Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-27 16:59:38    
Barua za wasikilizaji 28/3/2004

cri
    Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha Sanduku la Barua. Leo tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu na kuwaletea maelezo kuhusu

    Msikilizaji wetu Gullam Haji Karim wa sanduku la posta 97 Zanzibar, Tanzania ametuletea barua alipokuwa Lindi Tanzania kwa karibu wiki mbili. Anasema hapo Lindi wanaishi watoto wake. Anasema yeye kuanzia tarehe mosi Februari 2004 amestaafu kazi aliyokuwa anaifanya. Pia ametupatia anuani yake mpya ambayo anaitumia kwa sasa kuwa ni sanduku la barua 504, Lindi, Tanzania, simu No. 0748 541248, simu ya mkononi 0232202834, LINDI dukani 0748232614. Anasema ukifika hapo unaweza kuacha salamu kwa mwanake.

    Anasema pia anapenda kuwajulisha wasikilizaji wenzake wote kuwa, sasa atakuwa Tanzania Bara. Wale wasikilizaji wa mikoa ya kusini hasa walioko Lindi mjini anawaomba wamtembelee. Anasema anakaa dukani nyuma ya kituo cha malazi Barabara ya msanabarini, dukani kwa riziki kwa mungu store. Anawashukuru wote watakaomtembelea.

    Bwana Karim anasema alipokuwa Lindi tarehe 29/2/04,baada ya taarifa ya habari na kipindi cha sanduku la barua alisikia barua yake ya salamu za mwaka mpya wa kichina ikisomwa, alifurahi sana lakini kwa sababu alikuwa ugenini na aliazima redio haikuwa vizuri sana kwake. Alisikia kwa mbali sana. Lakini alifahamu na kusikia barua hiyo ikisomwa.

    Anasema yupo hapo mkoani Lindi kwa muda wa mwezi mmoja. Na atarudi Zanzibar kwa ajili ya kufunga mizigo yake na kuhama moja kwa moja. Mara afikapo mara ya pili atatoa anuani hiyo itumike rasmi pamoja na namba za simu. Anatoa mwaliko tumtembelee huko mkoa wa kusini wa Tanzania Bara. Kuna bahari nzuri na fukwe za mchanga mweupe. Atakuwa mwenyeji wetu kuna mengi ya kutazama na kujifunza, anasema Lindi ni mji mzuri na mdogo usio na vurumai kubwa na ni shwari kabisa.

    Tunamshukuru Bwana Gullam Haji Karimu kutuandikia barua na kutuelezea hali ya Lindi, mji mzuri na anaoupenda,na akituoneshaa furaha yake ya kuhamia huko. Tuna matumaini kuwa Bwana Karim na pamoja na mke wake na watoto wao wataishi huko Lindi kwa raha mustarehe. Na tuna matumaini pia kuwa akiwa huko Lindi ataendelea kutusikiliza na kutuletea barua kama alivyoahidi, na kutuelezea mengi atakayoshuhudia huko Lindi ambao ni mji mzuri na mdogo usio kuwa na vurumai kubwa na ni shwari kabisa.

    Msikilizaji wetu mwingine Reginald David wa Chuo cha Magereza Kiwira, sanduku la posta 256, Tukuyu, Mbeya Tanzania ametuletea barua akitusalimu. Anasema kuwa Kiwira ni wazima, hofu yake ni kwetu sisi tulio mbali naye pamoja na wasikilizaji mbalimbali wa idhaa ya kiswahili popote duniani.

    Anasema dhumuni hasa la barua yake ni kutaka kutujulisha baada ya kimya cha muda mrefu bila ya kuwasiliana nasi kuwa, Msikilizaji wetu Ndugu Victor David Jacob alifariki dunia tangu tarehe 15/6/2003 siku ya alhamisi kwa ajali ya gari na kuzikwa siku iliyofuata,kwa hiyo kwa niaba ya familia ya Marehemu anasema hana budi ya kutujulisha sisi pamoja na wasikilizaji wenzake kupitia idhaa ya Radio China Kimataifa, kwani marehemu alikuwa na mawasiliano na Radio China kimataifa.

    Tunashukuru Bw David kwa taarifa hiyo, na sisi tunapenda kuwapa pole jamaa na marafiki waliofiwa na tunamwomboleza kwa dhati msikilizaji wetu Victor David Jacob,ni matumaini yetu kuwa mungu atailaza roho yake pema peponi.

    Msikilizaji wetu David Kakopar wa sanduku la posta 1054, Mkabogo, Kigoma, Tanzania ametuletea barua akitoa salamu na akiwa na matumaini kuwa watangazaji wa Radio China Kimataifa hatujambo. Anasema uzima na ndio furaha yake pamoja na wasikilizaji wote, na anatushukuru sana kwa moyo wa dhati kwa kuendelea kuwa pamoja na wasikilizaji.

    Bwana Kakopar anasema, makusudi yake katika barua hii moja kutushukuru na kutupongeza kwa kazi nzuri iliyojaa juhudi na maarifa katika kuandaa vipindi vyote. Pili anasema, tulimwahidi kumtafutia marafiki wa kalamu wanafunzi wanaosoma somo la Kiswahili chuo kikuu, anauliza mpango huo vipi? Wanafunzi hao wana pilikapilika za kuhitimu masomo na kukabiliwa na mtihani, kweli ni vigumu kumsaidia.

    Tatu anaipongeza serikali ya China na Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na ushirikiano wa kiuchumi kwa kuwaletea wakandarasi wa barabara, kilimo na maji mfano mradi wa maji wa ziwa Viktoria kupelekwa Shinyanga, barabara ya Kigoma Burundi kupitia Kalinzi ambako ndio Kata anayoishi,miradi yote hiyo imeshikwa na kandarasi ya China amefurahishwa na jinsi mkandarasi wa China anavyotengeneza barabara kwa ustadi na kwa moyo wa upendo. Anasema barabara hii itawaondolea kikwazo cha usafiri kati ya kijiji na mji wa Kigoma na Tanzania na Burundi.

    Nne naomba ni jinsi gani hawa wachina wanaojua Kiswahili wanavyoweza kufahamiana na yeye kama Komredi mwenzao. Anaomba tumwanzishie uhusiano kwa barua ya lugha ya Kichina.

    Kwa kweli habari aliyotuletea ni nzuri na imetufurahisha, tunamshukuru na ni matumaini yetu kuwa ataendelea kutuelezea hali kuhusu miradi hiyo.

    Na Bwana Kakopor anasema ana wasiwasi kuwa barua zake huwa hazitufikii,hali hii kwa kawaida haiwezi kutokea,labda tu kutokana na sababu fulani ambazo labda sisi sote hatuzifahamu. Sisi tunamuomba asiwe na wasiwasi andelee kutuandikia barua, kwani kama alivyosema kwa hali ya kawaida ni lazima tuzipate, kama tulivyoipata hii tunayoisoma.

    Pia anasema anaomba atumiwe tena jarida la The Messenger na China Today, na mwisho kabisa anatutakia kazi njema katika mwaka mpya wa Kichina 2004 Februari.

    Na Bwana Kakopar anasema,baadhi ya waafrika wa vijijini wamekuwa na tabia ya kuharibu mazingira yao kwa kuchoma moto vichaka na misitu yaani wanajitafuna kama punguani bila kujali athari ya kesho kwa hali ya hewa. Hivyo anaomba somo la moto na mazingira angalau tulifundishe kupitia radio na magazeti kwa watu wa dunia ya tatu.

    Kweli hifadhi ya mazingira ni kazi muhimu kwa binadamu wote,hata nchini China bado wako baadhi ya watu wa sehemu fulani ambao walikata miti ovyo,kuchafua mazingira na kutojua kuhifadhi hali asili ya maumbile. Hivi sasa serikali ya China inasisitiza zaidi suala la hifadhi ya mazingira,na wachina wa sehemu mbalimbali wamefanya juhudi za kupanda miti ili kuboresha mazingira,lakini bado kuna kazi kubwa zinazotakiwa kufanyika.

    Anasema pia kuwa alisema kwenye gazeti kwamba nchini China kuna watu 1.5 milioni wenye virusi ya ukimwi. Anauliza je kuna mikakati gani nchini China katika kupambana na tatizo hili la ukimwi. Kuhusu suala hili tafadhali aendelee kusikiliza maelezo yetu na kutembelea tovuti yetu.

    Bwana Kakopar anasema,China itaandaa michuano ya olimpiki ya mwaka 2008 na anatamani kuhudhuria kwenye mashindano hayo. Anatuomba tumshauri ajiandae vipi? Kuhusu jambo hili ni vigumu kwa sisi kumshauri,lakini tungependa kumwambia awasiliane na idara za michezo ya nchi yake ili aweze kupata ushauri kutoka kwa idara inayohusika.

    Bwana Kakopar pia anasema,China ni wanunuzi wa kahawa ya Tanzania, na yeye ni mkulima wa kahawa wa Chama cha ushirika Rumacoco. Wapo kwenye mtandao kwani wana TV na kompyuta. Anataka kujua watawezaje kupata wateja wa China na kujitangaza huko, kwani wanazalisha kahawa bora, na kikindi chao kilipata ushindi wa kuboresha kahawa Tanzania. Hapa tungependa kumkumbusha anuani yetu ya tovuti kwenye mtandao wa intrernet?www.cri cn.

    Anasema, Mwandishi wa habari Chen Lian Ying alikwisha tembelea Kenya, je mwandishi wa China atakuja lini Tanzania? Anasema anamkaribisha sana mwandishi yeyote wa idhaa ya Kiswahili atakaye tembelea Kigoma kaskazini ambako ni eneo la kijani, karibu sana.

    Idhaa ya Kiswahili 2004-03-28