Katika majira ya Spring mwaka 2000, upepo mkubwa uliovuma ulisababisha kuweko kwa mavumbi angani ambayo yalitambaa katika sehemu nzima ya kaskazini ya China, Beijing ilikuwa sehemu moja iliyoathiriwa vibaya na vumbi hilo, ambapo watu waliweza tu kuona vitu vilivyoko karibu na mita 100. Upepo huo uliopeperusha vumbi si kama tu uliathiri maisha ya wakazi, bali pia ulisababisha uchafuzi mkubwa kwa mazingira. Hali hiyo ilifanya serikali ya China kuifuatilia sana. Hapo baadaye China iliweka mpango wa kutenga Renminbi zaidi ya Yuan bilioni 56 kwa kuanzisha mradi wa kudhibiti upepo mkubwa kwa kutumia miaka 10 kuanzia mwaka 2001 katika sehemu ya kaskazini ya China yenye eneo la kilomita za mraba laki 4, zikiwemo mikoa ya Mongolia ya ndani na Hebei.
Mji wa Zhangjiakou iliyoko sehemu ya kaskazini magharibi ya Beijing, ni sehemu iliyotiliwa mkazo katika mradi wa kudhibiti upepo mkubwa. Sehemu ya kaskazini, hususan sehemu ya miji ya Beijing na Tianjing iliathiriwa vibaya na mavumbi yaliyotoka jangwa la Maousu na jangwa la Kubuqi yenye eneo la kilomita za mraba elfu 80 kwa kupitia mji wa Zhangjiakou.
Baada ya ujenzi wa miaka 3, maeneo yenye miti au majani ya sehemu ya Zhangjiakou yamepanuka kwa udhahiri. Mkurugenzi wa idara ya misitu ya mji huo, Bw. Kang Chengfu alisema,
"Kutokana na matokeo ya ufanisi, hivi sasa maeneo yenye miti na majani yanaongezeka. Katika sehemu za mradi huo, maeneo yenye miti na majani sasa yamefikia zaidi ya 70% kutoka pungufu ya 30% ya hapo awali, hatua ambayo inaimarisha moja kwa moja hifadhi ya ardhi, hususan kuzuia mmomonyoko wa ardhi na ardhi kubadilika kuwa jangwa."
Bw. Kang alisema kuwa mradi wa kudhibiti upepo mkubwa na mavumbi wa sehemu ya Beijing na Tianjing umefanya hewa ya sehemu ya Zhangjiakou kuwa safi kuliko zamani. Katika miaka miwili iliyopita, siku zenye upepo mkubwa mjini Zhangjiakouzimepungua kwa udhahiri, tena upepo uliovuma ulikuwa mdogo ukilinganishwa na ule wa mwaka 2000.
Kiongozi wa idara ya misitu Bw. Wei Diansheng alisema kuwa mradi wa kudhibiti upepo na mavumbi wa sehemu ya Beijing na Tianjing ni mfano mmoja wa kuboresha mazingira ya asili kwa kupanda miti na majani. Alisema kuwa hata katika mwisho wa miaka ya 70 ya karne iliyopita, China ilianzisha harakati ya kupanda miti. Kanda za misitu za mfumo wa miradi ya kuzuia upepo na mavumbi ya sehemu za kaskazini mashariki, kaskazini na kaskazini magharibi za China, zinajulikana zaidi kwa "mradi wa misitu wa Sanbei". Mradi huo wa misitu wenye eneo la kilomita za mraba zaidi ya milioni 4, unaanzia sehemu ya mashariki kwenda sehemu ya magharibi kwa umbali wa zaidi ya kilomita elfu 4 na mia 4. katika eneo la mradi huo kuna karibu majangwa yote yanayojulikana sana hapa nchini. Kwa kuwa eneo hilo ni lenye mvua kidogo, hivyo mavumbi ni rahisi kupeperushwa na upepo. Alipozungumzia ufanisi wa mradi wa misitu, Bw. Wei alisema,
"Baada ya kujenga mradi wa misitu wa Sanbei kwa zaidi ya miakia 20, hivi sasa mazingira ya asili ya baadhi ya sehemu yameboreshwa kwa udhahiri. Kwa mfano, mfumo wa misitu ya mradi wa kuzuia upepo mkubwa umekamilishwa kwenye ardhi tambarare ya Sanjiang, kaskazini mashariki mwa China; sehemu yenye mchanga mwingi ya Kerxin, mashariki ya mkoa wa Mongolia ya ndani imekuwa na miti na majani mengi; sehemu yenye mchanga mwingi ya Mausu, sehemu ya kati ya Mkoa wa Mongolia ya ndani na sehemu ya kaskazini magharibi ya mkoa wa Sanxi imeboreshwa kulinganishwa na zamani ambapo sehemu yenye miti na majani imepanuka kwa hatua kubwa. Baadhi ya sehemu zilizoko kusini mwa mkoa wa Xinjiang hivi sasa zimekuwa na maji na miti.
Habari zinasema kuwa mradi wa hifadhi ya mazingira ya asili kwa kupanda miti unaojengwa nchini ni pamoja na mfumo wa misitu kwenye shemu inayopita mto wa Changjiang, kupanda miti kwenye ardhi iliyoendelezwa kuwa mashamba na udhibiti wa jangwa. Baada ya ujenzi wa miradi hiyo kuanzishwa, hivi sasa Chinba imekuwa nchi ya kwanza kwa wingi wa misitu iliyopandwa na binadamu. Kutokana na takwimu, katika miaka ya karibuni, ongezeko la misitu iliyopandwa na binadamu linaongezeka kwa zaidi ya hekta milioni 6 na laki 6 kwa mwaka, hali ambayo eneo la misitu iliyopandwa na binadamu katika miaka 50 iliyopita lilikuwa hekta milioni 44 tu.
Mji wa Ningguo, mkoani Anhui, sehemu ya mashariki ya China ni sehemu inayoongoza katika harakati ya kupanda misitu. Sehemu hiyo ambayo iko katika sehemu ya chini ya mto wa Changjiang, imepata mafanikio makubwa katika harakati ya kupanda misitu. Naibu meya wa mji huo Bw. Yu Honghan alisema,
"Baada ya kujitahidi kwa miaka 6 au 7 hivi, ongezeko la misigu la mji wa Ningguo limefikia 4%, hivi sasa zaidi ya 70% ya ardhi ya mji huo imekuwa na miti na majani".
Habari zinasema kuwa maendeleo ya misitu ya mji wa Ningguo yanaleta ufanisi kwa hifadhi ya rasilimali ya maji na ardhi ya mji huo, vilevile umechangia uboreshaji wa mazingira ya asili na ubora wa maji wa miji ya jirani zake ikiwemo Hangzhou na Shanghai. Katika siku za baadaye, China itajitahidi kupanda miti katika miji mikubwa na sehemu ya vijijini. Habari zinasema kuwa katika shughuli za kupanda misitu, China imekuwa na ushirikiano na jumuia ya kimatiafa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-05-25
|