Msikilizaji wetu Noel E Mashauri wa S.L.P 42 Kiomboi-Iramba Singida Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, kwanza anapenda kutoa salamu kwa watangazaji na watayarishaji wa vipindi wa Radio China kimataifa. Anasema yeye ni mzima wa afya anaendelea vizuri na shughuli za ujenzi wa taifa bila kusahau kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa. Sisi hapa Radio China hatujambo, na tunashukuru sana kwa salamu zako.
Bwana Noel anasema pia anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Redio China kimataifa kwa yote wanayowafanyia wasikilizaji. Pamoja na juhudi za watangazaji wote kwa umahiri wao mkubwa wa kutangaza. Anasema juhudi hizo ni kubwa na zinahitaji ushirikiano wa dhati ili kuzidumisha, kwa upande wake yuko bega kwa bega na radio yake pendwa, kwa namna moja ama nyingine kudumisha hayo ambayo redio China inayafanya kuleta urafiki, amani na ushirikiano katika sehemu zote duniani.
Anasema kwa kuthibidisha hilo ametuletea shairi la pongezi, shairi hilo linasema hivi:
Redio China hongera, kutangazia dunia
Kwa habari zako bora, wasikilizaji ringia
Na mafunzo yalofaulu, kwetu sisi twasifia
Waitangaza dunia, redio China hongera
Radio China pongezi,kwa huo uwepo wako
Hutakosa njema enzi, kwa wote rafiki zako
Jinsi ulivyo mjenzi, shikana huko na huko
Redio China hongera,waitangaza dunia
Redio China waleta, mshikamano ulo mwema
Waunganisha kupata ,dunia isiyovuma
Kwa vurugu na kufuta, tofauti na lawama
Amani waitafuta, kwa shime isiyokoma
Waitangaza dunia,redio China hongera
Anasema anavyodhani hayo yote yasingefanikiwa kama kusingekuwa na mshikamano mzuri kati ya wafanyakazi wote wa redio China .Utangazaji bora na uhariri makini ndiyo unaofanya mafanikio yaongezeke na kukua siku hadi siku hivyo. Shairi lake linaendelea kusema:
Kwa sasa najibarizi, kwa uzalendo pomoni
Kwa wale wafanyakazi, Han mei mama chen
Fadhili Mpunji kazi, kwao bidii si duni
Na wahariri wajuzi, kwa mpangilio makini
Nawapongeza wote, redio China hongera
Bwana Noel Mashauri anasema, anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa kumtumia bahasha ambazo zimeshalipiwa stempu, hali ambayo inamrahisishia si yeye tu bali na wasikilizaji wenzake wote katika kutuma majibu na taarifa nyingine. Hivyo ni njia ambayo itakuza uhusiano wetu sisi wasikilizaji na redio China na wananchi wake kwa ujumla, na pia hapa chini ni salamu zake:
Wapenzi twajivunia, kwa mapendo madhubuti
Ni bure wahudumu,hata wale mahutihuti
Daraja unganisha, usumbufu hatupati
Wananchi wote Asia, Afrika na Djibuti
Ulaya na amerika, marafiki ni bahati
Asante kwa kurahisisha mawasiliano
Ni redio hiyo hiyo ,imeunga urafiki
Bila kinyongo cha moyo, tena taharuki
Kuonyesha nia inayo, inadumishwa mashabiki
Kwa kukudhi itakayo, klabu za salamu lukuki
Asante kwa kurahisisha mawasiliano
Bwana Mashauri anasema, asingependa kuendelea zaidi ila tudumishe urafiki wetu, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, vile vile kidole kimoja hakivunji chawa
Angependa kukumbusha kuwa wasikilizaji wa Radio China kimataifa wanawapenda sana wafanyakazi wa redio yao wakiwakilishwa na Han mei, mama Chen, Fadhili Mpunji na wengine.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-20
|