Zhang Xiuming ni mkulima anayeishi katika kijiji kimoja cha milimani cha wilaya ya Xiji cha mkoa ujiendeshao wa kabila la Wahui wa Ningxia, kaskazini magharibi mwa China. Kwa vizazi vingi, yeye na wanakijiji wengine wanaishi milimani wakilima katika ardhi zisizokuwa na rutuba, maisha yao ni ya kujilisha tu, siku zote wanaishi kwenye nyumba za udongo, hawajawahi kufikiria hata ndotoni kwamba, iko siku wataacha nyumba za udongo na kujenga nyumba za matofali na vigae.
Lakini sasa maisha yake yamebadilika, akitazama nyumba mpya iliyojengwa kwa matofali na vigae,Zhang Xiuming mwenye umri wa miaka 56 alitabasamu kwa furaha akisema kwamba,tangu binti yake aondoke nyumbani kufanya kazi katika kiwanda cha mkoa wa Fujian, wamepata pesa za kujenga nyumba mpya .
Kama binti wa Mzee Zhang Xiuming alivyofanya, chini ya msaada wa serikali ya huko, wakulima wengi zaidi na zaidi wa vijijini wameondoka makwao na kutafuta ajira nje, wanafanya kazi kwa bidii ili kubadilisha maisha ya familia zao ambayo yalikuwa ya hali duni.
Kwa mujibu wa takwimu, mwaka jana kwa jumla mji wa Guyuan ilitoa watumishi zaidi ya laki 5, na kuleta mapato ya yuan za Renminbi milioni 637, ambapo mapato ya wastani ya kila mtumishi yalikuwa yuan za renminbi 1211. Na kila mkulima wa mji huo alipata faida ya yuan za renmingbi 375 kwa wastani,mapato hayo yalichukua theluthi moja ya mapato yao yote ya mwaka nzima.
Mzee Zhang alimwambia mwandishi wa habari kwa furaha kwamba, mwanzoni alimruhusu binti yake kufanya kazi katika mkoa wa Fujian, kusini mashariki ya China kutokana na kuiamini serikali, na hasa ni kwa sababu ya umaskini wa kwao. Lakini kitu kilichomfurahisha ni kwamba, mwaka wa kwanza binti yake aliletea nyumbani yuan za renmingbi 2000, fedha hizo zinalingana na mapato ya miaka 10 ya familia nzima kwa kulima mashamba, sasa mtoto wake wa kikume pia ameenda Fujian kufanya kazi.
Mkoa ujiendeshao wa kabila la Wahui wa Ningxia ni mmojawapo wa mikoa mitano ijiendeshayo ya makabila madogo madogo nchini China, pia ni mkoa pekee wa kabila la wahui. Ina watu milioni 5.8, ambao theluthi moja ya watu wake ni wa kabila la wahui. Sehemu ya Xihaigu iliyoko kusini mwa mkoa ujiendeshao wenyewe wa kabila la wahui wa Ningxia ni maskini sana kutokana na ukame na milima mirefu. Hali yake ya uchumi ni mbaya sana, vifaa vya kilimo ni vya duni,wakulima wa hapa wanapaswa kupambana na mazingira mabaya kwa moyo shupavu kizazi hadi kizazi.
Ili kuwasaidia wakulima kupunguza umaskini, kuanzia kati kati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya sehemu ya Xihaigu ya mkoa wa Ningxia ilijaribu kuwasaidia wakulima kutafuta kazi katika sehemu za pwani zilizoendelea. Ilianzisha vituo vya kusaidia watu kufanya kazi njie, kuwaandaa wakulima ufundi, na kuunda chombo maalum kilichoshughulikia upashanaji wa habari, kuhifadhi haki na maslahi ya wakulima, hata kutenga fedha maalum kwa kuwasafirisha wakulima kwenda miji kufanya kazi.
Ding Hufeng ni mkulima wa kabila la wahui kutoka wilaya ya Xiji, aliwahi kufanya kazi nje kwa miaka minne, halafu alirudi nyumbani kuanzisha kiwanda chake mwenyewe kwa mitaji na ufundi aliojifunza nje. Baada ya kuendesha kiwanda chake kwa miaka mitatu, ametajirika haraka, na sasa amekuwa mwanakiwanda maarufu nyumbani kwake. Alisema kwa furaha kuwa, hawezi kufikiria hata ndotoni kwamba, mkulima wa milimani kama yeye naweza kujipatia mali nyingi katika muda mfupi wa miaka mitatu.
Mkuu wa tarafa ya Jiangtai ya wilaya ya Xiji Bw. Wu Jianxun alisema kuwa, kuwasaidia wakulima kuondoka milimani na kufanya kazi nje, matokeo yake ni mazuri sana, siyo tu kuongeza mapato ya wakulima, kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kisehemu,bali pia kubadilisha mawazo ya jadi ya kujifunga na hali duni ya maisha.
Idhaa ya Kiswahili 2004-05-06
|