Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-06 09:17:32    
Barua za wasikilizaji 6/7/2004

cri
    Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161, Bariadi, Shinyanga, Tanzania ametuandikia barua akisema Marafiki wapendwa, wahariri na watangazaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, pokeeni salaamu nyingi kutoka Bariadi Tanzania. Anasema ni hivi karibuni tu amerudi kutoka huko Morogoro na Dar es Salaam ambako alikuwa amekwenda kizazi. Lakini anasema mwishoni mwa wiki aliyotuandikia barua atarudi tena huko Morogoro(kati kati ya Tanzania).

    Anatuambia kuwa anapenda kutujulisha kuwa amepokea barua tuliyomuandikia tarehe 26 mwezi Mei, na anashukuru sana kwa kadi nzuri zenye picha za wanyama wa China ambao wako hatarini kutoweka katika uso wa dunia. Anasema yeye ana imani kwamba serikali ya wananchi wa China itazidisha mikakati na mipango ya kuwahifadhi wanyama hao kwa kuwawekea uangalizi maalumu.

    Pia anatuambia akiwa msikilizaji wa kila siku wa matangazo na vipindi vya idhaa ya Kiswahili, alisikia katika taarifa ya habari iliyosomwa tarehe 4 mwezi wa 6 majina ya washindi 10 maalum waliochaguliwa kuitembelea China kwa mwaliko na Radio China Kimataifa. Wasikilizaji hao kutoka mataifa mbalimbali tayari wameishaitembelea Radio China Kimataifa na China kwa ujumla. Anasema anataka kutumia nafasi hii kuwapongeza sana, ingawa miongoni mwao hakuna hata msikilizaji mmoja wa Idhaa ya Kiswahili. Bwana kulwa anasema anajua hata sisi watangazaji na wahariri wa idhaa yetu tulisikitishwa na matokeo hayo.

    Anasema lakini hakuna sababu ya kukata tama, kwani yeye na wasikilizaji wetu wataendelea kusikiliza vipindi na matangazo yetu na kushiriki kwa juhudi kubwa katika mashindano yatakayoandaliwa na Radio China Kimataifa. Anasema penye nia pana njia. Vile vile anapenda kuwapongeza wasikilizaji wote ambao watakuwa wamepata ushindi wa kwanza, wa pili na wa tatu na ambao watakuwa wametiwa moyo kwa ushiriki wao kwa mashindano ya ujuzi kuhusu mikoa ya magharibi mwa China ambayo yalifanyika mwaka jana na matokeo yake kutangazwa mwaka huu.

    Pia anasema kwa mara nyingine tena anatoa pongezi kwa ushirikiano uliopo kati yetu na wasikilizaji wetu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Na ansema ana matumaini kuwa mtaendelea kuwahudumia vyema na pia kuzidisha ushirikiano na mawasiliano bila kusita hata katika mazingira ya namna gani.

    Msikililzaji wetu mwingine Homoud A. Tamim wa sanduku la posta 267 Kigoma, Tanzania ametuletea barua akianza na Salamu kwa watangazaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China. Nasema kwa sasa afya yake ni nzuri baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya figo yaliyomfanya alazwe na kutibiwa. Anasema anashukuru sana kwa kunifahamishwa kuwa barua ya klabu yeo ya Tanganyika tuliipata bila wasiwasi.

    Anasema hata wanachama wote wa Klabu ya Tanganyika wamefurahi sana kupokea barua tulizowatumia. Anasema klabu yao ipo na inaendelea kuisaidia Idhaa ya Kiswahili CRI ipate wasikilizaji wengi zaidi huko Kigoma. Anasema tangu waanze kazi hiyo watu wengi wameanza kusikiliza zaidi matangazo ya idhaa yetu.

    Na sasa hivi wana wanachama wa klabu yao Tanganyika, wana mpango wa kusafiri kwenda vijijini kuisaidia idhaa yetu ipate wasikilizaji wengi zaidi. Kwani anasema wamepeleleza na kugundua kuwa vijijini watu wengi hawasikilizi idhaa hii kwa sababu hawajui mitabendi zetu. Anasema lakini wao tayari wameandaa mitabendi ili kwenda vijijini kuzisambaza na wasikilizaji wa huko waweze kutusikiliza vizuri bila ya matatizo.

    Bwana Tamim pia anashukuru sana kwa kumfahamisha kuwa tarehe 26 Aprili mwaka huu ni siku ya maadhimisho ya miaka 40 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Tanzania. Anasema anashukuru sana kwa kufahamishwa kwani yeye alikuwa hamfahamu, na sasa hii haiwezi kutoka akilini kabisa wala hawezi kuisahau tena. Bwana Tamim anamaliza kwa kuomba tumtumie japo vitambulisho vya uanachama wa Idhaa ya Kiswahili. Anasema kila wanapojarinu kuwahamasisha watu kusikiliza matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa watu kwanza huwauliza Vitambulisho vya Uanachama. Kwa hiyo inawapasa watumie muda mrefu sana kuwaelewesha wasikilizaji.

2004-07-06