Mradi wa ushirikiano wa kinga na tiba ya ukimwi kati ya China na Marekani umeanzishwa rasmi mkoani Henan, kaskazini mashariki ya China. Mradi huo utagharimu yuani milioni 15 kwa mkoa wa Henan katika miaka mitano ijayo ili kuusaidia mkoa huo kufanya utafiti, upimaji, uchunguzi na uingiliaji kati kwa ugonjwa wa ukimwi na kuwaandaa watu wenye ujuzi wa kinga na tiba ya ukimwi.
Mradi huo unagharimiwa na serikali ya Marekani, na kituo cha udhibiti wa magonjwa cha Marekani kinashughulikia utekelezaji wa mradio huo. Idara husika ya Marekani imeeleza kuwa, ushirikiano kati ya serikali kuu na serikali ya mkoa wa China na serikali ya Marekani katika utekelezaji wa mradi huo umeonesha kuwa China imeahidi kithabiti kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa ukimwi.
Habari zinasema kuwa, mradi huo utaweka mkazo katika kuimarisha kazi ya kuwaandaa watu wenye ujuzi wa upimaji na matibabu ya ugonjwa wa ukimwi mkoani Henan, kuongeza kiwango cha upimaji wa ukimwi, na kutoa misaada kwa familia zilizoathiriwa na ugonjwa wa ukimwi.
2004-05-29
|