Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-03-29 17:36:28    
Kijana mlemavu anayefanya mwujiza

cri

Bw. Xie Yanhong na kocha wake Bw. Ge Jie.

    Katika makala hii, tunakuleteeni maelezo kuhusu kijana wa ajabu, Bw. Xie Yanhong, aliyeogelea na kufanikiwa kuvuka mlangobahari wa Uingereza kwa kutumia saa 16 na dakika 44. Kijana huyo ni mlemavu asiyeweza kudhibiti mikono wala miguu. Lakini yeye ni mlemavu wa kwanza duniani aliyepata mafanikio ya kuvuka kwa kuogelea mlangobahari wa Uingereza, na mlangobahari wa Qiongzhou, ulio kusini mwa China.

    Kuvuka mlangobahari wa Uingereza kumekuwa ni ndoto ya watu wengi wanaopenda mchezo wa kuogelea. Tokea mwaka 1875 mpaka hivi sasa, kumekuwepo na watu zaidi ya elfu 6 ulimwenguni waliojaribu kuogelea na kuvuka mlangobahari wa Uingereza, lakini ni watu wapatao 800 tu ambao wamepata mafanikio, na miongoni mwa watu hao, hakuwepo mlemavu hata mmoja. Hata hivyo, Bw. Xie Yanhong kutoka Dalian, mji wa mashariki ya China, alivunja rekodi tarehe 24, mwezi Agosti, mwaka 2003, na kuwa mlemavu wa kwanza duniani aliyefanikiwa kuongelea na kuvuka mlangobahari wa Uingereza.

    Hivi karibuni, Bw. Xie alihojiwa na Radio China ya Kimataifa akiwa kwenye kiti cha magurudumu. Alipogusia kuvuka mlangobahari wa Uingereza, alisisimka sana.

    "Mimi ni mlemavu wa kawaida, lakini ninatamani mambo makubwa, nayo ni kuvuka mlangobahari. Sasa nimetimiza malengo mawili ya kuvuka mlangobahari wa Qiongzhou na wa Uingereza. Nina mpango wa kuvuka milangobahari mingine duniani, mmoja au miwili kila mwaka. Mafanikio yangu yanatokana na misaada kutoka kwa kocha wangu, pia kwa watu wengi wanaoniunga mkono."

    Mwaka huu Bw. Xie Yanhong ana umri wa miaka 36. Alizaliwa akiwa na ulemavu wa mikono na miguu, hivyo hawezi kusimama kwa miguu wala kushika vitu kwa mikono. Lakini tangu utotoni mwake, alikuwa na hamu kubwa ya kupata mafanikio katika shughuli zote. Alikuwa si kama tu anajitegemea katika maisha yake, bali pia amemaliza masomo ya sekondari ya juu kwa misaada ya jamaa na wanafunzi wenzake. Baadaye, ili kujitegemea yeye mwenyewe na wazazi wake, Bw. Xie alianzisha duka moja dogo katika maskani yake, Dalian, mji wa pwani, mashariki ya China. Na akaanza maisha ya kujitegemea.

    Alipokuwa na umri wa miaka 22, kwa msaada wa jamaa zake, kijana huyo aliogelea baharini kwa mara ya kwanza, na akaupenda mchezo huo unaompa hisia mpya na za uhuru. Kuanzia hapo, alikuwa anaogelea baharini kila alipopata nafasi, na kuendelea na mchezo wa kuogelea wakati wa siku za baridi kwa miaka 10 mfululizo. Hata hivyo, hatua kwa hatua, Bw. Xie alipata matatizo yaliyosababishwa na ulemavu wake, kwa vile, anaweza kutumia mikono peke yake, kwani miguu yake haifanyi kazi hata kidogo, hali ambayo imeathiri mwenendo wake wa kuogelea. Mwaka 2000, Bw. Xie aliyekuwa anatafutatafuta kocha, akawa mwanafunzi wa kocha wa kuogelea Bw. Ge Jie. Akihimizwa na kusaidiwa na kocha huyo, kipaji chake cha kuogelea kikaanza kujitokeza. Mwanzoni alikuwa anaweza kuogelea kwa mita 20 tu, lakini baada ya miezi miwili tu aliweza kumaliza kuogelea mita elfu 5 bila kupumzika.

    Akiwa na ulemavu mkubwa, maendeleo yoyote aliyopata Bw. Xie yametokana na jitahda za mara kwa mara kuliko watu wasio na ulemavu. Kocha wake Bw. Ge Jie aliandaa mpango maalumu kwa mwanafunzi huyo maalumu. Alisema,

    "Kwa vile ana uzito mkubwa zaidi pamoja na ulemavu, nilimtaka aongeze mazoezi ya kuogelea kwa masafa marefu, ili kuongeza uvumilivu na nguvu zake. Katika mazoezi, anafanya bidii kubwa kwa hiari."

    Baada ya mazoezi ya muda wa mwaka mmoja na nusu, Bw. Xie alikuwa alikuwa ana uwezo wa kuogelea urefu wa kilomita 3 kwa saa, ambapo mwendo wake unafanana na watu wasio na ulemavu.

    Kijana huyo alikuwa na hamu ya kuonesha uwezo wake baada ya kupata maendeleo hayo. Lakini katika mashindano ya walemavu, hakuna shindano la kuogelea kwa ngazi yake. Ndiyo maana, alishauriana na kocha yake kuhusu kuvuka mlangobahari kwa kuogelea.

    Mwaka 2002, Shirikisho la kimataifa la kuogelea liliandaa shindano la kuvuka mlangobahari wa Qiongzhou, kusini mwa China, na Bw. Xie Yanhong alitoa ombi la kushiriki kwenye shindano hilo. Lakini ombi lake lilikataliwa kutokana na afya yake. Hata hivyo, hakufa moyo, na akapata mafanikio ya kuogelea na kuvuka mlangobahari wa Qiongzhou tarehe 4, Juni mwaka 2003.

    Mafanikio hayo yalimpa moyo sana, ambapo aliweka lengo la kushinda kuvuka mlangobahari wa Uingereza.

Bw. Xie Yanhong alipoogelea na kuvuka mlangobahari wa Uingereza.

    "Mlangobahari wa Uingereza ni changamoto kubwa kwa mashabiki wa kuogelea kwa masafa marefu. Mimi nina ulemavu, nataka kuogelea kuvuka mlangobahari huo kwa lengo la kuwapa wengine nguvu na kuwaonesha moyo wa walemavu wa China wa kupenda maisha."

    Mlangobahari wa Uingereza hujulikana kwa maji baridi na mikondo ya maji inayobadilika sana. Hayo ni matatizo makubwa kwa watu wasio na ulemavu, lakini Bw. Xie mwenye ulemavu mkubwa alikata shauri na kuyashinda. Aliongeza mazoezi, ambapo mbali na zoezi la kawaida la kuogelea kwa mita elfu 10 kila siku, aliogelea kwenye bahari yenye mazingira yanayofanana na yale ya mlangobahari wa Uingereza, ili kuinua uwezo wa kujikinga na baridi na mikondo ya maji. Ushujaa wake ukazaa matunda, na alivuka mlangobahari wa Uingereza na kufanya mwujiza.

    Alipohojiwa baada ya kupata mafanikio hayo, alisema kuwa, "Maji ni baridi kweli katika mlangobahari wa Uingereza, lakini moyo wangu ni wenye ujoto unaotokana na watu wengi wanaotufuatilia sisi walemavu na uungaji mkono wao umenipa moyo."

    Bw. Xie anapenda kutoa wito kwa walemavu wote ulimwenguni kupitia Radio China Kimataifa, anasema, "Sisi walemavu popote duniani ni sawa, haifai tujisikie kuwa tumeachwa na jamii, bali jamii inatuhitaji, inapenda sisi tuishi kwa moyo imara na upendo. Tuone kuwa, si lazima tupokee misaada kutoka kwa watu wasio na ulemavu, bali pia na sisi tuwape misaada fulani, na sisi tuko sawa."

Idhaa ya Kiswahili 2004-03-29