"Nitakapostaafu nitarudi nyumbani na kuanzisha zahanati moja ya kitibet. Ingawa nyumbani kwetu watu ni maskini, lakini nitawatibu wanavijiji wenzangu bila kujali kama nitaweza kuchuma pesa nyingi au la." Bi. Yinmucao alisema. Hivi karibuni, Bi. Yinmucao, Deqingbaizhen na Mingjicuomu walifanikiwa kupitia maswali ya tasnifu zao za shahada ya pili, na kuwa madaktari wa kwanza wa kike wa kitibet wenye shahada ya pili katika historia ya Tibet.
Walianza masomo yao mwezi Septemba, mwaka 2001 katika chuo cha tiba ya kitibet mkoani Tibet. Kabla ya hapo, Yinmucao na Mingjicuomu walikuwa walimu wa chuo hicho, na Deqingbaizhen alikuwa daktari wa magonjwa ya kuambukiza.
Yinmucao mwenye umri wa miaka 40 anatoka kijiji cha Anguona, tarafa ya Jiamenguan, wilaya ya Xiahe, mkoani Gansu. Yinmucao alipokuwa na watoto wawili alikuwa na hamu kubwa ya kusoma. "wazazi wangu wana umri zaidi ya miaka 70, nilipokuwa nasoma ilikuwa ni lazima pia nitunze wazazi na watoto wangu, wakati mwingine nilikuwa naamka saa kumi alfajiri na kuanza kusoma vitabu huku nikifanya kazi." Yimucao alisema. Mwezi Agosti mwaka 1980, aliingia darasa la tiba ya kitibet katika shule ya afya kusini mwa Gansu. Mwaka 1992, alijiunga na chuo cha tiba ya kitibet kusomea shahada ya kwanza. Mwaka 2001 alijiunga na chuo hicho tena kusomea shahada ya pili.
Mama ya Deqingbaizhen ni mtaalamu wa chuo hicho. Deqingbaizhen alisema kuwa, "Sikutaka kujifunza utibabu kwa sababu niliogopa sana damu nilipokuwa mtoto. Nilijifunza vizuri katika kozi za sayansi, hivyo nilitaka sana kuingia chuo kikuu cha Qinghua. Lakini nilipomuona mgonjwa mmoja aliyekuwa akitokwa na damu kwa wingi kichwani akipata nafuu baada ya kutibiwa na mama yangu katika hospitali ya kitibet, niliona kuwa mama yangu ni hodari sana, hivyo nikachagua kujiunga na kozi ya tiba ya kitibet." Alipojifunza utibabu pia alikuwa na hamu kubwa ya kujifunza kiingereza. Mwezi Januari mwaka huu, alipewa tuzo maalumu ya mafanikio ya utibabu na taasisi ya uchumi na tekenolojia ya mkoa wa Sichuan kwa makala yake ya kiingereza iitwayo "utafiti kuhusu tiba ya kitibet katika kutibu ugonjwa wa maini" iliyotolewa kwenye gazeti moja la tiba la china.
Mingjicuomu mwenye umri wa miaka 33 anatoka wilaya ya Xietongmen, mji wa Rikaze mkoani Tibet. Alipokuwa na umri wa miaka 15 alijua kukariri maandishi ya vitabu vitatu katika vitabu nne vya tiba ya kitibet, yaani "msingi wa utibabu", "nadharia za utibabu" na "mazoezi ya utibabu". Mwaka jana, alitunga vitabu vya "sayansi ya tiba ya kitibet kwa akina mama" vyenye maneno elfu 20.
Tiba na dawa za kitibet zina historia ya zaidi ya miaka elfu 2, lakini kwa mawazo ya jadi wanawake hawaruhusiwi kugusa dawa za kitibet". Naibu mkuu wa chuo cha tiba ya kitibet ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maswali ya tasnifu ya wanawake hao watatu Bw. Nimaciren alisema kuwa, wao watatu wote ni hodari, na wamebadilisha historia ya tiba na dawa za kitibet.
Chuo cha tiba ya kitibet kilianzishwa mwezi Septemba, mwaka 1989 mkoani Tibet. Hivi sasa chuo hicho kina walimu 63, wanafunzi 479 na kituo cha kuandaa wanafunzi wa shahada ya pili wa kozi ya tiba ya kitibet. Na mwaka huu, chuo hicho kitakuwa na kituo cha kuandaa wanafunzi wa shahada ya tatu.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-15
|