Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la posta 97, Zanzibar, Tanzania anasema katika barua yake kuwa ameshtushwa na habari za kupasuka kwa mtambo wa gesi ya sumu, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100, na wengine kupata madhara na wale walionusurika kuhamishiwa sehemu yenye usalama kwa maisha yao.
Anasema anawapa mkono wa rambirambi wale waliofiwa na ndugu na jamaa zao na anawatakia moyo wa subira na kwa wale waliopata madhara. Anawapa pole na kuwatakia wapone haraka na kurejea katika makazi yao.
Bwana Karim anasema ajali ya aina yoyote haina macho. Muda si mrefu baada ya kutokea kwa ajali kubwa ya tetemeko la ardhi huko Bam nchini Iran, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mali zao, na wengine kufukiwa katika vifusi, huko Afrika Magharibi Cotonou (Benin) ajali ya ndege iliua watu zaidi ya 150. Basi ajali ni ajali, japo kuwa wahenga wanasema ajali haina kinga, lakini inatakiwa mtu kujikinga na ajali, na anawapa pale kwa wale wote waliokumbwa na maafa na kuwaomba wawe na subira.
Bwana Karim ametuelezea vizuri kuhusu ajali zilizotokea duniani, kweli mwaka jana na mwaka huu ajali za aina mbalimbali zilitokea katika nchi mbalimbali duniani, na kusababisha hasara na madhara kwa maisha na mali za watu. Hivi karibuni serikali ya China imekuwa ikiharakisha kukamilisha mfumo wa jamii wa kukabiliana na matukio yanayotokea ghafla ili kupunguza madhara na hasara kwa wananchi.
Msikilizaji wetu mwingine Makoye Mazoya wa Halmashauri ya wilaya, sanduku la posta 200, Magu Mwanza, Tanzania anatuambia katika barua yake kuwa, hana budi kumshukuru "Babuka" aliyetujalia na kutufikisha mwaka 2004, tuombe baraka zake ziendelee mara dufu .Amina.
Pamoja na shukurani hizo anapenda kutushukuru kwa zawadi tulizokwisha mtumia mwaka 2003 ikiwa ni pamoja na kalenda ya 2004, kadhalika anaipongeza China kuchukua nafasi ya tatu, kwa kufaulu kurusha chombo cha safari za anga ya juu: 'Bwana awazidishie"
Mwisho anasema tudumishe undugu kati ya Tanzania na China, tuwe na mshikamano wa kuweza kusaidiana kwa hali na mali, na vilevile anataka tusisite kumtumia magazeti ya picha inapowezekana. Tunamshukuru kwa shukrani zake kwetu, na tunapenda kumwambia asiwe na wasiwasi, inapowezekana, tutaendelea kumtumia magazeti, tunataka aendelee kusikiliza vipindi vyetu na kutuletea maoni yake.
Msikilizaji wetu wa sanduku la posta 1325 Bramwel Sirali wa Kitale, Kenya anasema katika barua yake kuwa, kuja China, angependa safari yake iwe hivi, apate mwaliko wa barua kama ule alioupokea wakati ule wa kongamano la tarehe 19 Septemba mwaka 2003 hapo Kisii. Angependa safari yake ianze siku ya Jumatatu, atoke hapo Kitale moja kwa moja hadi Kisii akipitia Webuye palipo na kiwanda kikubwa cha makaratasi nchini Kenya.
Anasema akiwa sehemu ya mbele kwenye gari aweze kuona mandhari nzuri ya magharibi mwa Kenya, Kakamega palipo na jiwe linalolia machozi kwenye njia ya kwenda Kisumu. Akifika Kisumu apate chakula cha mchana?ugali na samaki wa kutoka ziwa Victoria la Kisumu. Wakati huo huo wimbo wa Gabriel Omolo, 'Lunch Time' uchezwe isiwe kana kwamba watu hula nyama pekee, bali mchanganyiko maalum. Anaamini kuwa Wajaluo watafurahi kwa kuwachagulia wimbo wa mwenzao hapo Kisumu. Asingependa kusahau gazeti la kila siku 'Daily Nation'. Kisha safari iendelee mpaka Kisii hali akisalimiana na askari kadha wa kadha wa hapo nyumbani kwake Kitale.
Bwana Sirali anaendelea kusimulia ziara ya China anayoitazamia akisema, hapo Kisii angependa kupanda gari la watalii tayari kwa safari kwa mbuga za wanyama, pengine Maasai mara akiwa na Bibi Du Shunfang. Kisha waende moja kwa moja hadi shule ya msingi Ngong. Halafu wazuru shule ya upili ya starehe na kukutana na mwalimu msikilizaji wa Radio China kimataifa, waandamane naye hadi chuo kikuu cha Kenyatta. Pia nisingependa kusahau miwani kwa ajili ya haya. Kwa kweli ni vizuri sana kulingana na desturi ya mwafrika asiye na kipawa cha michezo; lazima apitie shule hizo tatu?shule ya msingi, shule ya upili halafu chuo kikuu ndipo apate anga nafasi ya kwenda nje ya nchi.
Anaeleza, katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta angependa kuonana na kikundi cha wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wasiozidi 30. Wakati makaratasi yanakunjwa kuwapata washindi saba wa nafasi maalum angependa kumwona kwanza Bw. Xavien T.L. Wambwa, Bw. Mogire Machuki, Bw. Franzi Mako Ngogo, Bw. Kefa Gichana na pia Bw. Gabriel Mwangi tuliyemkosa sana hapo Kisii. Kwa vile kina dada waliwahi kufika Beijing kukiwepo na mmoja si vibaya sana.
Anasema, ili safari yake iweze kufanikiwa maana angependa Nabii kutoka Hawaii awe hapo na rafiki yake kutoka kwake Sibanga ili watuombee mema kutoka kwa mungu kabla hawajasafiri pamoja hadi Honolulu. Akiwa angani pamoja na wenzake angependa wasalimiane hewani na wakristo wa St. Andrews Sibanga Parish na wote wanaomfahamu na ujumbe kwao ni wasife moyo kwani Bwana amewaandalia yalio mema.
Anasema, wakifika nchini China kwanza wangependa kumwona Bw. Fadhili Mpunji, Bw. Pomboo, mama Chen, Bw. Du Jiman, na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili kuwalaki na kumshukuru Mungu kwa ajili ya safari ndefu yenye kufaulu sana. Anasema ingekuwa vyema kama tukiwatayarishia ramani ya kila sehemu wanayozuru ili waweze kuijua China vizuri. Waona majimbo yote 23 kwenye ramani. Wakitembelea mkoa wa Hebei palipo na Ukuta Mkuu wa China ikiwezekana wazuru mkoa wa Jiangsu, Sichuan ama magharibi mwa China Qinghai. Angependa kuzuru kiwanda cha taa za mvuke cha China kwa vile anapenda sana nuru. Anasema furaha yake inaweza kuongezeka kama watafika usiku, kwani nuru yote ya Beijing itaangaza macho yake kwa hivyo kamwe hatatembea gizani!
Bwana Sirali ametusimulia vizuri ziara ya China anayoitarajia, kwa kweli yeye ni msimulizi mzuri na ametufurahisha sana. Wasikilizaji wetu wengi wana matumaini ya kupata nafasi ya kuja kutembelea China, kama wachina wengi wanavyotamani kupata nafasi ya kwenda nchi za Afrika kama Tanzania na Kenya kutembelea mbuga za Serengeti au Masai mara, kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea kwenye sehemu ya pwani na kwingineko kwenye mandhari nzuri. Bora tujitahidi na kutafuta njia ya kutimiza lengo letu.
Idhaa ya Kiswahili 2004-03-14
|