Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-05-27 21:44:09    
Maisha ya Wakazi wa Guangzhou

cri

    Mji wa Guangzhou ulioko kusini mwa China ni mji mzuri wa kuishi. Ukienda mjini Guangzhou utakuta vyakula vitamu vya aina nyingi, mikahawa ya chai na baa ziko nyingi. Wakazi wazee na wa makamo wa Guangzhou wanaishi maisha ya raha, na vijana wa mji huo pia wanafurahia maisha ya utajiri baada ya kazi.

 

   Kunywa chai katika mikahawa ya chai ni desturi ya wakazi wa Guangzhou. Asubuhi na mapema kila siku, watu wengi wakiamka tu huenda katika mikahawa ya chai iliyoenea mjini kote. Kikombe kimoja cha chai, aina mbili au tatu za viburudisho ndicho kifungua kinywa cha watu wengi. Hasa kwa wazee waliostaafu huwaalika marafiki wengine kwenda pamoja katika mikahawa ya chai, huwa wanakunywa chai huku wakizungumzia mambo mbalimbali.

 

    Bibi Tan Aizhen ni mfanyakazi mstaafu wa mji wa Guangzhou, yeye anapenda kwenda katika mkahawa wa chai ulioko katika mtaa wa Donghu wenye mandhari nzuri.

    "Nikiwa na wakati huenda kwenye mkahawa huo wa chai pamoja na marafiki zangu, hapo kuna aina nyingi za viburudisho, lakini nia yetu hasa ya kuja hapo siyo kula chakula tu, bali ni kujiburudisha na hali nzuri katika mkahawa huo. Tukikusanyika hapo huwa tunabadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa,kimaisha,kiuchumi na kadhalika."

    Bibi Tan aliona kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, mabadiliko mengi yametokea katika mkahawa huo,zamani hali ya kimazingira ya mkahawa huo haikuwa maridadi kama ilivyo sasa, na pia hakukuwa na aina nyingi za viburudisho kama ilivyo sasa. Sasa mkahawa huo wa chai umepambwa vizuri, na chakula chenyewe pia kimekuwa kizuri zaidi na zaidi.

    Wakazi wa mji wa Guangzhou wanaweza kunywa chai kila wakati, asubuhi na mapema, mchana na usiku. Hivyo wakati wowote, unaweza kuwakuta watu wanaokunywa chai katika mikahawa mbalimbali ya chai. Licha ya wazee, pia vijana wanapenda kwenda katika mikahawa ya chai baada ya kazi, kwao mikahawa ya chai ni kama ukumbi wa upashanaji habari, wanaweza kuongea kuhusu habari yoyote kama vile habari za michezo, hali ya kazi zao na kadhalika. Zaidi ya hayo, wafanyabiashara wameifanya mikahawa ya chai kama mahali pa kufanya mazungumzo ya kibiashara. Bwana Li Gan ana kampuni ya kibinafsi, akizungumzia ubora wa kunywa chai alisema :

    "Sasa mikahawa ya Chai ya Guangzhou ni kama sehemu yetu ya habari. Kuishi mjini Guangzhou, kama hujui kunywa chai, utakosa nafasi nyingi za kibiashara."

    Hivyo, kunywa chai kuna maana nyingi kwa wakazi wa Guangzhou, si kama tu kula chakula, bali pia ni nafasi nzuri ya kuwasiliana na kubadilishana mawazo.

    Mikahawa ya chai pia imeonesha vizuri hali ya maisha ya wakazi wa Guangzhou. Wakazi wa Guangzhou wengi wanapenda kukusanyika pamoja kwa watu wa familia , ifikapo mwishoni mwa wiki, wazee kwa watoto, wanaume kwa wanawake kutoka familia mbalimbali wanamiminikia katika mikahawa mbalimbali ya chai, baadhi yao wakichelewa huwa wanakosa nafasi ya kukaa kutokana na kuwepo kwa wat uwengi.

    Wakazi wa Guangzhou licha ya kupenda kunywa chai, pia wanapenda kunywa mchuzi. Nyumbani au katika mikahawa, watu hufikiria zaidi mchuzi kuliko vitoweo. Hivyo ustadi wa kupika mchuzi umekuwa kipimo cha kuonyesha hali ya upikaji chakula kwa akina mama. Bibi Huang Xiaokuan ni mwalimu wa shule ya sekondari, licha ya kazi yake ya mafundisho, anapenda sana kupika mchuzi.

   

 "Sisi wakazi wa Guangzhou tunatilia maanani sana kunywa mchuzi, na tunapika mchuzi tofauti katika majira tofauti. Kwa mfano, wakati wa majira ya mchipuko, tunapika mchuzi unaosaidia kujenga nguvu na kuondoa unyevu mwilini ; katika majira ya joto, tunapika mchuzi wa kuondoa joto mwilini; katika Majira ya baridi, hali ya hewa ya Guangzhou ni nzuri, huwa tunapika mchuzi za kujenga afya."

   Licha ya chakula, wakazi wa Guangzhou pia wanatilia maanani sana kujenga afya, wanapenda kufanya mazoezi na kucheza michezo ya aina mbalimbali baada ya kazi, kama vile kupanda mlima na kucheza mpira. Bwana Zhuyi anafanya kazi katika shirika la habari, alipozungumzia maisha yake baada ya kazi alisema:

    "Baada ya kazi, mimi napenda kucheza mpira wa tenisi. Kila wiki lazima nicheze mpira kwa mara moja au mbili pamoja na marafiki zangu. Baada ya mchezo huwa tunakula chakula pamoja na kupiga soga ili kupashana habari kuhusu michezo ya duniani na kadhalika."

    Hali ya hewa ya Guangzhou ni joto kiasi tena ni yenye unyevunyevu, hivyo maua yanaweza kuchanuka kwa mwaka mzima, Guangzhou ni mji maarufu wa maua nchini China. Maisha ya kila siku ya wakazi wa Guangzhou hayawezi kuendelea bila ya maua. Mabibi wanaponunua mboga sokoni hawawezi kusahau kununua kifurushi cha maua yanayopendeza. Zaidi ya hayo, wakazi wa Guangzhou hupenda kupanda maua kwenye vyombo vya aina mbalimbali katika roshani, na kupamba sebule na vyumba vya kulala kwa maua mabichi au maua makavu. Kila mwaka, mji wa Guangzhou unafanya tamasha kubwa la maua wakati wa kusherehekea sikukuu ya jadi ya mwaka mpya, ambayo inawavuta wakazi wenyeji ,wageni kutoka nchini na nchi za n'gambo walio wengi sana kutembelea na kununua maua yanayopendeza sana.

    Matumizi ya kiasi kikubwa ya maua ya wakazi wa Guangzhou yamestawisha soko la maua mjini Guangzhou, katika vitongoji vya Guangzhou yako mashamba kadhaa makubwa ya kuotesha na kupanda maua. Katika kijiji cha Fangchun kilichoko kusini magharibi ya mji wa Guangzhou, Bibi Chen Lan ameshapanda maua kwa miaka 6. Alisema kuwa, japokuwa maua yanaleta uzuri kwa watu wengine, lakini kupanda maua ni kazi ya kutoa jasho sana, hata kuotesha kwa mbegu za aina mpya ya maua huwa kunahitaji majaribio ya mara nyingi, kuvumilia kushindwa mara kwa mara. Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa ya kuchapa kazi, amefaulu kuotesha aina kadhaa ya maua yanayokaribishwa sana na wateja, na mapato ya shamba lake yameongezeka mwaka hadi mwaka. Anaongeza kuwa, jambo linalomfurahisha zaidi ni kazi yake ambayo inaweza kuboresha maisha ya wakazi wa Guangzhou.

Idhaa ya Kiswahili 2004-05-27