Je, inzi au maji huweza kusaidia kueneza UKIMWI?kwa mfano kutokana na matapishi au kinyesi cha mgonjwa wa UKIMWI?
Kabla uambukizaji kwa njia hizo kuweza kutokea ni lazima kwanza mambo matatu yatimie.
a) Lazima matapishi ahyo au kinyesi hicho kiwe na viini vya UKIMWI.
b) Ni lazima maji hayo au inzi hao wafaulu kubeba viini hivyo vikiwa vingali hai.
c) Ni lazima huyo mwenye kuambukizwa awe na jeraha au mahali palipochubuka mwilini mwake ambapo viini hivyo vya UKIMWI vitaweza kuingilia kutokana na inzi au maji hayo.
Kwa kawaida si rahisi kwa mambo hayo matatu kuweza kutokea kwa ukamilifu kwa wakati mmoja; na kwa hiyo uambukizaji wa UKIMWI kwa njia ya inzi na maji sio jambo la kawaida, bali ni la kinadharia tu.
Kubusu nako je! Hakuwezi kueneza ugonjwa huu?
Hapa kwetu hadi sasa kuna taarifa ya mtu mmoja tu ambaye ameambukizwa UKIMWI kwa njia ya kubusu. Yalelekea kwamba kubusu kusiko kwa kawaida?kwa mfano kubusu kwa nguvu na kwa muda mrefu huku kidomo ikiwa ina vijeraha au imechubuka?inaweza kwa nadra sana kueneza ugonjwa huu.
Je, viini vya UKIMWI huweza kuishi katika njia ya kinyesi? Inakuweje basi tabia ya kukaribiana kwa njia tupu ya nyuma kusababisha kuenea kwa ugonjwa huu?
Kukaribiana kwa njia ya tupu hufuatana na kujeruhi ama kuchubua njia ya kinyesi na kutokwa na damu kidogo, viini vya UKIMWI vilivyomo katika damu inayotoka na katika maji maji ya kiume yanayotoka wakati wa kufanya kitendo kama hicho, hupata mteremko rahisi wa kuingia mwilini. Hii ndiyo sababu inayofanya ugonjwa huu uenee kwa haraka sana kwa watu wenye tabia ya namna hii. Katika nchi za magahribi ambako tabia hii imeota mizizi, ugonjwa wa UKIMWI unajulikana kama ni ugonjwa wa wale wanaume wenye tabia hiyo; na kwa kweli katika nchi hizo asilimia sabini ya wagonjwa wote wa UKIMWI huwa ni wanaume hao.
Kushirikiana taulo, chupi au shuka na mtu mwenye UKIMWI ni hatari?
Huweza kuwa ni hatari iwapo wenye kushirikiana vitu hivyo wana vidonda au majeraha mwilini sehemu zinazohusika?yaani sehemu zile zitaguswa na nguo hizo. Lakini kwa kuwa jambo kama hilo si rahisi kutokea, uambukizaji ugonjwa kwa njia hii sio jambo la kawaida.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-14
|