Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-12 19:29:29    
Safari katika ziwa la Qinghai 2

cri
    Hii ni sehemu ya pili ya makala "Safari katika ziwa la Qinghai".

    Ukiangalia kutoka mbali utawaona ndege wengi kama waumini wanaokuwa katika hija, wamejaa kote visiwani. Ukiangalia kwa darubini, utaona baadhi yao wakiinua vichwa kuangalia mbinguni, wengine wanainamisha vichwa kama wanasinzia; na wengine wanapiga piga mabawa au kusepetuka sepetuka. Ukiwa visiwani utaona viota vya aina mbalimbali hapa na pale na mayai yametapakaa kila mahali kiasi ambacho hata kuweka miguu ni shida. Watalii ni lazima wawe makini na viota, ama sivyo ndege watawarukia kwa kasi kutoka angani ili kuwahi kulinda watoto wao.

    Mara nyingine ndege wanaruka kwa makundi makubwa wakilia lia angani, milio yao inayofurahisha masikio ni kama sauti kutoka peponi. Mtalii mmoja kutoka Beijing Bi. Cui Qing alituambia kwa msisimko wa furaha, "Kwa kweli mandhari ni nzuri, kundi la ndege lo! Ndege wengi walitotoa mayai, tumepiga picha nyingi. Ziwa hili linanifurahisha kweli."

    Sababu ya kuwepo kwa ndege wengi ni kuwa, huko ni mahali panapofaa kuishi kwa ndege kutokana na jiografia na mazingira bora ya kimaumbile. Visiwani, sehemu ya ardhi ni bapa, hali ya hewa ni vuguvugu, na pande tatu zinazungukwa na maji, majani ni mengi na yanastawi, samaki ni wengi, visiwa hivyo ni visiwa vilivyotulia. Ndege wanaridhika na hali ya visiwa hivyo na kufanya maskani yao.

    Mandhari nzuri tunayoiona inapatikana kwa jasho. Kuanzia miaka ya 60 ya karne iliyopita, hali ya hewa duniani imekuwa ikibadilika na kuwa joto, maji katika ziwa la Qinghai yanapungua kwa sentimita 10 hadi 20 kwa mwaka, hali hiyo ni tishio kubwa kwa ndege wanaoishi katika ziwa hilo. Ili kuhifadhi mazingira ya ziwa hilo vituo kadhaa vya hifadhi ya ziwa la Qinghai vilianzishwa, na muda mfupi baadaye sehemu hiyo imewekwa katika orodha ya sehemu za hifadhi ya kimaumbile. Mkuu mmoja aliyefanya kazi kwa miaka 14 katika kituo kimoja cha hifadhi ya visiwa vya ndege, Bw. Jie Lianming alisema, "Kando ya ziwa tumejenga vituo vinne, karibu kila nusu ya mwezi tunalizunguka mara moja ziwa hili, kazi yetu ni kuchunguza michirizi ya kumimina maji ziwani ili kuhakikisha kina chake."

    Kutokana na juhudi za wafanyakazi hao mazingira bora yamehakikishwa na watalii wanapata burudani la kuona ndege wengi.

    Visiwa vya ndege ni kama bustani ya edeni kwa ndege, na pia ni sehemu yenye mandhari ya ajabu mkoani Tibet. Idadi ya watalii wanaokwenda huko kujionea maisha ya asili ya ndege na kujisikia raha uhusiano mzuri kati ya binadamu na maumbile haijawahi kupungua. Kwenye kisiwa cha upande wa magharibi tuliona ndege wawili walio karibu nasi wakiangalia huku na huko angani, wakati tulipochukua kamera tayari kuwapiga picha, nao walionekana kama wameelewa nia yetu, wakainua vichwa na kupiga piga mabawa wakituacha tuwapige picha kwa maringo. Hali kama hiyo yatosha kuwaondolea watu uchovu wote walioupata katika shughuli za kazi.

Idhaa ya kiswahili 2004-07-12