Kwa nini ugonjwa wa UKIMWI unatisha sana?
Ugonjwa huu unatisha sana kutokana na sababu nyingi mbalimbali, baadhi yake zikiwa ni hizo tatu zifuatazo:
1. Unafyeka watu kama Majani:
Mpaka sasa takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba katika kila watu 100 wanaopata ugonjwa huu 60%-70% huwa ni wale wenye UKIMWI Baridi, 23-26% huwa ni wale wenye UKIMWI Vuguvugu; 2%-15% huwa ni wale wenye UKIMWI Moto; na katika kipindi cha miaka miwili hadi mitano hao wenye UKIMWI Moto watakuwa wamekwisha kufa.
2. Hautibiki:
Mpaka sasa wataalam hawajafaulu kugundua dawa za kuchanja ama njia nyingine za kuzindika watu ili wasiugue UKIMWI.
3. Hauna Kinga:
Ijapokuwa ugonjwa umelipuka katika miaka ya hivi karibuni tu lakini tayari umeshaenea sehemu nyingi sana duniani. Kutokana na kuambukizana, takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya watu wenye UKIMWI imekuwa ikiongezeka mara mbili kila baada ya miezi sita hadi mwaka mmoja.
4. Unaambukiza:
Ijapokuwa wataalam katika sehemu nyingi duniani wanaendelea kujitahidi sana kutafuta dawa za kuponyesha UKIMWI, lakini mpaka sasa hayajapatikana mafanikio yenye matumaini makubwa.
5. Ni ugonjwa wa maisha:
UKIMWI haimaliziki mwilini. Ukishaambukizwa utabaki nayo mpaka ufe. Viini (virus) vya ugonjwa huu vikishaingia mwilini mwako vitaendelea kubana humo na kuzaana humo katika maisha yako yote; na kwa vile mpaka sasa haijagunduliwa dawa ya kuweza kuviua basi ni dhahiri kwamba ukiambukizwa ugonjwa huu utakuwa ni mtu mwenye wasiwasi maisha yako yote kwani japo UKIMWI yako iwe ni ya baridi hujui ni lini itaweza kubadilika na kuwa ya vuguvugu au ya moto.
Isitoshe licha ya kuwa ni ugonjwa wa maisha, kama wewe ni msichana, ugonjwa huu utaweza kuendelea kuonekana kwa baadhi ya watoto wako kwa miaka mingi baada ya wewe mwenyewe kutoweka.
Mtu mwenye UKIMWI (AIDS) anaambukizaje wengine?
Kila kimtokacho mtu mwenye UKIMWI (iwe UKIMWI Moto au Vuguvugu, au Baridi) ndicho kinachoeneza ugonjwa kwa wengine. Baadhi ya vitu hivyo vinavyotoka na ambavyo imethibitika kwamba mna viini vya UKIMWI ndani yake ni:
Maji ya kiume ya uzazi; damu; mate; maziwa; machozi; na utoko.
Njia yoyote inayoruhusu ama kuwezesha vitu hivi vinavyomtoka mtu mwenye UKIMWI vipenye na kumwingia mtu mwingine tunaweza kuviita ni daraja la kuvusha ama kueneza ugonjwa huu.
Kwa hiyo mtu mwenye UKIMWI ataweza kuambukiza wengine ugonjwa wake kwa njia zifuatazo:
(a) Kama atajuana kimwili na watu wengine.
(b) Kama atajitolea kutoa damu yake kuwasaidia wengine wenye kuhitaji damu.
(c) Kama atajitolea kutoa maji yake ya kiume ya uzazi yahifadhiwe kwa madhumuni ya kuwasaidia kina mama wanaohitaji kupata watoto kwa njia hiyo.
(d) Kama vyombo vitakavyotumika kumhudumia (anapodungwa sindano; au anapochanjwa; au anapotahiriwa; au anapotoga masikio; au anaposhonwa na kufungwa vijeraha n.k.) vitatumika pia kuwahudumia watu wengine kabla ya kusafishwa na kuchemshwa sawa sawa inavyopasa.
(e) Kama atakubali kubeba mimba na kuzaa watoto.
Kuna njia nyingine ambazo zinamwezesha mtu kuambukiza wengine ugonjwa wake, lakini kwa kuwa uambukizaji kwa njia hizo ni wa nadra hatutazitaja hapa. Baadhi ya njia hizo chache nyingine zitatajwa katika majibu mbalimbali yatakayotolewa kwa maswali yanayofuata.
Idhaa ya Kiswahili 2004-05-26
|