Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-06-21 19:11:07    
Roboti ya kwanza ya China inayofanana na mchezaji wa soka yatengenezwa katika chuo kikuu cha mambo ya viwanda cha Harbin

cri

    Roboti ya "Mchezaji nyota wa soka" inayojulikana kwa jina la "HIT" itavutia macho ya watazamaji katika uwanja wa michezo ya soka. Hii ni roboti ya kwanza ya China inayopiga mpira kwa miguu miwili, ambayo ilioneshwa tarehe 18 mwezi Juni katika mashindano ya kombe la dunia ya kuchagua maroboti ya soka ijulikanayo kwa FIRA mwaka 2004, ambayo pia ni mashindano ya tano ya ubingwa wa maroboti ya soka yaliyofanyika tarehe 18 mjini Wuhan.

    Roboti ya "HIT" ambayo ina kimo cha nusu mita na yenye viungo 17, ilitengenezwa kwa aluminium ngumu. HIT inafanana na binadamu, kwa kuwa ina kichwa, mwili na miguu, lakini inatofautiana na binadamu kwamba kiuno, kinyonga, magoti na miguu yake vinaunganishwa na bolti zaidi ya mia moja.

    Mwilini mwa HIT, kuna zana mbili zinazopokea mawimbi ya tarakimu ambazo zinaongoza vitendo na viungo vyake, HIT inaweza kutembea vizuri kwenye njia yenye mwinuko na mashimo, vilevile inaweza kunyanyua mguu wake kupiga mpira. Kupitia kamera ya video, HIT inaweza kutambua mpira, wachezaji na vikwazo, hivyo inaweza kuvikwepa na kupiga mpira kwa usahihi mbele ya mlango wa goli.

    Profesa wa chuo kikuu cha mambo ya viwanda cha Harbin Bw. Hong Bingrong alisema kuwa wataalamu na wahandisi wa China walitumia muda wa zaidi ya miaka kumi, lakini hawakufanikiwa kutengeneza roboti lenye miguu miwili, hivyo maroboti ya China yaliyoshiriki kwenye mashindano ya soka, mengi yalikuwa magari yenye magurudumu mamwili, na chombo cha kuchezea watoto kilichotengenezwa na kampuni ya SONY, Japani ni mbwa mwenye miguu minne.

    Bw. Hong Bingrong alisema kuwa kwanza, roboti yenye miguu miwli, ina viungo vingi, ikitaka kutembea, sharti viungo vyake vyote vishirikiane, hivyo ni kazi yenye nguvu; Pili, roboti kutembea kwa miguu miwili inahitaji zana za kiwango cha juu cha udhibiti wa kompyuta; Tatu, roboti la soka lina mfumo wa ufahamu wa kiwango cha juu kwa mazingira. Hivyo, roboti yenye miguu miwli ilikuwa kikwazo kwa utafiti wa roboti wa China.

    "Lengo letu ni kufanikiwa kutengeneza timu ya maroboti ya soka inayoweza kuishinda timu ya wachezaji binadamu ifikapo katikati ya karne ya 21." Bw. Hong aliongeza kusema, "Watu wengi wanadhani kwamba mashindano ya soka ya maroboti ni mchezo tu unaoburudisha binadamu, lakini hali halisi ni kwamba hatua hiyo ni mafanikio mapya kabisa ya utafiti na teknolojia ya binadamu inayoungana na uzoefu, inaonesha kiwango cha utafiti wa mitambo inayojiendesha na yenye akili ya binadamu, hivyo mashindano ya soka ya maroboti ni ushindani mojawapo mkali.

2004-06-21