkononi duniani, inajaribu kuongeza uwezo wa kupiga picha kwa aina zote za simu za mkononi inazozalisha tangu kuanzia nusu ya pili ya mwaka 2004, na kuchukulia uwezo huo kuwa ni wa kimsingi kama wa milio na orodha ya namba za simu. Wachambuzi wa masoko wa Marekani wanasema kuwa maendeleo ya simu zinazoweza kupiga picha yamepatwa na matatizo. Kwa upande mmoja wafanyabiashara wa simu za mkononi wanajitahidi kuuza simu zao, lakini kwa upande mwingine sehemu nyingi za umma zimekataza watu kutumia simu za aina hiyo. Kutatua suala hilo kunahitaji wafanya biashara wa simu za mkononi kushauriana na idara za usimamizi za serikali za nchi mbalimbali.
Kampuni moja ya Uingereza hivi karibuni imevumbua tekinolojia ijulikanayo kwa "Sehemu ya usalama peponi" ambayo inafanya simu zinazoweza kupiga picha kupoteza uwezo wake huo katika maeneo fulani. Lakini sharti lake ni kuweka zana za udhibiti katika simu zenye uwezo wa kupiga picha wakati zinapozalishwa. Wataalamu wachambuzi wanasema kuwa maendeleo ya simu zinazoweza kupiga picha yanakumbwa na matatizo kutokana na kwamba, ni vigumu kwa wafanya biashara wa simu kukubaliana katika kipindi cha muda mfupi kutumia kigezo cha aina moja katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-02-24
|