Mkutano wa tatu wa wakuu wa Umoja wa Afrika ulifunguliwa tarehe 6 Julai huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Mkutano huo ulifanyika kwa siku 3, viongozi wa nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo walijadili namna ya kuondoa umaskini barani Afrika, kuendeleza uchumi na kusukuma utandawazi wa kikanda wakifuata waraka wa "Mikakati ya Kamati ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2004-2007" na nyaraka nyingine mbili. Aidha kusukuma mbele usalama wa kikanda hasa kutatua suala la mgogoro wa sehemu ya Darfur, magharibi ya Sudan pia ilikuwa ni ajenda kubwa ya mkutano huo.
Umoja wa Afrika ulianzishwa mwaka 2002, makao yake makuu yako Addis Ababa, Ethiopia. Umoja wa Afrika ni umoja wa pili muhimu kati ya nchi na nchi baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya. Umoja huo ni jumuiya halisi ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Jukumu kubwa la Umoja wa Afrika ni kulinda amani na utulivu wa Bara la Afrika, kutekeleza mikakati ya kufanya mageuzi na kupunguza umaskini, na kutimiza lengo la maendeleo na ufufuzi.
Umoja wa Afrika una nchi wanachama 53. Vyombo vyake vikuu ni Baraza la wakuu wa Umoja wa Afrika, Baraza la utendaji, Kamati ya kudumu ya wajumbe na Kamati ya Umoja wa Afrika. Mkutano wa wakuu ni chombo chenye madaraka ya juu kabisa cha Umoja wa Afrika, mkutano huo unafanyika mara moja kwa mwaka. Jukumu lake kubwa ni kutunga sera za pamoja za Umoja wa Afrika, kusimamia hali ya utekelezaji wa sera na maazimio, kutoa maagizo kwa Baraza la utendaji na Kamati ya Umoja wa Afrika. Baraza la utendaji linaundwa na mawaziri wa mambo ya nje au mawaziri wengine wa nchi wanachama, mkutano wa baraza hilo unafanyika mara mbili kwa mwaka. Baraza hilo linashughulikia utekelezaji wa maazimio ya mkutano na vikwazo dhidi ya nchi wanachama.
Umoja wa Afrika ulianzishwa badala ya Umoja wa nchi huru za kiafrika yaani OAU ulioanzishwa mwezi Mei mwaka 1963. Mwezi Septemba mwaka 1999, mkutano maalum wa 4 wakuu wa OAU ulipitisha Taarifa ya Silte ukaamua kuunda Umoja wa Afrika. Mwezi Julai mwaka 2000, mkutano wa 36 wa wakuu wa OAU uliofanyika huko Lome, Togo ulipitisha Mswada wa katiba ya Umoja wa Afrika. Mwezi Julai mwaka 2001, mkutano wa 37 wa wakuu wa OAU uliamua rasmi kukaa katika kipindi cha mpito kabla ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika.
Tarehe 8 Julai mwaka 2002, Umoja wa nchi huru za Afrika OAU ulifanya mkutano wa mwisho wa wakuu wa OAU. Umoja wa Afrika uliitisha mkutano wa kwanza wa wakuu kuanzia tarehe 9 hadi 10 Julai mwaka 2002, na kutangaza kuanzishwa rasmi kwa Umoja wa Afrika.
Mwezi Februari mwaka 2002, Umoja wa Afrika uliitisha mkutano maalum wa kwanza wakuu huko Addis Ababa, ukijadili mswada wa marekebisho ya katiba ya Umoja wa Afrika, hali ya Cote D'ivoire, mchakato wa amani ya Burundi pamoja na hali ya sehemu ya maziwa makuu.
Mkutano maalum wa wakuu wa Umoja wa Afrika ulifanyika huko Silte, mji wa pwani wa Libya tarehe 27 hadi 28 Februari mwaka 2004. Mkutano huo ulipitisha maazimio kuhusu matumizi ya maliasili ya maji na maendeleo endelevu ya kilimo.
Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika lilianzishwa huko Addis Ababa tarehe 25 Mei mwaka 2004, viongozi wa nchi 15 wanachama wa baraza hilo walihudhuria mkutano huo.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-22
|