Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-07-29 19:06:09    
Mwanahistoria mkubwa Sima Qian na Kitabu chake "Rekodi ya Historia"

cri

    "Rekodi ya Historia" ni kitabu kikubwa cha historia na pia ni maandishi yenye taathira kubwa katika fasihi ya China, Sima Qian ndiye mwandishi wa kitabu hiki.

    Kitabu cha "Rekodi ya Historia" kiliandikwa katika Enzi ya Han ya Magharibi, enzi ambayo ilianzia mwaka 206 hadi 25 K.K. nchini China, na ndani ya kitabu hicho mambo yaliyoelezwa ni ya miaka 3000 tangu enzi na dahari mpaka Enzi ya Han ya Magharibi kuhusu siasa, uchumi, utamaduni na historia. Ingawa kitabu hicho ni rekodi ya historia lakini pia ni kitabu cha kwanza kabisa cha fasihi ya kihistoria.

    Kabla ya kukielezea kitabu hicho, kwanza tumfahamu mwandishi wa kitabu hicho, Sima Qian.

    Sima Qian alikuwa mwanahistoria na mwanafasihi katika Enzi ya Han ya Magharibi nchini China, alizaliwa mwaka 135 K.K. katika ukoo wa msomi, baba yake Sima Dan alikuwa afisa wa mambo ya historia katika kasri la mfalme. Sima Qian alikuwa na tabia ya kudadisi mambo tokea utotoni, na alikuwa na mawazo yake mwenyewe kuhusu matukio na watu walioandikwa katika kumbukumbu za historia. Mwaka 108 K.K. Sima Qian alirithi kazi ya baba yake, akishughulika na kazi ya ukutubi katika kasri la kifalme. Pamoja na mfalme aliwahi kutembelea na kufanya uchunguzi katika sehemu nyingi na kumbukumbu nyingi za kihistoria nchini China, na baada ya kulimbikiza data nyingi, Sima Qian alijiandaa kuandika kitabu chake "Rekodi ya Historia". Lakini wakati huo alikumbwa na matatizo kutokana na kumtetea jemadari Li Ling aliyepigana vita mpakani. Kisa chenyewe ni hivi: Jemadari Li Ling alichaguliwa na mfalme kwenda kupigana vita dhidi ya wavamizi kwenye mpaka wa kaskazini. Mwanzoni, habari njema za matokeo ya vita zilikuwa zikimjia mfalme kwa mfululizo ambapo mawaziri wengi walimpongeza mfalme kwa uchaguzi wake wa hekima. Lakini baadaye hali ilikwenda kombo, jemadari huyo na askari wake walivamiwa na maadui kutoka pande zote; ingawa walipigana kufa na kupona kwa siku nane mfululizo lakini mwishowe karibu wote waliuawa. Naye jemadari Li Ling akasalimu amri. Kusikia hayo mfalme alikasirika mno, na mawaziri waliomsifu uhodari wake wa uchaguzi hapo awali, wote wakaanza kumshutumu jemadari Li Ling isipokuwa Sima Qian aliyemtetea jemadari huyo apimwe kwa pande zote, ushupavu wake katika vita, na kushindwa kwake. Kusikia utetezi wake mfalme alighadhibika vibaya akamtia Sima Qian gerezani papo hapo na akatoa hukumu ya adhabu kali ya kudhalilisha ya "kukatwa uume". Baadaye mfalme alitambua kosa lake kwa Sima Qian, akamwachia huru na kumpa cheo kikubwa cha utamaduni katika serikali, lakini wakati huo Sima Qian hakuwa tena na hamu ya kushughulika na mambo mengine, aliona kwamba yeye ni mtu mwenye kasoro, na umuhimu pekee wa kuishi ni kumaliza kitabu chake cha "Rekodi ya Historia". Sima Qian alitumia miaka 13 kumaliza kitabu chake ambacho kina sura 103 na maneno zaidi ya laki tano. "Rekodi ya Historia" ni kitabu cha historia ambacho hakikuwahi kuandikwa hapo kabla nchini China, alikusanya vitabu vyote vya kihistoria na kuhariri kutoka mfalme hadi mfalme pamoja na watu waliohusika, na kutoka enzi hadi enzi, kitabu chake kinahusika na mambo ya matukio makubwa, unajimu, elimu ya kalenda, hifadhi ya maji, uchumi, utamaduni, mambo ya jeshi, jiografia, mila na desturi. Ni kitabu cha mfululizo wa historia ya China kwa kueleza wafalme, mawaziri, maofisa, majemadari, washauri. Na kila makala iliandikwa kwa makini na ufasaha.

    "Rekodi ya Historia" ni kitabu chenye thamani kubwa, thamani yake sio tu kwa jili ya maelezo ya historia bali pia ni kwa ajili ya fasihi yake kubwa. Kwa ufanisi alifinyanga sura halisi za watu walioandikwa katika kumbukumbu za kihistoria kwa mujibu wa data, na ni kitabu kinachotofautiana na maandishi mengine ya kihistoria yaliyoandikwa na maofisa wa kasri la kifalme ambao kutokana na misimamo yao ya kujipendekeza mbele ya wafalme, waliandika sifa zisizostahili na kuacha dosari na makosa. Kadhalika pia kimesifu makabwera waliofanya mapigano dhidi ya udhalimu wa watawala wa kimwinyi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-07-29