Kutokana na sera ya serikali ya China ya kusaidia kilimo, vijiji na wakulima na kuongezeka kwa bei za nafaka, ongezeko halisi la mapato ya wastani kwa wakulima lilikuwa asilimia 10.9 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu. Ongezeko hilo si kama tu lilikuwa asilimia 2.2 zaidi kuliko ongezeko la mapato ya wakazi wa mijini, bali pia lilikuwa kubwa kabisa tokea mwaka 1997.
Tarehe 16 mwezi huu katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya habari ya Baraza la Umma la China, msemaji wa habari wa Idara ya takwimu ya China Bw. Zheng Jingping alisema kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, pato la wastani la mkulima lilifikia yuan 1345, ambalo ni ongezeko la asilimia 16.1 ikilinganishwa na mwaka jana. Mabadiliko ya bei yakizingatiwa, basi ongezeko halisi lilikuwa asilimia 10.9, ambalo ni asilimia 8.4 zaidi kuliko ongozeko la mwaka jana.
Bw. Zheng Jingping alichambua kuwa, kutokana na serikali ya China kuimarisha uungaji mkono kwenye sera za kilimo, vijiji na wakulima, kumewawezesha wakulima kupata faida kubwa. Katika nusu ya kwanza, wastani wa kodi kwa kila mkulima ulipungua kwa yuan 4.3, ambazo ni asilimia 27.2 ikilinganishwa na mwaka jana; na pato la mkulima lililopatikana kwa njia nyingine limefikia yuan 67, ambalo ni ongezeko la asilimia 15.2, zikiwemo posho ya nafaka yuan 8.2 na posho nyingine yuan 4.5.
Mwaka huu ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mageuzi ya kupunguza au kufuta kodi za kilimo. Katika mikoa 8 nchini China, kodi hizo zimepunguzwa au kimsingi kufutwa, na katika mikoa mingine, kodi hizo zimepunguzwa. Katika bajeti ya serikali ya China, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kilimo, vijiji na wakulima zimeongezeka kwa yuan bilioni 30 ikilinganishwa na mwaka jana. Katika mikoa 29, wakulima wanaopanda mazao ya nafaka wanalipwa posho moja kwa moja, na fedha za posho hizo zimefikia yuan bilioni 11.6, ambazo zimewanufaisha wakulima milioni 600. Kutokana na makadirio ya idara husika, sera ya kuwalipa wakulima posho ya nafaka, aina nzuri za mazao na mashine za kilimo, na kupunguza au kufuta kodi za kilimo kumeliwezesha pato la wastani la kila mkulima kuongezeka moja kwa moja kwa yuan 50, yaani asilimia 2.
Bw. Zheng Jingping alisema kuwa, kutokana na kuongezeka kwa bei ya nafaka tangu mwezi Oktoba mwaka jana na kuongezeka kwa mazao ya nafaka mwaka huu, mapato ya wakulima kwa kuuza mazao ya kilimo yameongezeka kwa kiasi kikubwa, pato la wastani la kila mkulima katika nusu ya kwanza lilifikia yuan 589, ambalo ni ongezeko la asilimia 18.9 ikilinganishwa na mwaka jana. Mapato ya wakulima yaliyopatikana kwa kufanya kazi za vibarua nyumbani kwao yameongezeka kwa asilimia 27.5, na yaliyopatikana katika miji mingine yameongezeka kwa asilimia 15.3. Ongezeko halisi la mapato hayo lilikuwa asilimia 7.8.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-20
|