Hivi karibuni, jina la Bibi Zhou Xiaoguang limekuwa likisikika mara kwa mara katika vyombo vya habari, kwa kuwa hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mbunge wa taifa kutoa matangazo ya kuomba mawaidha na mapendekezo kutoka kwa wanamji hapa nchini. Hivyo Bibi Zhou alifuatiliwa sana na waandishi wa habari. Katika siku za kati ya tarehe 18 mwezi Januari na tarehe 8 mwezi Februari mwaka huu ambazo ni za kipindi cha sikukuu kubwa kabisa ya Spring, Bibi Zhou alitoa matangazo kwa siku 20 mfululizo kuomba mawazo na mapendekezo ya wanamji ili kufanya maandalizi ya kuandaa rasimu ya mswada wakati utakaofanyika hapa Beijing mwezi Machi. Bibi Zhou alisema, "Mjini Yiwu kuna watu wengi wanaofanya biashara au kuanzisha viwanda katika sehemu za nje, na baadhi yao walikwenda hata katika nchi za nje, lakini watu hao huwa wanarejea nyumbani katika kipindi cha sikukuu ya Spring. Ninataka kuwapatia nafasi ya kutoa mawazo na mapendekezo yao."
Mara tu baada ya matangazo kutolewa katika TV, ofisi aliyoianzisha Bibi Zhou ya kusikiliza maoni na mapendekezo ya wanamji ikaanza kuwa na shughuli nyingi. Kuna siku wafanyakazi walipokea simu zaidi ya mia moja. Mbali na kupiga simu, kulikuwepo baadhi ya watu ambao walifika moja kwa moja ofisini kutoa maoni yao kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo ya kilimo na biashara. Bibi Zhou alisema kuwa, kuomba mapendekezo ya wanamji kupitia njia ya TV, si kama tu kumeimarisha uhusiano kati ya mbunge huyu na wanamji, bali pia aliweza kufahamu mambo mengi ambayo hakuyafahamu hapo zamani, kutokana na barua nyingi alizopata kutoka kwa wanamji. Hivi sasa, Bibi Zhou na wasaidizi wake wanachambua mapendekezo waliyopata ili yawasilishwe bungeni yakiwa kama rasimu ya mswada. Habari zinasema kuwa katika mkutano mkuu wa bunge wa mwaka uliopita, Bibi Zhou Xiaoguang alitoa miswada ya maoni na mapendekezo 36 kwa jumla.
Bibi Zhou mwenye umri wa miaka 42 mwaka huu ni mkurugenzi mkuu wa kiwanda kimoja kikubwa binafsi mjini Yiwu, na alichaguliwa kuwa mbunge wa tokea mwezi Januari mwaka uliopita. Kabla ya hapo, Bibi Zhou alichaguliwa kuwa mjumbe wa mabunge ya miji ya Yiwu na Jinhua, ambapo alitoa maoni na mapendekezo kadhaa kw idara husika kuhusu maendeleo ya viwanda binafsi pamoja na mazingira ya biashara ya mji wa Yiwu kwa wageni waliotoka nchi za nje.
Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa taifa, Bibi Zhou alianza kufuatilia mambo mengi zaidi baada ya kupata hadhi ya ubunge wa taifa. "Mimi ni mbunge pekee wa taifa katika mji wa Yiwu, hivyo mambo ninayopaswa kueleza ni mambo yanayohusiana na wakazi wa mji wetu mzima, wala siyo kuwawakilisha wafanyabaishara peke yao."
Kwa kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa mbunge kutoa matangazo katika TV, hivyo alifuatiliwa na watu wa sekta mbalimbali. Bwana Chen Youjian ni mkazi wa mji huo ambaye hivi karibuni alikwenda katika ofisi ya Bibi Zhou kutoa mapendekezo yake, alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema kuwa hii ni njia nzuri kwa mbunge kusikiliza mawazo ya wananchi na kupeleka maombi yao kwenye mkutano wa bunge.
Vitendo hivyo vya Bibi Zhou pia vimesifiwa na baadhi ya wataalamu wa China. Profesa wa kitivo cha usimamizi wa serikali cha chuo kikuu cha Beijing Bw. Jin Anping alipofanya uchambuzi alisema kuwa kuomba maoni ya wanamji kwa kutumia chombo cha habari naona ni njia nzuri. Kwa China ya leo, magazeti , vituo vya radio na mtandao wa Internet vimekuwa vitu vya kawaida kabisa. Mimi binafsi naona huu ni mtindo mzuri wa kuhimiza siasa ya demokrasia kwa kutumia vyombo vya habari."
Hata hivyo, kuna baadhi ya watu wenye maoni tofauti. Wanasema kuwa ingawa kuomba mapendekezo ya wakazi kwa kutumia chombo cha habari ni mtindo mpya kabisa, lakini ni vigumu kutumiwa na watu wengi. Kwa sababu Bibi Zhou Xiaoguang anamiliki kiwanda, ana pesa nyingi, kwa hiyo sio shika kwake kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, lakini kwa wabunge wengine wasio na viwanda, si rahisi kwao kufanya hivyo. Bibi Zhou yeye mwenyewe anaona kuwa kuna njia nyingi za kuimarisha mawasiliano kati ya wabunge na wananchi. Kuomba mapendekezo ya wanamji kwa kutumia vyombo vya habari ni njia mojawapo tu, kuitisha mkutano na kuwatembelea wananchi pia ni njia nzuri ya kuimarisha uhusiano kati yake na wananchi.
Bibi Zhou alisema kuwa hivi sasa anasoma vitabu au kwenda nje kufanya uchunguzi kuhusu masoko ili kuongeza elimu yake. Anasema kuwa awe mfanyabiashara au mbunge, anapaswa kujitahidi kufanikisha kazi zake, na kutimiza matakwa ya wananchi waliomchagua.
Idhaa ya Kiswahili 2004-03-02
|