Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-07 20:48:33    
Mwanahistoria Mkubwa wa China, Dai Yi

 


cri

        Bw. Dai Yi

    Mwezi Januari mwaka jana mradi kabambe wa kuhariri historia ya Enzi ya Qing ulianza rasmi. Huu ni mradi mkubwa wa serikali ya China katika utamaduni, mradi huo utagharimu RMB yuan milioni mia kadhaa.

    Nchini China kuna desturi ya kuhariri historia ya enzi iliyotangulia. Katika miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, kila baada ya enzi fulani kumalizika basi mfalme wa enzi inayofuata alikuwa akiharakisha kazi ya kujumlisha historia ya enzi iliyopita ili kusaidia utawala wake. Kutokana na desturi hiyo China ni nchi yenye vitabu vingi vya historia, mfano wa vitabu hivyo ni "Historia 24".

    Mwaka 1911 enzi ya mwisho ya kifalme yaani Enzi ya Qing ilitokomezwa, ingawa wakati huo serikali iliyoendeshwa na mabwana wa vita iliwahi kushirikisha watu kuhariri historia ya enzi hiyo lakini kutokana na dosari na makosa mengi, muswada wa historia hiyo haukuchapishwa rasmi, lakini muswada huo kwa kiasi fulani una thamani.

    Mwaka 2003, mradi wa kuhariri historia ya Enzi ya Qing ulitolewa na serikali. Bw. Dai Yi, mzee aliyekuwa na umri wa miaka 77 wakati huo alichaguliwa kuwa mkurugenzi wa Kamati ya Uhariri.

    Bw. Dai Yi alizaliwa mwaka 1926 katika ukoo wa maofisa wa ngazi ya chini, alikuwa na tabia ya kusoma toka utotoni mwake. Kwa kiasi fulani tabia hiyo iliashiria kuwa yeye asingekuwa mwanasiasa, wala mfanyabiashara, bali angekuwa msomi atakapokuwa mtu mzima. Alisema, "Tokea utotoni mwangu kabla ya umri wa kwenda shule nilipenda kusoma soma lakini wakati huo vitabu nilivyosoma vilikuwa sio halisi, bali vilikuwa ni vitabu vya picha kwa watoto kama 'Mashujaa kwenye Vinamasi' na 'Madola Matatu ya Kifalme', vitabu ambavyo vinasimulia hadithi za kihistoria nchini China. Mimi ni mtu wa kawaida kabisa mwenye juhudi, watu wote wanaodadisi mambo fulani wanapaswa kuwa na juhudi na baada ya juhudi watakuwa na msukumo wa kikazi."

    Mzee Dai Yi aliongeza kusema kuwa alijua umuhimu wa juhudi. Katika miaka ya 30 hadi 40, ingawa China ilikuwa imezama katika machafuko ya vita, lakini kwa kufanya juhudi alifaulu mtihani wa kuingia Chuo Kikuu cha Mawasiliano mjini Shanghai. Lakini mwaka 1946 alipokuwa mwaka wa pili ghafla aliamua kuacha masomo yake katika chuo hicho na kujiunga na Chuo Kikuu cha Beijing kwa mtihani na kusomea historia. Tokea hapo kwa muda wa miaka 60 hivi hakuwahi kuacha kufanya utafiti wa historia, na kuwa mwanahistoria mashuhuri aliyebobea zaidi historia ya Enzi ya Qing.

    Katika muda wa miaka 20 hivi Dai Yi amewahi kuandika vitabu vingi muhimu kuhusu historia ya Enzi ya Qing ikiwa ni pamoja na "Utafiti kuhusu Historia ya Qing" yenye maneno milioni 8, "Watu Mashuhuri katika Historia ya Qing" pamoja na vitabu vya aina 30 kikiwemo kitabu cha "China na Dunia katika Karne ya 18". Bw. Dai Yi alisema, Enzi ya Qing iliyodumu kwa miaka 268, ina umuhimu mkubwa katika historia ya China, na hiyo ndio sababu iliyomfanya abobee katika utafiti wa historia ya enzi hiyo. Alisema, "Naona mchango wa Enzi ya Qing katika historia ya China ni mkubwa zaidi kuliko enzi nyingine, kwa sababu ilipofika karne ya 18 enzi hiyo ilitangulia mbele duniani kiuchumi na iliunganisha China kisiasa na mipaka ya sasa ya China iliwekwa katika enzi hiyo, mchango katika mambo hayo mawili ni mkubwa na muhimu sana, ni kipindi ambapo China ilikuwa kileleni katika historia."

    Bw. Dai Yi alisema, kwa mtafiti wa historia hakuna kitu chochote kinachomfanya aone ufahari kuliko kuhariri historia sahihi kwa ajili ya kuviachia vizazi vya baadaye. Lakini uhariri wa historia ya Enzi ya Qing ni mgumu, kwani kuna maoni tofauti miongoni mwa wanataalumu kuhusu namna ya kuhariri historia hiyo, kwamba ihaririwe kwa sura au kwa mfululizo wa miaka kama watu wa kale walivyofanya. Baada ya kutoleana hoja na kushauriana, mwishowe wameafikiana kuhariri kwa muunganisho wa ule wa mtindo wa zamani yaani kwa mfululizo wa miaka pamoja na mtindo wa kisasa yaani kwa sura.

    Bw. Dai Yi alisema kuwa uhariri wenyewe unaonesha dhahiri ukweli wa mambo yaliyotokea katika historia, na hautasikiliza mapendekezo ya serikali ya sasa kwa kulazimishwa. Alisema, "Mwanahistoria kwake muhimu ni kufuatilia ukweli ulivyokuwa katika historia bali sio kubuni historia kwa upotovu. Mambo ya zamani yaandikwe kwa ukweli wake, na historia iliyopotoka irudishwe jinsi ilivyokuwa. Wanahistoria sio wafuasi wa bendera ya serikali, lazima wawe na uhuru wa kuheshimu ukweli mambo yenyewe."

    Bw. Dai Yi alisema, histori ya enzi hiyo itakuwa na maneno milioni 30 ambayo ni mengi kuliko maandishi yoyote ya "Historia 24". Anaona fahari kubwa kushughulika na kazi hiyo akiwa hai. Anaamini kuwa kwa kuungwa mkono na serikali ya China, na kwa kuwa na wataalamu wa uhariri, upo uwezekano wa kumaliza kuhariri historia ya Enzi ya Qing kwa muda wa miaka 10.

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-06