Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-22 17:14:53    
Uganda yaonesha mfano kwa Afrika katika udhibiti wa ukimwi

cri
    Rais Yoweri Museveni wa Uganda hivi karibuni alipotoa hotuba katika mkutano wa kimataifa wa ukimwi uliofanyika huko Bangkok Thailand, alitangaza kwa furaha kuwa Uganda ambayo iliathiriwa vibaya sana na ukimwi, sasa kiasi cha watu walioambukizwa na virusi vya ukimwi nchini humo kimepungua hadi kufikia 6%. Aliwahakikishia wawakilishi waliotoka nchi zaidi ya 160 kuwa ukimwi ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa.

   Hivi sasa, ukimwi bado ni ugonjwa unaotishia vibaya maisha ya binadamu, hususan katika sehemu ya kusini mwa Sahara. Mwaka 2003 zaidi ya watu milioni 3 waliambukizwa virusi vya ukimwi, wakati watu milioni 2.2 walikufa kutokana na ukimwi. Barani Afrika, ambako kuna 10% ya idadi ya watu wote duniani, watu zaidi ya milioni 25 wameambukizwa virusi vya ukimwi, ikiwa ni 70% ya idadi ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi duniani. Katika sehemu hiyo kuna nchi 7 ambazo zaidi ya 17% ya idadi ya watu wake wameambukizwa virusi vya ukimwi, baadhi ya nchi hizo idadi hiyo ni zaidi ya 35%.

   Wakati ukimwi unaendelea kuwaathiri vibaya binadamu, rais Museveni ana imani kubwa kiasi hicho, kutokana na uzoefu iliopata Uganda katika kupambana na Ukimwi kwa miaka zaidi ya kumi iliyopita.

   Kabla ya zaidi ya miaka kumi iliyopita, Uganda ilikuwa kama nchi nyingine za Afrika zilivyo sasa. Ilikuwa ni nchi yenye idadi  kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi, ambapo 30% ya wanawake wajawazito waliambukizwa virusi vya ukimwi. Toka kugunduliwa mtu wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya ukimwi nchini humo mwaka 1982, Uganda ilikuwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 13, hadi sasa kumekuwa na watu milioni moja wamekufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukimwi, hivi sasa bado kuna wagonjwa au watu walioambukizwa virusi vya ukimwi, ambao wengi ni vijana na watu wa makamo. Licha ya hayo, ukimwi umesababisha watoto milioni 2 kuwa yatima.

    Walakini kutokana na jitihada ziliyofanyika kwa miaka zaidi ya 10 iliyopita, serikali na watu wa Uganda wamefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi ya ukimwi. Hivi sasa, kiasi cha watu wa nchi hiyo walioambukizwa virusi vya ukimwi kimepungua hadi 6%, kiasi hicho ni cha chini kuliko katika nchi nyingine za Afrika. Uzoefu wa Uganda katika kudhibiti ukimwi, umesifiwa na jumuiya ya kimataifa kuwa "mfano wa kudhibiti ukimwi katika Afrika". Shirika la Afya Duniani, WHO katika mwaka 1998, liliitunukia Uganda "Tuzo ya kutoa mchango mkubwa kwa kuhimiza watu wa Afrika kuwa na afya nzuri", mwaka 2000 Shirika la Mpango wa Ukimwi la Umoja wa Mataifa lilimtunukia Rais Museveni "Medali ya kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika udhibiti wa ukimwi duniani".

    Ni vipi Uganda iliweza kupunguza idadi ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi na kupata mafanikio makubwa katika upande huo? Ofisa wa kamati ya ukimwi ya Uganda alisema kuwa mafanikio hayo hasa yalitokana na mambo sita.

    La kwanza ni kuwahamasisha watu wote washiriki katika harakati za kupambana na ukimwi.

    Pili ni kutangaza wazi sera husika. Serikali ya Uganda imesema kuwa kuzuia ukimwi ni suala la kwanza kwa Uganda, ambalo linahusiana na maendeleo ya nchi.

    Tatu, ni kuimarisha usimamizi na kupashana habari. Serikali ya Uganda ilianzisha kamati ya ukimwi ya taifa, ambayo ni rahisi kusawazisha ushirikiano ili kuukabili ukimwi kwa pamoja.

    Nne, ni kuweka mpango kamili wa kupambana na ukimwi, ambao unatolewa baada ya kila miaka mitano.

    Tano, ni kuimarisha utafiti wa sayansi ili kuzalisha madawa mapya.

    Sita ni kujenga mfumo wa ushirikiano. Uganda inazingatia ushirikiano kati ya idara husika za nchini na za nchi za nje, na ilianzisha vitengo 7 vinavyoitisha mkutano kila mwezi, na kufanyika mkutano wa taifa wa kila mwaka.

    Ingawa Uganda inakabiliwa jukumu kubwa katika siku za baadaye, lakini hakika itapata mafanikio mapya katika mapambano dhidi ya ukimwi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-22