Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-04-27 22:20:35    
Mwaka wa Kima wavutia watu wa duniani

cri

            

 Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483, Dubai, U.A.E ametuletea barua pamoja na picha yake moja akieleza kuwa, "Mfalme kima ni hadhithi ya kuvutia ya kichina"

    Ikiwa mwaka huu wa 2004 ni mwaka wa alama ya mnyama "kima" kwa mujibu wa kalenda ya kijadi ya kichina, kwa kweli kima amekuwa ni mmoja katika wanyama wenye umaarufu mkubwa nchini China.

    Simulizi za hadithi mbalimbali za kikale nchini China, zimekuwa zikielezea mengi kuhusu taswira ya kumtumia kima katika simulizi zake, hata opera maarufu za kichina kama vile "opera ya kibeijing" ambayo ndio opera ya kitaifa ya China, imekuwa ikitumia hadithi kuhusu kima katika uigizaji wake, kama vile hadithi maarufu ya "Mfalme Kima" iliyoandikwa na mwandishi mashuhuri wa kichina katika enzi za utawala wa Ming Bw. Wu Cheng'en.

    Nilivutiwa zaidi na simulizi za "Mfalme Kima" pale nilipokutana uso kwa uso na mwigizaji wa ngoma za kitamaduni za kichina katika banda la kibiashara la China, kwenye maonesho ya kibiashara ya kila mwaka hapa mjini Dubai yenye kuwashirikisha washiriki kutoka mataifa mbali mbali ya dunia, yaliyoanza tarehe 15 Januari na kumalizika tarehe 15 Februari mwaka huu wa 2004.

    "Samahani Bwana, naomba kupiga picha ya ukumbusho na wewe!" hivyo ndivyo nilivyoanza kumwomba mwigizaji mmoja wa kichina aliyejichora usoni mwake mithili ya sura ya kima kwa rangi nyekundu na nyeupe pamoja na michoro midogo midogo miembamba pembeni yake, huku akiwa amevaa nguo ndefu mpaka chini yenye rangi ya dhahabu na iliyojaa nakshi za kupendeza. "Oh!" muigizaji huyo alishusha pumzi na kucheka, na baadaye kuniambia "Bila ya taabu rafiki yangu", hapo ndipo nilipopata bahati hiyo ya kupiga picha na mwigizaji huyo wa kichina wa hadithi ya "Mfalme Kima" ambaye pamoja na waigizaji wengine, alikuwa akionesha ustadi wake jukwaani mbele ya mamia na maelfu ya watu waliojazana kila siku katika banda la kibiashara la China kwa kipindi chote cha mwezi mzima wa maonesho hayo ya kila mwaka ya kibiashara mjini Dubai.

    Ni wazi kabisa alama ya "Mfalme Kima" ni mojawapo ya alama zinazogombea kuchaguliwa kuwa "nembo" rasmi itakayowakilisha mashindano ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 nchini China, hivyo naitakia kila la kheri na mafanikio alama hiyo, ili hatimaye kamati ya China ya kuchagua nembo itakayotumika katika michezo hiyo, itafikia uamuzi wa kuiteua alama ya "Mfalme Kima", kwani kwa kweli itawavutia watu wengi kote duniani, mimi nikiwa mmoja wapo.

    Bwana Mbarouk Msabah ametuelezea hadithi nzuri ya kufurahisha, tuliposoma barua yake na kutazama picha aliyotuletea, tulifurahi sana, na picha yake hiyo ya kupendeza tutaiweka kwenye tovuti yetu, ili kuwafurahisha wasikilizaji wengine wote. Tunamshukuru kweli Bwana Msabah kwa maelezo yake mazuri.

    Katika barua yake nyingine Bwana Mbarouk Msabah pia anasema kuwa, angependa kutoa pongezi zake za dhati kwa uongozi wa Radio China Kimataifa kwa Idhaa hii ya Kiswahili kutokana na kuanzisha kwa tovuti yake hapo mwishoni mwa mwaka jana.

    Anasema, kwa kweli anashindwa hata kuielezea furaha yake kuhusu jambo hilo, kwani baada ya kuitembelea tovuti hiyo katika mtandao wa Internet alivutiwa nayo sana licha ya kwamba alikuwa akiyapata matangazo yetu hapo kabla kwa kutumia tovuti ya CRI on line Radio 4U.

    Anasema, njia hiyo ya kuanzisha tovuti maalumu kwa ajili ya Idhaa ya Kiswahili itawasaidia sana wasikilizaji wetu wanaoishi nje ya eneo la Afrika Mashariki na Kati kuweza kuyasikiliza matangazo yetu katika hali ya usikivu mzuri na wakati mwafaka kutokana na shughuli zao za kikazi, kwani hata akiwa kazini hutembelea tovuti yetu na kusikiliza vipindi vyetu pamoja na kusoma makala mbalimbali ambazo zinakuwepo ndani ya tovuti hiyo.

    Kwa njia hiyo, bila shaka yoyote Radio China Kimataifa itazidi kupata umashuhuri na kuweza kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi kila pembe ya dunia ambako wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili wanapatikana. Yeye akiwa miongoni mwa wasikilizaji wetu kwa zaidi ya miaka 16 sasa angependa kutoa shukrani zake nyingi kwetu kutokana na juhudi zetu za kukuza urafiki, maelewano na udugu kati ya China na Mataifa mengine, kwani Radio China Kimataifa daima imekuwa ni daraja linalowaunganisha Wachina na Walimwengu kwa misingi ya kuleta uwelewano kwa watu tofauti.

    Mwisho angependa kuwasilimia Dada Chen, Bw. Fadhili Mpunji pamoja na watangazaji wote wa Radio China Kimataifa. Na sisi tunamshukuru sana kutembelea tovuti yetu kwenye mtandao wa internet. Na kutokana na nguvu kazi ambazo bado hazijatosha katika idhaa yetu, bila shaka bado kuna dosari kadhaa katika tovuti yetu, hata kuna makosa fulanifulani katika tafsiri zetu, ni matumaini yetu kuwa Bwana Mbarouk Msabah na wasikilizaji wetu wengine watatoa maoni na mapendekezo ya kutusaidia kufanya vizuri zaidi tovuti yetu ili kuwavutia zaidi wasikilizaji.

    Tunapenda kuwakumbusha tena wasikilizaji wetu kuwa, tarehe 26 Aprili itakuwa siku ya maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania, kuanzia tarehe 23 hadi 29 mwezi huu tutawaletea wasikilizaji wetu kipindi maalum cha maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Msikose kutusikiliza.

Idhaa ya Kiswahili 2004-04-27