Sehemu ya magharibi ya China ni sehemu yenye mazingira magumu, wakazi wa sehemu hiyo wanaishi maisha ya umaskini, watoto wao wanasoma katika shule zenye hali duni sana. Lakini katika miaka ya hivi karibuni tangu serikali ya China kutilia maanani kuendeleza sehemu ya magharibi, na kupeleka vijana wanaojitolea kufanya kazi huko kama walimu, sehemu hizo zimeongezwa nguvu na uhai. Wakati huo huo, vijana hao pia wamebadilisha fikra zao wanaposhiriki katika mchakato wa China wa kubadilisha maisha ya watu wa sehemu za maghairbi nchini China.
Msichana Feng Ai mwenye umri wa miaka zaidi ya 20 mwaka huu ni mwanafunzi wa chuo kikuu maarufu cha Fudan cha Shanghai, anasoma shahada ya pili, lakini amekwenda kwa hiari mara mbili katika sehemu maskini za magharibi kama mwalimu .
Mwezi Agosti mwaka 2000, msichana Feng Ai alihitimu chuo kikuu, kutokana na sifa yake ya kimasomo na kimaadili, alipewa kibali cha kusomea shahada ya pili bila mtihani, lakini aliamua kusimamisha masomo kwa mwaka mmoja na kuomba kufanya kazi katika sehemu ya magharibi.
Mara ya kwanza, msichana Feng Ai alitumwa kufanya kazi kama mwalimu katika wilaya ya Xijie ya mkoa ujiendeshao wa Ningxia, kaskazini magharibi ya China. Wilaya ya Xijie iko katika milima mirefu, ni wilaya maskini ya kitaifa, na iliwahi kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa kuwa mahali pasipofaa kuishi kwa binadamu, mapato ya wastani ya mwaka ya wanavijiji wa sehemu hiyo ni chini ya yuan za renminbi 300, ni kama dola za kimarekani 35 hivi. Watoto wengi wa sehemu hiyo hawajawahi kuondoka milimani.
Kazi ya msichana Feng Ai ni kufundisha masomo ya Kichina, Kiingereza na Jiografia katika shule ya sekondari ya Baiya. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwa mwalimu. Mwanzoni hakujua namna ya kukabiliana na wanafunzi, lakini alijaribu kuzoea kazi hiyo kwa haraka na kuwafundisha kwa njia zake mwenyewe. Kwa mfano, licha ya vitabu vya kiada, wanafunzi wa sehemu hiyo hawana vitabu vingine vyo vyote, Feng Ai aliwasimulia mambo ya nje kutokana na maarifa yake mwenyewe. Wanafunzi wengi hawajawahi kuona garimoshi, aliwachorea picha za garimoshi na kituo cha garimoshi. Katika darasa la jiografia, yeye ni kama mwongoza watalii, alijaribu kuwawezeksha wanafunzi wakumbuke kwa urahisi majina ya milima na miji maarufu duniani. Watoto walivutiwa sana na ufundishaji wake.
Ili kuboresha hali duni ya ufundishaji shuleni, na kuwatafutia wanafunzi maskini vifaa vya kujifunza na nguo za siku za baridi, alitumia mbinu mbalimbali kuomba msaada kutoka kwa jamii. Kutokana na juhudi zake, wanafunzi na walimu wa chuo kikuu alichojifunza na watu wa fani mbalimbali walimchangia vifaa vya kufundisha na nguo za siku za baridi. Kampuni moja ilitoa kompyuta 17 kwa shule hiyo, jambo hilo limeboresha kwa kiasi kikubwa hali ya ufundishaji wa shule hiyo.
Msichana Feng Ai si kama tu ametafuta msaada kwa shule hiyo, bali pia ameingiza fikra za kisasa za kuwaelimisha watoto milimani, kama vile kufanya mkutano wa wazazi wa wanafunzi kila baada ya muda fulani. Msichana Feng anasema:
" Shule nyingi vijijini katika sehemu hiyo hazina utaratibu wa kufanya mkutano wa wazazi. Kutokana na pendekezo langu, mkutano wa kwanza wa wazazi wa wanafunzi ulifanyika katika shule ya sekondari ya Baiya, na umewekwa utaratibu kadhaa, kama vile kumchagua mjumbe mmoja kutoka kila kijiji, mjumbe huyo kila baada ya muda fulani anakuja shuleni kufahamishwa hali ya masomo ya wanafunzi kutoka kijiji chake, halafu anarudi kijijini kuwaambia wazazi wa wanafunzi hali ya watoto wao ."
Msichana Feng Ai pia alijaribu kujua hali ya wanafunzi wake kwa njia ya kutembelea nyumbani kwao ili kuwafundisha kutokana na hali halisi ya wanafunzi wake. Aliwaambia wazazi wa wanafunzi umuhimu wa elimu kwa maisha ya usoni ya watoto wao, kwa familia na kwa jamii, na kuzitaka familia maskini kushikilia kuwapeleka watoto wao shuleni.
Vitendo hivyo vya Feng Ai vimeleta athari nzuri kwa walimu wengine wa shule yake, mwalimu Ma Yinghu alisema:
" Kuhamasishwa na kitendo cha Feng Ai, walimu wengine wa shule pia wanaanza kuwatembelea wazazi wa wanafunzi, ili kufahamu hali yao ya nyumbani, na kuweka msingi mzuri wa ufundishaji unaofaa. Msichana Feng Ai kweli ameleta nguvu ya uhai kwa shule."
Katika mwaka huo mmoja, msichana Feng Ai alikonda sana, na kutiwa rangi ya jua mwilini, lakini wakati huo huo amepata mavuno makubwa, wanafunzi 8 wa darasa alilofundisha walifaulu mtihani wa kwenda chuo kikuu, kiasi hicho kimezidi awamu yoyote iliyopita. Na kiasi cha wanafunzi walioacha masomo pia kilipungua. Japokuwa maisha yake ya milimani yalikosa burudani za mjini, lakini alikuwa na furaha tele moyoni.
" katika sehemu ya magharibi, nilihisi kuheshimiwa na kuhitajiwa sana. Nimeona thamani yangu. Wanafunzi wananichukulia kuwa mwalimu wao, rafiki yao na dada yao mkubwa. Nimejenga uhusiano mzuri sana na wanafunzi na wakazi wenyeji. Naona maisha yangu ya mwaka huo katika sehemu ya magharibi yamenipa vitu vingi sana, hiyo ndiyo sababu iliyonifanya niamue kurudi tena sehemu ya magharibi."
Baada ya kumaliza maisha yake ya mwaka mmoja ya ualimu katika wilaya ya Xijie, msichana Feng Ai alirudi Shanghai kuendelea na masomo yake ya shahada ya pili. Mwezi Juni mwaka jana, alipopata habari kuwa, idara husika zilikuwa zinawaandikisha wanafunzi wa vyuo vikuu kuhudumia sehemu ya magharibi, aliamua bila kuchelewa kujiandikisha kwa mara nyingine tena.
Hivyo katika siku za joto mwaka jana, msichana Feng Ai alifunga safari tena kuelekea kwenye milima ya sehemu ya magharibi. Alitumwa kuwa mwalimu katika shule ya sekondari ya wilaya ya Noingliang ya mkoani Yuannan, kusini magharibi mwa China. Kutokana na maarifa yake ya kuwa mwanafunzi aliyejitolea, pamoja na uwezo wake mkubwa, mara hiyo aliteuliwa kuwa kiongozi wa kikundi cha wanafunzi wajitoleao wa sehemu aliyokuweko na naibu mkuu wa shule yake. Muda si mrefu uliopita, yeye pia alichaguliwa kufanya kazi katika idara ya elimu ya wilaya ya Ningliang. Msichana Feng Ai alisema kuwa, atatumia vizuri fursa hiyo kutoa mchango wake kwa elimu ya sehemu za magharibi nchini China.
Idhaa ya Kiswahili 2004-06-17
|