Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-11 21:44:54    
Ngome za Kuishi za kabila la Watibet

cri

    Nyanda za Juu za Qinghai-Tibet nchini China zinajulikama kama ni paa la dunia. Kutokana na jiografia isiyo ya kawaida, watu wa huko wa kabila la Watibet wanaishi katika nyumba za ngome.

    Makazi ya Watibet yana historia ndefu sana, magofu yaliyobaki yana kumbukumbu kuaanzia Enzi ya Mawe yaani miaka elfu 4 iliyopita. Kwa sababu ya kuwa Watibet wanakaa huku na huko katika eneo kubwa, makazi yao pia yanatofautiana kutokana na sura tofauti ya nchi. Kusini mwa Tibet kwenye mabonde wanaishi katika ngome, kaskazini mwa Tibet wanaishi katika mahema na katika sehemu zilizopitiwa na mto Yaluzangbu na sehemu za misitu wanaishi katika nyumba za mbao. Lakini kati ya makazi hayo, yasiyo ya kawaida na ya kuvutia zaidi ni ngome zao.

    Nyumba za ngome ni za mraba, sehemu ya chini ni pana na juu nyembamba, na paa ni la bapa. Hata hivyo nyumba hizo zinatofautiana kutokana na sehemu tofauti zilipo. Mjini, nyumba za ngome huwa za fahari, na vyumba ndani ya ngome vinapangwa kwa busara. Nje ya mji, nyumba za ngome hujengwa milimani mahali penye mwanga wa jua bila upepo mkubwa. Nyumba hizo hujengwa kwa mawe na mbao, kwa nje ukuta hujengwa kwa mawe tupu na ukuta ni mnene hata kufikia mita moja, ukutani kuna madirisha madogo na machache. Kwa hiyo nyumba kama hizo zinaonekana madhubuti sana. Nyumba za ngome zina aina tatu, yaani ngome za ghorofa, ngome za mnara na ngome pekee bila ua.

    Ngome za ghorofa huwa na ghorofa moja au mbili, zenye ghorofa tatu ni chache, ua wake huzungukwa kwa ukuta mrefu.

    Ngome za mnara huwa na paa la msonge ambapo ndani ya msonge huwa na vyumba viwili au vitatu kwa ajili ya kusali. Ngome kama hizo zinajitokeza sana kwa sababu ya msonge katika sehemu ya makazi.

    Ngome pekee, maana yake haina ua, ngome kama hizo hujengwa hapa na pale milimani na vijijini pia. Ndani ya kijiji ngome hizi hujengwa huria na zinatofautiana kwa urefu, njia finyu za kokoto zinaunganisha kati ya ngome. Hii ni mandhari nyingine pekee katika Tibet.

    Katika sehemu za kilimo na ufugaji, nyumba za ngome hutumika kufungia mifugo katika ghorofa ya chini, chumba cha kulala, jiko na ghala hupangwa katika ghorofa ya kwanza, na chumba cha kusali huwa katika ghorofa ya pili. Paa la ngome hutumika kwa kuanika nafaka. Watibet hawatumii kitanda wala meza, bali wanakaa na kulala sakafuni juu ya godoro

    Watibet wote ni waumini wa dini ya Buddha, alama za dini yao zaonekana wazi kila mahali. Nje ya nyumba zao hutundika vitambaa vya rangi nyekundu, buluu na nyeupe, na pembezoni mwa madirisha hutundikwa tepe za rangi nyekundu, nyeupe, buluu, njano na ya kijani. Rangi hizo tano zinamaanisha moto, mawingu, mbingu, ardhi na maji, na zinaonyesha matumaini yao mema.

Idhaa ya Kiswahili 2004-06-11