Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-02-26 09:28:58    
Mji wa Shihezi, lulu la jangwa katika kaskazini magharibi ya China.

cri

Sura ya mji wa Shihezi. 

    Mkoa wa Xinjiang uliopo mpakani kaskazini magharibi mwa China una eneo kubwa, na unachukua moja ya sita ya eneo la ardhi ya China. Lakini inasikitisha kuwa, eneo la jangwa mkoani Xinjiang pia ni kubwa sana, ambalo huchukua zaidi ya asilimia 60 ya eneo zima la jangwa nchini China. Hata hivyo, kutokana na jitihada za watu wa vizazi kadhaa, hivi sasa miji mingi inayoonekana kuwa na rangi ya kijani imejitokeza katika eneo hilo la jangwa, na miongoni mwa miji hiyo, mji wa Shihezi ambao ni maarufu kama lulu la jangwa ndio mfano mzuri.

    Bw. na Bi. Wallace wanaotoka Marekani walifika mjini Shihezi mwaka mmoja uliopita, ambapo wanafanya kazi za ualimu katika chuo kikuu kimoja. Ingawa walikuwa wamekaa katika mji huo kwa muda mfupi, maelezo yao yameonekana kuwa wanaupenda mji huo. Bw. Patrick Wallace alisema, "Huu ni mji unaojaa rangi ya kijani. Kila unapoenda, unakuta majani na miti. Wakati wa usiku, unaweza kuangalia nyota angani. Na wakati wa siku za baridi, theluji ni nyeupe na safi sana. Tunafurahia sana kuishi katika mji wa Shihezi."

    Hivi sasa, katika kitongoji cha mji huo, imepandwa misitu inayokinga jangwa, na katika mji huo wenye eneo la kilomta 460 za mraba, karibu asilimia 40 ya eneo lake imepandwa mimea, hali ambayo ni nadra kuonekana katika miji iliyopo sehemu ya kaskazini magharibi mwa China. Mwaka 2000, mji huo ulipewa tuzo ya mfano mzuri ya kuboresha mazingira ya kukaa iliyotolewa na Umoja wa mataifa, na mwaka 2002, ulisifiwa kuwa ni mji wa bustani nchini China.

Jangwa linalozingira mji wa Shihezi. 

    Lakini nikikuambia kuwa, katika miaka 50 iliyopita, Shihezi ilikuwa mji mdogo uliojaa matete, utelezi na jangwa, utaweza kuamini? Wakati huo, wenyeji wa huko walisema kuwa, katika mji huo, upepo ulikuwa ni mkali kiasi cha kuhamisha mawe. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya upandaji miti ya mji huo Bw. Ran Baiyu alisema kuwa, mji wa Shihezi umebadilika kuwa mji wa bustani kutoka mji mdogo wenye upepo na jangwa. Mafanikio hayo yametokana na jitihada za wakazi wa vizazi kadhaa na utiliaji maanani wa serikali ya huko kuhusu uboreshaji wa mazingira. Ofisa huyo alikumbusha kuwa, "Katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, watu wa kwanza waliokuja kuendeleza sehemu hiyo walitoa wito wa kukinga upepo, kuzuia jangwa na kuboresha mazingira ya kuishi, ambao ni matakwa ya msingi ya maisha ya watu. Hadi kufikia miaka ya 60, liliweka lengo la kujenga mji wenye sura ya mashamba, na wakati wa miaka ya 80, lengo letu lilikuwa ni kujenga mji wenye mazingira mazuri ya kiasili. Na mpaka miaka ya 90, tuliweka lengo la kujenga mji wa bustani."

    Katika mpango wa serikali kwa mji huo, upandaji miti na majani siku zote unapewa kipaumbele. Kwa miaka zaidi ya 50 iliyopita, serikali ya mji huo imesaidia sana kazi za upandaji miti na majani kwa sera na fedha, nayo imetunga utararibu mkali wa kusimamia shughuli za upandaji miti na majani. Katika miaka mitatu ya hivi karibuni, serikali imegharimia jumla ya fedha za Renminbi Yuan milioni 300 katika kazi hiyo. Mbali na kuingiza aina za miti zenye sifa nzuri, serikali pia iliwaandaa watu maalumu wanaoshughulikam na utunzaji na usimamizi wa bustani na maeneo ya majani na miti mjini humo.

    Katika mji wa Shihezi, kupanda miti na kuboresha mazingira ni vitendo vya hiari vya wenyeji. Juu ya jambo hilo, Bw. Chen Quanwen anayeshughulikia usimamizi wa mabustani alisema, "Wakazi wa mji huo wamekuwa na nia imara ya kupenda na kutunza mimea. Kwa mfano, tunapofanya doria ni nadra kuwaona wakazi wanaokanyaga majani. Na kuna barabara moja iitwayo matufaha, hakuna wakazi wanaochuma matunda."

Katika bustani moja mjini Shihezi.

    Wakiangalia mji wanaojenga, wakazi wa Shihezi wanajivunia sana. Bibi Qian Meiping mwenye umri wa miaka 60 mwaka huu alifika mji huo alipokuwa msichana mwenye umri wa miaka 15, akiambatana na wazazi wake waliohamia kutoka mji wa Shanghai, mashariki mwa China. Alieleza mabadiliko ya mji wa Shihezi katika miaka 40 iliyopita. Alisema, "Shihezi imebadilika sana. Nilipokuja, ilikuwa sehemu yenye utata, ilikuwa hakuna barabara, zilikuwepo nyumba zenye orofa moja tu pamoja na njia za udongo. Lakini sasa tunaona mji huo umepata maendeleo, umekuwa na mazingira mazuri na mimea mingi."

    Kama Bibi Qian Meiping, wakazi wengi wa mji huo ni watu waliohamia kutoka sehemu mbalimbali nchini walipokuwa vijana wakilenga kuendeleza sehemu hiyo, na hivi sasa wamezeeka. Kwa mawazo ya kidesturi ya Wachina, watu wanapozeeka wanataka kurudi maskani yao kuishi na watakapofariki dunia wangependa kuzikwa huko. Lakini mjini Shihezi, watu hao wengi wameuchukulia mji huo kama ni maskani yao ya pili. Mzee Pan Zhijian aliyehamia kutoka mkoa wa Henan, katikati ya China, alisema, "Shihezi imeendelezwa kwa haraka sana. Hivi sasa hali ya maisha imeboreshwa sana. Kuna viwanja vya michezo, kumbi za muziki, mji huu ni wa kupendeza. Tunaona mazingira ya hapa ni mazuri. Tukirudi maskani, hatuwezi kuzoea maisha ya kule. Na watoto wetu pia wamezoea maisha ya hapa."

    Hivi sasa, mji huo wenye mazingira safi uliopo magharibi ya China umewavutia watu wengi wafanye kazi na kuishi hapo. Miongoni mwa wakazi wake, si kama tu wapo watoto wa watu wa kwanza waliohamia kuuendeleza mji huo, bali pia wapo watu wanaokuja hivi sasa kutoka sehemu nyingine nchini China, na pia wapo wageni kama vile Bw. na Bi. Wallace. Watu hao wanapenda mji huo wa kijani uliopo jangwani, na kuishi kwa furaha mjini humo.

Idhaa ya Kiswahili 2004-02-26