Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa shule ya msing Kiliwi sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania, ametuletea barua akitoa pongezi kwa idhaa ya kiswahili ya Redio China kimataifa. Anasema anapenda kutumia fursa hii ya kupongeza uhusiano wa kibalozi kati ya Jamuhuri ya watu wa China na Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuadhimisha miaka 40 tangu zianzishe uhusiano wa kibalozi tarehe 26/4/1164, uhusiano ambao ulianzishwa na Viongozi wa wakati ule wa China na aliyekuwa rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania marehemu mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kweli uhusiano huu wa kibalozi kati ya China na Tanzania tunautakia uendelee kudumu milele.
Anasema, vile vile wasikilizaji wenzake wote wa Redio China kimataifa popote pale mlipo ulimwenguni anawataka muendelee kushirikiana kirafiki na idhaa ya kiswahili na Redio China kimataifa. Pamoja na hayo anapenda pia kutoa shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi wote wa Redio China kimataifa, watayarishaji na watangazaji wote wa CRI kwa kazi nzuri wanayoifanya ili kuwapa wasikilizaji habari kemkem na matukio muhimu na nyeti kutoka kote ulimwenguni
Vile vile anapenda pia kutoa shukrani zake za dhati kwa kumtumia bahasha ikiwa imelipiwa stempu pamoja na picha ya sanaa ya mnyama aina ya nguruwe, kwa hiyo anatuomba tuendelee na moyo huo huo wa kuwatumia wasikilizaji bahasha ambazo tayari zimelipiwa stempu, kwani kwa kufanya hivyo wasikilizaji watakuwa wamepunguza gharama za stempu.
Isitoshe anapenda pia tumtumie kamusi ya kiswahili na kichina atafurahi sana ikiwa ombi lake hilo likikubaliwa na wale wanaohusika hapa Radio China Kimataifa. Anasema, mengi zaidi hana isipokuwa anatutakia kila la heri na maisha mema kazini katika mwaka huu wa 2004. Anasistiza kuwa anapenda Urafiki kati yake na idhaa ya kiswahili ya Redio China kimataifa pamoja na wasikilizaji wengine uendelee vizuri..
Tunamshukuru sana kwa baura yake. Kuhusu kamusi ya kichina na kiswahili iliyochapishwa na wachina kwa miaka mingi iliyopita haijachapishwa tena. Kwa walivyoona wanafunzi wachina wakisoma kiswahili wapaswa kusoma kiswahili halisi, kwani tafsiri zenyewe zilizopo kwenye kamusi hiyo bila shaka zina dosari kiasi na hata makosa fulanifulani.
Msikilizaji wetu Mwingine Maluha Martin p.o.box 72203 Kitunda Relini, Dar-es-salaam Tanzania anasema katika barua yake kuwa ana matumaini kuwa sisi sote ni wazima na tunaendelea vizuri na shughuli zetu za utangazaji hapa Redio China kimataifa. Yeye ni mzima wa afya anaendelea vizuri na shughuli zake za kila siku, si hayo tu bali anamshukuru Mungu kwa kumfanikisha kufaulu mtihani wa kidato cha nne waliofanya mwaka jana 2003 kama alivyo kwisha tujulisha hapo awali kuwa amemaliza kidato cha nne.
Anasema, dhumuni la kutuandikia waraka huu ni kushukuru kwa barua tuliyomwandikia na pia kushukuru kwa jinsi tunavyoendelea kujali zaidi urafiki kati yake na sisi kwa kumwandikia barua mara kwa mara na kumtumia vivutio mbalimbali kama vile vitabu kuhusu China, picha ya ukataji wa kisanii ya kima pamoja na vitu vingine vingi kama kalenda.
Anasema anapenda kutuambia kuwa, klabu yake inaitwa Upendo Club. Klabu ya upendo ya wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili ya Redio China kimataifa ilianzishwa mwanzoni mwa mwaka huu mwezi wa pili, hii ni kwa kipindi cha miaka minne aliyokuwa shule amekuwa bweni na kushindwa kupata muda wa kuunda klabu ya wasikilizaji wa Radio China Kimataifa kutokana na kutingwa na shughuli mbalimbali za masomo, na alipomaliza masomo yake mwezi wa kumi na moja mwaka jana akafanikiwa kuunda klabu ya wasikilizaji ya Redio China kimataifa mwezi wa pili mwaka huu.
Anasema anapenda pia kutujulisha kuwa klabu yake ya upendo ya wasikilizaji wa Redio China kimataifa ina wanachama sita na sio hao tu bali wanamatumaini kuwa idadi ya wanachama itaongezeka zaidi. Jambo lingine analopenda kutujulisha ni kuwa klabu ya upendo ina mwenyekiti mkuu wa klabu ya wasikilizaj mwenye umri wa miaka 20 anayeitwa George Johanes ambaye ni kijana wa kiume anayetarajia kujiunga na chuo mwezi wa tisa, chuo ambacho kinaitwa DIT Dar-es-salaam instute of technology. Tunampongeza kwa kwa kuchaguliwa kujiunga na chuo hicho na tunatumaini iataitangaza Radio China Kimataifa hapo Chuoni kwake.
Klabu yake ya wasikilizaji wa Radio China Kimataifa imejitahidi kuweza kuitangaza Radio China na kuifanya ijulikane kiasi miongoni mwa watu katika maeneo wanayoishi na kuwapa watu ratiba na muda wakati ambapo matangazo ya Radio China Kimataifa yanarushwa hewani na wana mikakati kuhusu kuitangaza Radio China Kimataifa ili izidi kufanikiwa, kwa sababu wamegundua kuwa watu wengi wa huko wanakoishi hawaifahamu Redio China kimataifa kama redio nyingine za idhaa ya kiswahili.
Anasema anapenda pia kutuambia kuwa bahasha tunazomtumia ambazo tayari zimelipiwa stempu zinatumika huko kwao bila kikwazo, hii ni kwa sababu ametuma barua kama mbili kwetu na tumemrudishia majibu kupitia bahasha hiyo ambayo imelipiwa stempu, anashukuru sana kwa bahasha hiyo ambayo imelipiwa stempu. Kwa sababu inawasaidia kutotumia pesa, kutuma barua kwetu. Anasema kwa yeye ambaye ni mwanafunzi anayetegemea wazazi kumptaia fedha za matumizi mbalimbali, huo ni msaada mkibwa kwake kwa hiyo anatushukuru sana.
Jambo la mwisho anapenda kutufahamisha kuwa tovuti ya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa iliyofunguliwa tarehe 26 desemba mwaka 2003 inapatikana bila matatizo na kwa urahisi huko aliko. Anasema hana la zaidi, ila anatutakia na kutuombea tuendelee kudumisha urafiki zaidi. Nasi pia Radio China Kimataifa ni matumaini yetu kuwa, siku zijazo ataweza kutuletea maoni na mapendekezo kuhusu tovuti hiyo.
Msikilizaji wetu Richad Chenibei Mateka wa sanduku la posta 65 Kapkateny Mlima Elgon ametuletea barua akisema kuwa, anawapongeza wafanayakazi wote wa Radio China Kimataifa kwa kasi na huduma wanazotoa kwa wakenya na dunia kwa ujumla.
Anawajulisha watalii wa China kuwa Kenya imetekeleza wajibu unaohitajika na nchi za kimataifa na serikali mpya iliyo madarakani huko Kenya kwa kuwavutia watalii na wageni kutoka kote duniani.
MLima Elgon sasa unawavutia watalii wengi sana ambapo kuna wanyama aina ya pimbi, milima iliyopangwa na Mungu, misitu ya kiasili, vyakula vya mimeea kama viazi, vitunguu, mahindi, pareto, kahawa, majani ya chai, ufugaji wa ng'ombe na punda pia kuna nyumba za kitamaduni zinazotumika na jamii ya Elgon masai (sabaot) zilizojengwa kwa ustadi sana kwa fito, mianzi na udongo uliokandamana. Pia kuna mbuga za wanyama ya Mlima Elgon na Chepkitale. Pia kuna mito na hewa nzuri baridi.
Anasema anashukuru wachina waliokwenda kutalii nchini Kenya. Lakini pia anakumbusha kuwa bado kwa jumla bado Wakenya wanahitaji watalii wengi. Na upendo, urafiki na uhusiano huo kati ya Kenya na China uendelee.
Idhaa ya Kiswahili 2004-07-27
|