Msikilizaji wetu Mutanda Ayub wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya hivi karibuni ametuletea barua akiema kuwa, hapo Kenya wao ni wazima, hali ya huko ni shwari na mvua ikinyesha. Anasema anaendelea kufurahia mawasiliano yetu naye mara kwa mara, na anashukuru kwa posta kadi nzuri ambazo tumemtumia. Anasema hayo yote yamemfanya atukumbuke kila siku.
Anasema hajasahau kufungua tovuti ya Radio China kimataifa, na habari anazozikuta zimekuwa kama nyota kwake. Kwa yote anasema hongera kwa CRI. Anasema ana hakika ya kwamba kituo chetu ni kituo pekee, na hadhani kama kuna kituo kingine kinachotilia maanani haswa kuwasiliana na wasikilizaji wake kama ya Radio China kimataifa.
Kwa kinaga ubaga anasema kuwa tangu awasiliane na kuongea nasi kwenye semina pale Kisii hajachoka kueneza ujumbe kwa wenzake kusikiliza matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa, kwani hii yote imekuwa sehemu ya shughuli yangu ya kila siku.
Hapa tunamshukuru sana Bwana Ayubu kwa moyo wake wa kujitolea kuhamasisha watu mbalimbali kusikiliza radio China kimataifa.
Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalita wa Shule ya msingo Kiliwi, Divisheni ya Mwanashimba wa sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, ni matumaini yake kuwa watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa hawajambo na anapenda wapokee salamu zake. Tunashukuru sana kwa salamu hizo. Anasema vilevile anapenda kutujulisha kuwa kalenda, kadi za salamu, barua pamoja na karatasi ya kima ya ukataji wa kisanaa tulivyomtumia amevipokea salama.
Vilevile anashukuru kufahamishwa kuwa katika kalenda ya kichina, kila miaka 12 ni duru moja. Na kila mwaka unawakilishwa na mnyama wa aina moja. Jumla kuna wanyama wa aina 12 ambao ni panya, ng'ombe, chui, sungura, dragoni, nyoka, farasi, mbuzi, kima, kuku, mbwa na nguruwe. Pia tarehe 22 Januari mwaka 2004 ilikuwa siku ya mwaka mpya katika kalenda ya kichina, ambao mwaka huu ulikuwa mwaka wa kima katika kalenda ya kichina. Vilevile anafurahi kufahamu kuwa wachina huona kima ni nyota ya heshima, kima pia huwakilisha watu wenye tabia nzuri ya ushujaa, unyoofu na uthabiti.
Kumbe yeye tayari amejua mengi namna hii kuhusu kalenda na mwaka wa Kichina. Anasema pamoja na hayo anapenda kututumia shairi lake linalosema Mungu ibariki Radio China kimataifa mwaka 2004. Vilevile anaomba tumtumie gazeti la China today, atafurahi sana ikiwa ombi lake hilo litakubaliwa na wale wanaohusika hapo Beijing, China, lifuatalo ndiyo shairi lenyewe liitwalo, Muungu ibariki Radio China kimataifa mwaka 2004.
Bismillahi naanza, arahmani nasema
Mwenyezi mungu muweza, mtukufu wa rehema
Aliyenipa kuwaza, na duwa zangu kusema
Muungu wetu ibariki, Radio China kimataifa
Muunba wetu ibariki, radio hii aghaali
Isikike pande zote duniani, kwa mtambo wa Beijing
Uwajaze mashabiki, wanaotaka habari
Mungu wetu ibariki, Radio China kimataifa
Muungu wetu ijalie, kwa kila hali na mali
Watu wengi wasikie, Radio hii asiki
Kila mtu asifie, CRI ni mali
Muunba wetu ibariki, Radio China kimataifa
Kwa duwa yangu makini, ninakuomba rabani
Uijalie Beijing, na wasemao radioni
Radio na televisheni, uzilinde we maanani
Muungu wetu ibariki, Radio China kimataifa
Kwa wale watangazaji, wasemao mitamboni
Uwajalie kipaji, watagangaze kwa amani
Asiwapo mkosaji, makosa wayabaini
Muungu wetu ibariki, Radio China kimataifa
Mwisho tujalie sote, wanachama na wapenzi
Tusomewe yale yote, tuletayo kila mwezi
Musiliache lolote, ila lile lisofaa
Mwaka elfu mbili na nne, mungu ibariki Beijing
Tunamshukuru sana Stephen Magoye Kumalita kwa shairi lake la kututia moyo.
Msikilizaji wetu Thadeus Otieno Oktlo, wa Security Group S.L.P 18670 Nairobi Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu nying kutoka mjini Nairobi, na kushukuru sana kwa barua tuliyomtumia ambayo aliipata hivi karibuni ingawa alichelewa kidogo kuipata.
Anasema kuwa matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa yamemfurahisha na kuwaridhisha watu. kwani matangazo ambayo tumekuwa tikiyangaza kila jioni hata kusikia majina ya watu aliowatumia salamu yakisomwa, na wale aliowatumia salamu kumwambia kuwa wapmepata salamu zake huwa anafarijika.
Kwa maoni na mapendekezo yake anaomba tuendelee hivyo hivyo kwa matangazo na hata taarifa za habari ambazo huwa mnatangaza kupitia Radio China kimataifa kila jioni na anapenda kuendelea kuwa shabiki wa Radio China kimataifa, ili aendelee kutuma salamu nyingi kabisa. Tena anaomba tumtumie kadi nyingine za salamu ili aendelee kutuma salamu zake.
Basi kuhusu hilo asiwe na wasiwasi. Kama kawaida yetu kila tukiwatumia barua tutaambatanisha na kadi za salamu.
Msikilizaji wetu Nyamonge N Ryoba mmoja wa mashabiki bora kutoka Tanzania, anasema katika barua yake kuwa yeye ni msikilizaji maarufu Redio za kimataifa zinaosikika kwenye masafa mafupi kote ulimwenguni. Kwa hiyo yeye ni msikilizaji wa kila siku wa Redio China kimataifa. Hivyo amekuwa mwanachama hai katika klabu ya kemogemba kwa muda mrefu.
Anasema kwa matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kwa kweli anafurahishwa zaidi na vipindi vyake safi kama vile taarifa ya habari pamoja na kipindi cha salamu zenu. Ila tu anapenda kutuarifu kuwa wanachama wanapenda tujaribu kuwatumia fomu za kujaza, halafu wazitume kwetu kwani hiyo itakuwa nafuu zaidi kwao. Kwa upande wa bahasha ambazo tayari zimelipiwa gharama za stempu, aanasema tumefanya jambo la maana sana na wanashukuru.
Lingine ni kuhusu masuala ya magazeti mazuri ya kusoma na vitabu vya kichina ambavyo vimetafsiriwa kwa kiswahili. Anasema kama kuna uwezekano wa kivituma, angeomba tuvitume kwao iliwaweze kuwaona watangazaji wetu wa vipindi wanavyovisikia. Vilevile anasema kuwa terehe 26/6/04 Tanzania na China zilitimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi yake, akiwa mwanachama anaona fahari kubwa sana kwa jambo hilo kufikia hapo lilipo, na kuuombea uhusiano huo uendelee kudumu zaidi.
Anasema sasa yeye hayo maswala hajui yatafanikiwa wapi kwa hapa Tanzania anaomba tumfahamishe zaidi. Zaidi anaomba kama kuna uwezekano wa kupata fulana za Radio China Kimataifa angeomba atumiwe, kwani hiyo ni moja ya njia za kupata wanachama wengi zaidi. Kwa kweli hapa tunataka yeye atuwie radhi, kwani hivi sasa hatuna fulana kama hizo kwani siku hizi kutokana na kikomo cha matumizi ya radio yetu, hatuwezi kupata fulana hizo kwa ajili ya kuzawadia wasikilizaji wetu. Kama kutakuwa na mabadiliko tutawaarifu.
Vile vile anaomba tumfahamishe Redio ilifunguliwa tarehe ngapi, yeye anaamini kuwa ataendelea kuwa pamoja nasi mpaka hatua ya mwisho. Kwani sasa hivi yeye na familia yake huwa wanajiunga kusikiliza kwa pamoja matangazo ya Radio China kimataifa.Pia anaomba kukukmbusha kuwa tujitahidi tumsomee salamu anazozituma na atajisikia mtu mwenye furaha sana endapo salamu zake zitasomwa.
Radio China kimataifa iliazishwa mwaka 1942, Idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataiafa ilianza kurusha matangazo yake hewani Tarehe mosi Septemba mwaka 1961. Tunamshuku sana Bwana Nyamonge Ryoba na jamaa zake kwa ufuatiliaji wao kwa matangazo yetu. Na kuhusu kusomewa salamu zako hila halina wasiwasi, endeleeni tu kuitegea radio China kimataifa mtasikia salamu zenu zikisomwa.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-13
|