Hivi karibuni "Sheria Kuhusu Hakimiliki ya Jamhuri ya Watu wa China" imeanza kutekelezwa. Sheria hii ni nyongeza na ukamilifu wa sheria mpya ya hakimiliki iliyoanza kutumika mwaka jana. Katika muda wa miaka zaidi ya kumi iliyopita China ilikuwa imejitahidi sana katika hifadhi ya haki ya kunakili na imepata mafanikio makubwa.
Siku chache zilizopita mchezo wa televisheni "Miaka Yenye Hamasa Kubwa" ulioonyeshwa kote nchini China ulitumia wimbo wa zamani uitwao "Anga katika Sehemu Zilizokombolewa" bila ridhaa ya mtunzi ambapo kesi ya kukiuka haki ya kunakili ikafunguliwa mahakamani. Kushitakiwa kwa sababu tu ya kutumia wimbo wa zamani, ni jambo lisingetokea katika miaka zaidi ya kumi iliyopita. Wakati huo nchini China watu hawakuwa na mawazo yoyote kuhusu "hakimiliki". Lakini siku hizi mashitaka ya kukiuka haki ya kunakili yamekuwa mambo muhimu katika magazeti. Kuhusu hali ya hifadhi ya haki ya kunakili ilivyobadilika, naibu mkurugenzi wa Ofisi ya usimamizi wa hakimiliki katika Idara Kuu ya Hakimiliki Bw. Xu Chaosxian alisema,
"Mabadiliko makubwa yametokea katika muda wa miaka 10 iliyopita. Hifadhi ya hakimiliki kila baada ya miaka kadhaa hubadilika mara moja. Kuanzia mwaka 1979 suala la hifadhi ya hakimiliki ilipoanza kuchunguzwa hadi mwaka mwaka 1990 sheria ya kuhifadhi hakimiliki ilipotungwa, ni kipindi muhimu katika historia, na kuanzia mwaka 1990 sheria ilipotungwa hadi mwaka 2001 sheria hiyo iliporekebishwa ni hatua nyingine kubwa katika maendeleo ya kulinda hakimiliki. Kila hatua inamaanisha kuwa sheria ya hakimiliki ya China inakaribia zaidi sheria ya hakimiliki ya kimataifa, na hatua hizi ni za haraka kufikia kigezo cha kimataifa."
Sheria ya kwanza ya hakimiliki nchini China ilianzia tarehe mosi Juni mwaka 1991, si muda mrefu baadaye, China ilijiunga na mikataba mitatu ya kimataifa ya hakimiliki, hivyo hifadhi ya hakimiliki ya China imefikia ngazi mpya. Lakini jinsi siasa, uchumi na utamaduni yanavyoendelea na jinsi sayansi na teknolojia inavyokuwa juu zaidi, ndivyo hakimiliki inavyokuwa inavyoachwa nyuma. Baada ya kuzingatia kwa miaka mitatu, mwezi Oktoba mwaka 2001 "Marekebisho ya sheria kuhusu hakimiliki" imetangazwa.
Hakimiliki imewaletea watunzi wa maandishi ya fasihi, sanaa na sayansi hifadhi ya sheria. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 43 iliyorekebishwa, vituo vya redio na televisheni havitakuwa na haki ya kutumia nyimbo, muziki, mashairi na riwaya bila kibali cha watunzi.
Tarehe mosi Januari, mwaka 2001 "Sheria ya Hifadhi ya Software ya Kompyuta" ilianza kutekelezwa. Na siku chache zilizopita, Idara Kuu ya Hakimiliki imeanzisha utaratibu wa kusajili utengenezaji wa software kwa hiari katika kila mkoa ili kuwahudumia watunzi. Tarehe 15 Septemba mwaka huu "Kanuni za Utekelezaji" zilizosaidia sheria ya hakimiliki zilitangazwa, ambazo kwa uwazi zaidi zimewekwa kanuni za kuhifadhi hakimiliki na kutoa adhabu kwa nakala haramu.
Ili kuhakikisha haki ya watunzi wa maandishi, serikali inaongeza nguvu zaidi na zaidi katika utekelezaji wa sheria. Mkurugenzi wa usimamizi wa soko la bidhaa za sauti na picha Bw. Tuo Zuhai aliwahi kushiriki mara nyingi kampeni ya kupambana na nakala haramu. Alisema,
"Kutokana na takwimu, mwaka uliopita idara za utamaduni kwa ujumla ziliteka nakala haramu na za magendo milioni 100. Mwezi Agosti mwaka huu, kampeni kama hizo zilifanyika kwa wakati mmoja katika mikoa 31 na miji 100 ambapo ziliteketeza nakala milioni 30 haramu na za magendo.
Mwezi Mei mwaka huu, Shirikisho la Filamu la Marekani liliizawadia Wizara ya Utamaduni ya China hati ya maandishi likishukuru na kupongeza mafanikio ya kampeni dhidi ya nakala haramu. Hivi leo kila raia wa China ametambua juhudi zilizofanywa na serikali kuhusu hifadhi ya hakimiliki. Mtunzi mashuhuri wa maneno ya nyimbo Bw. Liao Yong alisema kwamba serikali imeleta mazingira mazuri kwa watunzi. Alituambia,
"Hivi sasa hatua na sheria nyingi kuhusu hifadhi ya hakimiliki zimeanzishwa na kutekelezwa, sheria na hatua hizo zinawatisha wale watengenezaji wa nakala haramu, na kwetu sisi watunzi ni ulinzi imara, na ulinzi huo unachochea zaidi juhudi zetu za utunzi."
Idhaa ya Kiswahili 2004-06-30
|