Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-03 20:10:31    
Lugha ya Kitibet yahifadhiwa

cri

    Nchini China kuna makabila 56, na miongoni mwa makabila hayo, mengi yana lugha yao. Hivi karibuni, waandishi wetu wa habari walitembelea huko Tibet wakaelewa kwa kina jinsi lugha ya Kitibet inavyohifadhiwa na kuenziwa. Ifuatayo ni ripoti waliyotuletea:

    Tulipoingia tu mkoani Tibet mara tukajikuta tuko katika dunia ya lugha ya Kitibet, kwani huko sio tu kuna mbingu buluu, milima yenye theluji na nyumbu, bali pia kuna utamaduni wa Kitibet wenye historia ndefu ikiwa ni pamoja na lugha na maandishi yake ya ajabu ajabu.

    Mkoani Tibet, ukifungua redio utasikia matangazo kwa lugha ya Kitibet, ukiwasha televisheni utaona vipindi vya lugha ya Kitibet, ukienda shuleni utasikia sauti ya watoto wakisoma kwa sauti kwa lugha ya Kitibet, na ukitembea barabarani utaona majina na matangazo ya bidhaa mbele ya maduka kwa maandishi ya Kitibet na ya Kichina, na hata ukisafiri kwa teksi pia utaweza kusikia nyimbo zikiimbwa kwa lugha ya Kitibet.

    Mmoja wa wafanyakazi katika Kituo cha Redio cha Tibet, Sunandajie alitueleza, "Kitibet ni lugha yetu tuliyozaliwa nayo, tunaitumia katika maisha yetu na kazi zetu. Nikiwa nyumbani napendelea kuangalia televisheni na kusikiliza redio kwa lugha ya Kitibet. Kitibet ni lugha inayotusaidia kufahamu mambo makubwa ya ndani na nje ya nchi na sera mbalimbali za nchi yetu."

    Tunafahamu kwamba asilimia 92 ya watu wa mkoani Tibet wanawasiliana kwa lugha ya Kitibet. Mfasiri wa lugha ya Kitibet Cidanwanjiu, alitueleza kuwa maandishi ya Kitibet yana historia ya miaka 1300, ni moja kati ya maandishi yenye historia ndefu duniani. Anaona kwamba kuhifadhi na kuendeleza lugha hiyo kuna maana kubwa katika kueneza elimu, kuendeleza uchumi na jamii na kuhifadhi historia ya Tibet. Alisema, "Serikali za awamu zote zinatilia maanani sana kazi ya uhifadhi wa lugha ya Kitibet na zinajitahidi kutekeleza sera kuhusu lugha za kikabila, kuhakikisha uhuru wa kuzitumia na kuendeleza lugha hizo. Kadhalika, kutokana na hali ilivyo zilichukua hatua nyingi ili maandishi ya Kitibet yapate maendeleo makubwa."

    Imefahamika kwamba, ili kuendeleza lugha ya Kitibet kwa mpango, katika miaka ya 80 ya karne iliyopita Mkoa Ujiendeshao wa Tibet ulianzisha ngazi tatu za idara yaani ya mkoa, ya miji na ya wilaya ili kuongoza shughuli za lugha ya Kitibet na kutafsiri kutoka Kichina, na "kanuni za kujifunza, kutumia na kuenzi lugha ya Kitibet" zimetolewa. Kanuni zinasema maandishi ya lugha ya Kitibet na lugha ya Kichina zinaheshimika sawa kisheria, kwa hiyo matumizi ya lugha ya Kitibet yamehalalishwa kisheria.

    Naibu mkurugenzi wa Kamati ya Mwongozo wa Kazi ya Lugha ya Kitibet mkoani, Bw. Danbachuda alisema, hivi sasa iwe ni katika shughuli za serikali au katika maisha ya kawaida, lugha ya Kitibet inatumika sana. Aliongeza kusema kwamba nyaraka za serikali lazima ziwe zimetafsiriwa kwa Kitibet na kuzitawanya zikiambatana na nyaraka za Kichina. Tungo za wasanii mkoani Tibet nyingi ni za lugha ya Kitibet, vyombo vya habari vingi vinatumia lugha hiyo katika matangazo ya redio, televisheni na magazeti. "Gazeti la Kila Siku la Tibet" lina kurasa 36 za lugha ya Kitibet. Zaidi ya hayo, lugha ya Kitibet pia inatumika katika shughuli za mahakama, utafiti wa kisayansi, posta na mambo ya upashanaji habari.

    Mtaalamu anayeshughulika na utafiti wa lugha ya Kitibet kwa miaka mingi, Danbachudashen, alituambia kwa msisimko, "Hapo zamani, kabla ya Tibet kukombolewa, waliofahamu maandishi ya Kitibe walikuwa asilimia 5 tu, Watibet wengi walikuwa hawakufahamu kusoma wala kuandika. Lakini hivi sasa, jamii imebadilika kabisa, Watibet wametia bahati yao mikononi mwao wenyewe, ndipo lugha hiyo imekuwa chombo chao hasa cha mawasiliano na masomo."

    Aliendelea kutufahamisha kuwa utafiti na mafundisho ya lugha ya Kitibet yanaendelea kwa kina na upana zaidi. Lugha hiyo sio tu imekuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi na za sekondari, bali pia inatumika katika chuo kikuu cha Tibet. Kutokana na jinsi tovuti ya kompyuta inavyoenea, maandishi ya Kitibet pia yameingia kwenye internet, na kuwa mojawapo katika katika maingiliano ya kimataifa.

    Aidha, tumeelewa kwamba sambamba na matumizi ya lugha ya Kitibet, Watibet pia wanathamini sana matumizi ya Kichina na lugha nyingine za ng'ambo. Bi. Dechingbaichen aliyehitimu katika chuo kikuu na kushiriki kazini hivi karibuni alisema, "Lugha ni chombo cha mawasiliano. Kutokana na jamii ya kisasa kuendelea haraka, mawasiliano yanahitajika sana kati ya mataifa, kanda na kazi. Lakini mawasiliano hayo yakitegemea lugha moja tu ya Kitibet yatakwamisha mawasiliano, kwa hiyo mkoani Tibet masomo ya kujifunza Kichina pamoja na lugha nyingine za nchi za nje yamekuwa ya watu wengi."

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-03