Zhuhai ni mji wa pwani kusini mwa China, ni mji mpya na wenye mandhari nzuri. Mji huu unajulikana nchini na nchi za ng'ambo kutokana na mazingira yake mazuri ya kuishi. Wakazi wa mji huo wanatoka sehemu mbalimbali na wanaishi kwa furaha.
Mzee Li Shunfa ni mkazi wa Zhuhai, alisema kuwa:
"Mimi nimeishi Zhuhai kwa miaka 50, katika kipindi hicho, mabadiliko makubwa yametokea mjini Zhuhai. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, nilipiga picha nyingi za mandhari ya Zhuhai. Zhuhai ya zamani kilikuwa kijiji kidogo cha wavuvi, ufukwe, nyumba za makuti na nyumba duni, lakini sasa majengo marefu yamechomoka hapa na pale."
Mzee Li ana umri wa miaka zaidi ya 70. Ana kumbukumbu halisi ya zamani na ya sasa ya mji wa Zhuhai kutokana na Kemera yake. Kutokana na ujenzi, mji wa Zhuhai umekuwa mzuri siku hadi siku, kijiji cha wavuvi cha zamani kimekuwa kumbukumbu ya picha tu. Jambo linalowafurahisha wakazi ni kuwa, maendeleo ya Zhuhai siyo mpangilio wa majengo marefu peke yake, bali ni uunganishwaji mzuri wa binadamu na mazingira.
Bwana Bao Jinxun na familia yake wanaishi mjini Zhuhai, kwenye roshani ya nyumba yao wanaweza kuangalia milima ya mbali wakati wa mchana, na kutazama mwezi wakati wa usiku. Bwana Bao alisema kuwa, zamani waliishi katika nyumba ya makuti, walikuwa wanapambana na maisha magumu kila siku, sembuse kuwa na wakati wa kufurahia mandhari nzuri huku wakinywa chai. Mtaa wanaoishi ni kama bustani, una miundombinu ya aina mbalimbali, na wanaishi maisha rahisi. Bwana Bao alisema :
"Mimi mwaka huu nina umri wa miaka 74, nilikuwa mkulima, nina watoto 3 wa kiume, mabinti 2, na wajukuu 8, naishi maisha mazuri sana, naona furaha tele."
Mwaka 1998, kituo cha HABITAT cha Umoja wa Mataifa kiliupa mji wa Zhuhai tuzo ya mfano bora wa kimataifa wa kuboresha mazingira ya makazi. Zhuhai pia umepewa sifa ya mji wa bustani na mji wa afya. Bwana Bao na familia yake wameshuhudia mabadiliko na maendeleo ya Zhuhai. Mazingira mazuri ya kuishi ya Zhuhai yamewavuta wasomi wengi kutoka nchini China na ng'ambo, jambo hilo kwa upande mwingine limeufanya Zhuhai kuelekea kuwa mji wa kimataifa hatua kwa hatua.
Bibi Chen Yan kutoka Shanghai ameishi mjini Zhuhai kwa miaka 10 hivi. Mwaka 1996, Bibi Chen Yan alifungua mkahawa wa kwanza wa kahawa mjini Zhuhai, sasa amekuwa mfanyabiashara maarufu katika eneo la chakula. Alisema kuwa, mwanzoni hakuwa na maarifa ya kuendesha biashara ya mkahawa wa kahawa, alijifunza usimamizi huku akiendesha biashara yake, hatimaye amefaulu.
Chen Yan si kama tu ni mtu wa kwanza kuendesha mgahawa wa kahawa mjini Zhuhai, yeye pia ni mwanamke wa kwanza mjini Zhuhai na mkoa wa Guangdong kumiliki leseni ya uendeshaji ndege.
Bwana Walter Strakosch kutoka Ujerumani, ni mtaalamu wa kukarabati injini za ndege, alikuja mjini Zhuhai mwaka 1998, na kuamua kuweka makazi yake huko. Mwaka 2002, Bwana Walter alipewa sifa ya mkazi wa heshima wa mji wa Zhuhai. Kwake yeye, mji wa Zhuhai ni mji mwenye uliochangamka.
"Mjini Zhuhai kuna fursa nyingi za kibiashara, kwenye maonyesho ya ndege yanayofanyika kila baada ya miaka miwili, tunaweza kuwakuta wateja wengi, hii ni muhimu sana kwa biashara yetu."
Mafanikio ya kibiashara na maisha mazuri yamemfanya Bwana Walter kuwa na hisia nzuri sana kwa mji wa Zhuhai na China nzima. Anapenda kusikiliza opera ya kibeijing, alisema kuwa, japokuwa hawezi kufahamu vizuri maneno yanayoimbwa, lakini anapenda sauti yake inayosikika kwenye opera ya kibeijing. Bwana Walter anapenda sana kuitembelea mitaa na kwenda sokoni pamoja na mke wake. Japokuwa hawafahamu sana Kichina, lakini wanaweza kuwasiliana na wachuuzi kwa kutumia ishara ya mikono. Nyumbani Bwana Walter hupenda kuongea na watoto wake kwa Kichina kichanga, na kuwafundisha hadithi ya watoto.
Bwana Walter ameufanya mji wa Zhuhai kama maskani yake ya pili, na kujifanya kama ni mwenezaji habari wa Zhuhai, licha ya yeye mwenyewe kupenda utamaduni wa kijadi wa Zhuhai, pia anajaribu kuwafahamisha marafiki zake waishio karibu naye na walioko nchini Ujerumani utamaduni bora wa kijadi wa China. Kutokana na athari yake, marafiki zake wengi wameamua kubaki na kuishi mjini Zhuhai, wamejifanya kama familia za kawaida za Zhuhai.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-22
|