China ni nchi yenye makabila mengi, ambapo kabila la Han ndilo lenye watu wengi kabisa, zaidi ya aisilimia 90 ya wananchi wote, na pia yapo makabila mengine 55, ambayo kwa desturi yanaitwa makabila madogo madogo kutokana na kuwa na watu wachache.
Katika mtaa wa Niujie, wanaishi watu wapatao elfu 50 kutoka makabila 22 madogo madogo. Miongoni mwao, zaidi ya elfu 10 ni wakazi wa kabila la Hui, kwa hivyo mtaa huo unachukuliwa kama maskani ya Wahui, ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu. Tunaweza kupata sura ya jumla ya mtaa huo kutokana na jina lake, Niujie, maana yake ni barabara ya ng'ombe, kwa vile nyama ya ng'ombe ndiyo chakula muhimu cha Waislamu.
Tukiondoka Xidan, eneo maarufu la biashara hapa mjini, na kuelekea kusini, tunakuta majengo ya rangi manjano yaliyopambwa na mistari ya kijani, huo ndiyo mtaa wa Niujie. Tunafika kwenye barabara kuu ya mtaa huo yenye urefu wa mita 600 na upana wa mita 40, ambapo miti 43 ya kale ipo kando pamoja na msikiti wa Niujie ambao ni maarufu sana, na maduka mbalimbali yanayowahudumia hasa Waislamu, yakiwemo ya nguo, chakula na kazi za mikono. Mtaa wa Niujie umenipa sura pana na safi, na maisha ya hapa ni ya maufaa.
Lakini Niujie ya miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa na barabara nyembamba na majumba mabovu yaliyochanganyika bila ya mpangilio. Kabla ya mwaka 1997, kulikuwepo jumla ya mita za mraba laki 3 na elfu 40 ya majumba yenye ghorofa moja pekee ambapo yalikuwa kongwa na mabovu, na kwa wastani kila mkazi wa mtaa huo alikuwa na eneo lenye mita 5 za mraba tu. Katika jitihada za kuboresha mazingira ya kuishi katika mtaa wa Niujie, serikali ya Beijing ilianzisha mradi wa bomoa bomoa mwaka 1997, ambapo wakazi walipewa makazi ya muda na majumba yao mabovu kubomolewa. Baada ya kujengwa majumba mapya wakaza wataweza kurejea kwenye mtaa huo wa Niujie. Hivi sasa, kipindi cha kwanza cha mradi huo kimekamilika, na familia zipatazo elfu 3 na mia 3 zimehamia kwenye makazi mapya kwa furaha. Kipindi cha pili, ambacho pia ni cha mwisho cha mradi huo kinatazamiwa kumalizika mwaka kesho, ambapo familia zote za Mtaa wa Niujie zitaweza kuishi katika majumba mapya.
Sasa hebu tunakwenda tukawatembelee baadhi ya wakazi wa mtaa huo. Mzee Feng Guanying mwenye umri wa miaka 70 ameishi katika mtaa wa Niujie kwa karibu nusu karne. Hivi karibuni, alihamia kwenye makazi mapya, anasema akiwa na msisimko, "Hapo mwanzoni, familia yangu yenye watu wanne, tuliishi katika nyumba moja yenye eneo la mita 16 za mraba tu. Sasa tuna nyumba yenye mita za mraba 74, ambapo kuna vyumba viwili vya kulala. Tumepata manufaa kweli, tuna vipasha joto katika majira ya baridi na kutumia kiyoyozi katika majira ya joto. Maisha ya sasa na ya mwanzoni hayawezi kulinganishwa."
Mzee huyo anaeleza kuwa mradi ulioandaliwa na serikali ya Beijing umeleta mabadiliko makubwa katika mtaa huo wa Niujie, hususan manufaa kwa wakazi wa kabila la Hui, ambao ni asilimia kubwa miongoni mwa wakazi wa mtaa huo.
Watu wa kabila la Hui ni waumini wa dini ya Kiislamu, ambapo hufanya ibada kila siku, kwa hivyo, wanatembelea mara kwa mara msikiti wa Niujie.
Ujenzi wa msikiti huo ulianza mwaka 996, ambapo China ilitawaliwa na mfalme wa enzi ya Song, baada ya upanuzi na ukarabati wa mara kwa mara katika miaka elfu 1 iliyofuata, msikiti huo sasa ni maarufu sana miongoni mwa Waislamu wa China wanaoishi katika sehemu ya kaskazini ya nchi hiyo. Tangu kuanzishwa kwa China mpya, serikali kuu ya China ilitenga fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa tatu wa msikiti huo. Hivi sasa, una eneo la mita za mraba elfu 6.
Imamu Yin Guofang wa msikiti wa Niujie anapohojiwa anasema, "Katika msikiti wa Niujie, kuna ibada tano kila siku, zinazowashirikisha waumini wapatao 100 hadi 150 kila mara. Idadi hiyo inaweza kufikia watu 700 hadi 800 katika ibada za siku ya Ijumaa."
Hivi sasa, msikiti wa Niujie umepitia historia ya zaidi ya miaka elfu moja, hata hivyo majengo yake mbalimbali yamehifadhiwa barabara, ambayo pia ni mfano mzuri wa mchanganyiko wa mitindo ya ujenzi wa kasri za kale za China na misikiti ya kiarabu.
Bw. Wei Chunjie ni mtumishi wa msikiti huo. Anafurahia kutuambia kwamba, msikiti huo ulikuwa wa kwanza kupewa huduma za gesi katika mtaa mzima wa Niujie katika sikuu za baridi mwaka 2001, hivyo wanaweza kutumia gesi, ambayo ni nishati safi sana, katika kuchemsha maji, kupika na kupata joto.
Kutokana na mpango wa serikali ya mji wa Beijing, fedha za Renminbi milioni 20, sawa na dola za kimarekani milioni 2.5, zitatumiwa kwa ajili ya kukarabati majengo mbalimbali ya msikiti na kupanua eneo la Waislamu wanawake kufanyia ibada. Aidha, mpango wa kuboresha zana za maji, umeme na hifadhi za vitu vya kale pia upo.
Mtumishi wa ofisi ya mambo ya kikabila na kidini ya manispaa ya Xuanwu, mijini Beijing, Bibi Ma Fenfen anasema, "Tunafuatilia maoni ya wananchi Waislamu na kujitahidi kukidhi matakwa yao, kwa ajili ya kuwaletea mazingira mwafaka."
Mzee Feng Guanying baada ya kuarifiwa mpango wa ukarabati wa msikiti wa Niujie, anafurahi sana, na kutuambia kwamba, Waislamu wa mtaa wa Niujie wanaisubiri siku hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-04-16
|