Mbarouk Msabah wa P.O.BOX 52483, Dubai, United Arab Emirates anasena kuwa Mwaka 2008 ambao utakuwa ni wenye pirika pirika nyingi nchini China kwa vile utakuwa ndio mwaka wa mashindano ya michezo ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika mjini Beijing, pia itakuwa ni moja kati ya fursa muhimu sana kwa nchi yenu katika kuionesha dunia juu ya ufanisi wa kimaendeleo uliokwishafikiwa na Jamhuri ya Watu wa China tangu kuasisiwa kwake.
Bila shaka yoyote maadalizi ya michezo mikubwa kama ya Olimpiki inayowashirikisha wanamichezo mashuhuri na hodari kutoka kila pembe ya dunia, yanahitaji muda mrefu, juhudi kubwa pamoja na gharama za mamilioni ya fedha ambazo zitahitajika kuandaa nyenzo muhimu kama vile kujenga viwanja vya michezo, hoteli na nyumba za kufikia maelfu kwa maelfu ya wageni pamoja na mifumo mizuri ya mawasiliano ambayo itatumika kuwaunganisha mamilioni ya watu kote ulimwenguni katika muda wote utakaokuwa ukifanyika mashindano hayo.
Ni wazi kabisa China itakuwa na fursa nzuri ya kutangaza maendeleo yake ya kiviwanda, sayansi na teknolojia kwa njia za kibiashara kwa kutumia michezo hiyo ya Olimpiki. Kwani tumekuwa tukishuhudia nchi kama Japan na Korea ya Kusini ikiyatangaza mashirika yake ya vyombo vya Elektroniki kama vile SONY na SAMSUNG kwa kutumia njia kama hizo, jambao ambalo limeweza kuleta faida kubwa kwa mashirika mbali mbali ya kibiashara katika nchi hizo.
Ulimwengu unafahamu kwamba China tayari imeshafikia kiwango kikubwa cha utengenezaji na uzalishaji wa bidhaa na vitu mbali mbali vyenye teknolojia ya juu kabisa ya kisayansi ambavyo tayari vimeshasambaa katika masoko kote duniani. Shauku na hamu yetu kubwa ni kuona kwamba michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 nchini China itakuwa ni kama njia mojawapo ya nchi yetu kuonesha "misuli" yake ya kibishara inayozidi kukua na kupanuka kila siku zinavyoendelea kusonga mbele, kwani kufanya hivyo kutasaidia sana makampuni mbali mbali nchini China kujipatia sifa na umashuhuri mkubwa kwa bidhaa zake kote ulimwenguni, jambo ambalo sio tu litafanya michezo hiyo ya Olimpiki kufana na kunawiri mno bali pia kutaongeza sana kiwango cha biashara ya nje nchini China.
Mwisho ningeiomba Radio China Kimataifa kuwa mstari wa mbele katika kuwajulisha wasikilizaji wake hatua mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Jamhuri ya Watu wa China katika maandalizi ya mashindano hayo muhimu kabisa ya kimichezo hapa duniani yanayofanyika kila baada ya miaka 4. Na ni matumaini yetu makubwa kwamba CRI itakuwa ikichukua juhudi kubwa kuwaridhisha wasikilizaji wake juu ya mwenendo mzima wa kufanyika kwa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 nchini China.
Nakutakieni kila la kheri na mafanikio katika kutuandalia vipindi na makala mbali mbali juu ya michezo hiyo yenye kusisimua na kusubiriwa kwa hamu na shauku kwa na mamilioni ya watu kote ulimwenguni.
Nilipofungua tovuti yenu katika mtandao wa Internet mnamo tarehe 19 Aprili mwaka huu, nilivutiwa mno na khabari za kufaulu kwa majaribio ya urushaji wa satlaiti mbili ndogo za uchunguzi wa kisayansi ziitwazo; "Satlaiti ya Majaribio NO. 1" na "Satlaiti ya Naxing NO. 1" kwenye kituo cha Xichang nchini China hapo tarehe 18 Aprili mwaka huu wa 2004.
Kwa kweli ufanisi wa majaribio hayo ya kisayansi, ambayo yameweza kufanikiwa kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na mabingwa wa fani za utengenezaji wa urushaji wa vyombo vya anga wa kichina, unaonekana kama ni ushahidi mwengine uliowazi kabisa wa kukua kwa teknolojia hiyo nchini China, baada ya tukio la kihistoria la mwezi wa Oktoba mwaka jana 2003 la kumtuma mwanaanga wa kwanza kabisa wa Kichina Bw. Yang Liwei katika anga za juu ndani ya chombo kilichotengeneza na Wachina wenyewe.
Nilifungua ukurasa huo ndani ya tovuti ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa na kuisoma kwa makini khabari hiyo ya kusisimua pamoja na kutazama picha nzuri zilizoonesha jinsi ya satlaiti hizo zilivyokuwa zikielekea angani pamoja na picha za wanasayansi waliojaa furaha katika kituo cha Xichang baada ya kufaulu kwa safari za satlaiti hizo mbili.
Ama kweli kuanzishwa kwa "tovuti" yenu hiyo kuntuletea manufaa makubwa sisi wasikilizaji wa Radio China Kimataifa, ambao tumekuwa tukitegemea sana njia za mtandao wa Internet kusikiliza matangazo yenu pamoja na kusoma khabari za matukio mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kisayansi yanayojiri nchini China na kwengineko duniani.
Bila shaka, juhudi munazozichukua katika kuifanya tovuti yenu hiyo iwe ni ya kuvutia, kupendeza na kusisimua pamoja na kuwanufaisha wasikilizaji wenu, zinaonekana kuonesha matunda yake ya mafanikio katika kipindi kifupi tu cha chini ya miezi 6, jambo ambalo linafaa kupewa sifa ya kipekee na lifuatalo ni shairi langu fupi la beti 3 linaloelezea sifa juu ya "tovuti" ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa:
Naingia uwanjani, Tovuti kuisifia
Mlo mbali sogeeni, Mpate kunisikia
Tovuti yenye dhamani, Sasa imeshaingia
Mtandao ingieni, Mpate kujionea
CRI funguweni, Kiswahili kuchagua
Faida jipatieni, Na mengi ya kusisimua
Kuingia mitamboni, Tovuti kuivumbua
Nasi twakushukuruni, kazi yenu ni murua
Watangazaji hongereni, Juhudi mumechukua
Idhaa ya Kiswahili 2004-05-18
|