Ziwa la Qinghai liko katika sehemu ya kaskazini-mashariki mkoani Qinghai, kilomita 150 mbali na mji mkuu wa mkoa huo Xining. Kutokana na barabara nzuri, ukisafiri kwa gari kutoka mji wa Xining kwa muda wa saa mbili hivi utafika huko baada ya kupita mlima wenye urefu wa mita 3500.
Kuna simulizi miongoni mwa wakazi, ikihadithia kuwa katika Enzi ya Tang, yaani kabla ya miaka 1300 iliyopita, binti mfalme mmoja alipokuwa safarini kwenda Mkoa wa Tibet kuolewa alitupa kioo chake cha kujitizamia na baada ya kioo hicho kuanguka ardhini kikageuka kuwa ziwa. Kwa hiyo mioyoni mwa watu wa kabila la Watibet ziwa hilo ni la mungu, kila baada ya miaka kadhaa nao hufanya tambiko kubwa huko ziwani.
Ukisimama karibu na ziwa hilo na kuangalia kwa mbali, utaona milima yenye majani na theluji, ziwa la maji tulivu kama kioo na vivuli vya milima ya theluji ziwani. Pembeni mwa ziwa, mbuga za malisho zenye majani ni kama zulia, maua yanachanua na kutoa harufu nzuri, na mahema ya wafugaji yanaonekana hapa na pale. Saa za mawio na machweo mandhari ya huko inaonekana kama picha nzuri ya kuchorwa.
"Visiwa vya ndege", hili ni jina lililotolewa kutokana na kuwepo kwa ndege wengi katika visiwa hivyo. Kisiwa kilichopo upande wa magharibi kinaitwa Xihaishan, umbo lake linafanana na nundu ya ngamia, eneo lake ni kiasi kilomita 0.3 za mraba. Kisiwa kilichopo upande wa mashariki kinaitwa Haixipi, eneo lake ni kiasi cha kilomita 4.6 za mraba. Ardhi ya visiwani ni bapa na iliyofunikwa na mimea mingi. Wenyeji walituambia kuwa katika miezi ya Machi na Aprili, ndege hufika na kuweka maskani huko kutoka sehemu ya kusini ya China. Wakati huo shughuli nyingi zinakuwa zimeanza visiwani. Ndege laki kadhaa wanarukaruka na kutuatua toka asubuhi mpaka jioni na wanajaa angani na ardhini, muda mfupi baadaye viota vinajaa visiwani. Tokea hapo hadi mwezi Oktoba visiwani panakuwa ni mahali peponi kwa ndege.
Mwezi Mei tulifika huko visiwani. Wakati huo ndege walioweka maskani huko walikuwa wameanza kuatamia. Kutokana na kuwepo kwa ndege wengi na sehemu ndogo, ndege walisongamana na walikorofishana kwa ajili ya kujipatia nafasi nzuri ya kuatamia, na baadhi wanajikuna kwa starehe.
(itaendelea?)
|