Mbarouk Msabah
P.O.Box 52483, Dubai, U.A.E
Nikiwa kama ni Mtanzania, ningependa kuchukua fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa maadhimisho ya kutimia miaka 40 tangu ulipoanzishwa uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya Watu wa China na nchi yangu Tanzania.
Kwa kweli Watanzania wote wanaona fahari kubwa sana juu ya maadhimisho hayo, kwani uhusiano wa kirafiki na kindugu kati ya China na Tanzania umekuwa na historia ya muda mrefu tangu pale nchi yetu ndio kwanza imejipatia uhuru wake.
Licha ya kwamba Mwenyekiti Mao Zedong muasisi wa Jamhuri ya Watu wa China aliwahi kufanya ziara nchini Tanzania katika miaka ya mwanzo ya uhuru wetu, China ilikuwa ni moja kati ya mataifa ya mwanzo kabisa yaliokuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania katika kujenga mustakabala wake wa baadaye, pamoja na kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.
Moja kati ya juhudi kubwa zilizofanywa na Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania ni ujenzi wa Reli ya "TAZARA" iliyounganisha bandari ya Dar es Salaam hadi nchini Zambia. Hatua ambayo imesaidia sana kukuza maendeleo ya kiuchumi katika eneo zima la Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika. Vile vile China imekuwa ikisaidia sana katika ujenzi wa viwanda, barabara, hospitalim na maeneo mbalimbali ya kiserikali na kiraia nchini Tanzania tangu miaka ya sitini hadi hii leo. Pia wataalamu wa kichina wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega na Watanzania katika sekta za huduma mbali mbali za kijamii, jambo ambalo limekuwa nikishukuriwa mno na Watanzania.
Ni vigumu kueleza yale yote ambayo yamepelekea uhusiano wetu na Jamhuri ya Watu wa China kuimarika katika misingi ya kusaidiana kidugu na kirafiki kwa maslahi ya pande zote mbili.
Watanzania na Wachina wana kila sababu ya kufurahia siku ya kuadhimisha mika 40 tangu pale waliposhikana mikono na kuanza urafiki wao.
Mwisho ningependa mpokee shairi langu maalumu nililolitnga kwa ajili ya maadhimisho ya mika 40 tangu ulipoanzishwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, shairi hilo linaitwa: "Udumu urafiki China na Tanzania".
Udumu Urafiki China na Tanzania
Ni miaka arobaini, sasa imeshatimia
Sote tusheherekeni, China na Tanzania
Tujae matumaini, urafiki utaendelea
Udumu urafiki, China na Tanzania.
Furaha haisemeki, leo tunafurahia
Umedumu urafiki, China na Tanzania
Kamwe hautetereki, wazidi kushamiria
Udumu urafiki, China na Tanzania.
Tangu enzi za uhuru, China ilijitolea
Ilikua kama ni nuru, inayo tuangazia
Nasi uwaishukuru, juhudi imechukua
Udumu urafiki, China na Tanzania.
Tuliotesha mbegu, nakisha kuipalilia
Kwa uwezo wa Mungu, ikaota na kuchanua
Leo sote ni kama dungu, Wachina na Watanzania
Udumu urafiki, China na Tanzania.
China ni kipenzi chetu, Watanzania twajivunia
China ni rafiki yetu, vyema twamtambua
China ndiye mwenzetu, mikono twamshikilia
Udumu urafiki, China na Tanzania.
Idhaa ya Kiswahili 2004-04-20
|