Miaka 10 imepita tangu mwaka 1994 ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza usio wa kibaguzi nchini Afrika ya kusini, utamaduni mpya wa kitaifa unaanzishwa nchini Afrika ya kusini. Waziri wa sanaa wa Afrika ya kusini Bwana Paulo Jordaan hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema kuwa, utamaduni huo mpya wa kitaifa umevunja utaratibu wa matabaka mbalimbali wa utamaduni katika zama za ubaguzi wa rangi, ambao unasukuma mbele maingiliano na maafikiano kati ya utamaduni wa aina mbalimbali.
Alipokumbusha zama za ubaguzi wa rangi, Bwana Jordaan mwenye umri wa miaka 62 alisema kuwa, serikali ya zamani ya Afrika ya kusini ilipanga vitu vyote kwa matabaka mbalimbali, watu weupe walikuwa juu sana, na weusi walikuwa wa tabaka la chini kabisa, na watu wa rangi nyingine mbalimbali kukaa kwenye tabaka la kati. Madaraka, mali na nafasi zote zilitokana na kutegemea utaratibu huo wa matabaka. Hali kadhalika kwa utamaduni. Utamaduni wa watu weupe uliheshimiwa na kuhifadhiwa, na kupewa kipaumbele kwa "maendeleo yake". Utamaduni wa waafrika ulibandikwa alama duni ya tabaka la chini. Utamaduni wa aina mbalimbali wenye tofauti ulitenganishwa na watu, hata serikali ilifanya chini juu kuzuia maingiliano na maafikiano kati ya tamaduni za aina mbalimbali.
Afrika ya kusini mpya imevunja seti hiyo ya utaratibu wa kingazi, inatilia maanani utamaduni wa aina zote, kuwatia moyo watu wenye utamaduni tofauti wabadilishane maoni na kufanya maingiliano. Bwana Jordaan alisema, Afrika ya kusini mpya ingekuwa nchi yenye makabila mbalimbali, lugha na tamaduni tofauti za aina mbalimbali.
Afrika ya kusini inapenda kutambua na kuhamasisha watu kufanya maingiliano ya kiutamaduni. Bwana Jordaan alinukuu maneno iliyosema mara kwa mara kuwa, Afrika ya kusini ni nchi ya watu wenye tamaduni tofauti waliokusanyika pamoja.
Bwana Jordaan aliainisha kuwa, Afrika ya kusini inapitia ufufuzi unaogundua kwa mara nyingine mila na desturi. Ufufuzi huo unaonekana katika kulitambua upya Bara la Afrika. Lakini alisisitiza kuwa, mbali na utamduni wa weupe na weusi, utamaduni wa Afrika ya kusini unahusiana na utamaduni wa nchi nyingine. Alitoa mfano kuwa, kila mwaka tamasha kubwa hufanyika huko Cape Town, kusini magharibi ya Afrika ya kusini, lakini muziki unaopigwa kwenye tamasha hilo hasa ni wa mitindo ya nchi za Asia ya kusini mashariki kama vile Indonesia na Malaysia. Hali kadhalika, utamaduni wa Durban kusini mashariki ya Afrika ya kusini una mtindo dhahiri wa India, kwani kuna wahamiaji wengi wa kutoka India huko Durban.
Kutokana na kukabiliwa na wimbi la utandawazi wa uchumi duniani, utamaduni mpya wa kitaifa unaojengwa nchini Afrika ya kusini mpya hakika unaweza kuathirika, lakini Bwana Jordaan hana wasiwasi juu ya hilo. Alisema kuwa, tamaduni za aina mbalimbali za nchi za magharibi zenye mtindo wa kisasa zilitokea Barani Afrika, na hilo, linaonekana dhahiri katika muziki. Aina zote za muziki wa kisasa tokea muziki wa jazz wa Marekani hadi muziki wa samba wa Brazil, zote zina athari za muziki wa kiafrika, na aina zote hizo za muziki wa kisasa ni ngeni kwa watu wa Afrika ya kusini.
Bwana Jordaan alisema kuwa, utandawazi wa utamaduni duniani kwa kweli ulikuwepo kwa aina nyingi mbalimbali katika kipindi cha historia cha miaka mingi. Utandawazi wa utamaduni duniani unaitaka kila nchi kuzifungulia mlango nchi nyingine kwa urafiki badala ya kuzilazimisha nyingine kupokea dhana na kanuni zake.
Idhaa ya kiswahili 2004-08-02
|