Misri ni nchi muhimu katika dunia ya kiarabu. Serikali mpya ya Misri iliyoundwa tarehe 13 Julai imeonesha sura mpya kwenye sekta ya diplomasia. Tarehe 28 Julai, rais Hosni Mubarak wa Misri, waziri mkuu Ahmed Nazef na viongozi wengine walifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bwana Colin Powell, wakibadilishana maoni kuhusu jinsi ya kutatua mgogoro wa Palestina na Israel, kutuliza msukosuko ndani ya mamlaka ya utawala wa Palestina, hali ya Iraq na hali mbaya ya kibindamu wa Darfur, Sudan.
Siku moja kabla, rais Mubarak kwa nyakati tofauti alifanya mazungumzo na rais Bashir Al Assad wa Syria na waziri wa mambo ya nje wa Hispania Miguel Angel Moratinos walioitembelea Misri, wakibadilishana maoni kuhusu hali ya kikanda na masuala yanayozihusu pande zote. Tarehe 25 Julai, Rais Mubarak pia alikutana na mfalme wa Bahrain Hamad bin Al-halifa.
Tarehe 21 Julai, serikali mpya ya Misri iliitisha kwa mafanikio mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi jirani za Iraq, na kumpokea waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq Bw Iyad Allawi.
Japokuwa lilitokea tukio la kutekwa nyara kwa mwanadiplomasia wa Misri na kikundi cha watu wenye silaha nchini Iraq tarehe 23 Julai, jambo hilo liliwahi kuzusha malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani vya Misri, lakini serikali ya Misri imefaulu kumfanya mwanadiplomasia huyo aachiliwe huru kwa njia ya kidiplomasia. Juhudi hizo zimesifiwa na wananchi na vyombo vya habari vya Misri.
Ikiwa nchi kubwa ya kiarabu, Misri imejitahidi kutoa mchango wake katika shughuli za mashariki ya kati. Lengo kuu la mazungumzo kati ya rais Mubarak na rais Assad wa Syria, mfalme wa Bahrain na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw Colin Powell ni kutuliza hali ya Palestina na Israel, na kutatua suala la Iraq. Hivi majuzi, msukosuko wa kisiasa wa mamlaka ya utawala wa Palestina ulioendelea kwa zaidi ya siku kumi umesuluhishwa kimsingi, waziri mkuu wa mamlaka ya utawala wa Palestina Ahmed Qureia ameondoa ombi lake la kujiuzulu, na kuendelea kushika wadhifa wake, kiongozi Yassir Arafat amekubali Qurei asimamie kikamilifu idara za polisi, mambo ya ndani na usalama .
Vyombo vya habari vilidokeza kuwa, mkuu wa shirika la upelelezi la Misri Bwana Suleiman alikuwa anawasiliana mara kwa mra na rais na waziri mkuu wa mamlaka ya utawala wa Palestina, na kuwasukuma wafanye mageuzi ndani ya mamlaka ya utawala kabla ya mwezi Agosti, ili kusawazisha madaraka na uhusiano kati ya rais na waziri mkuu, kuanza kufanya mageuzi ya kisiasa na kupiga vita ufisadi, ili kuboresha hali ya kisiasa ya Palestina. Inamaanisha kuwa, kabla ya Bw. Powell kufika Misri, Misri ilikuwa imefanya juhudi kubwa katika kutuliza msukosuko wa mamlaka ya utawala wa Palestina.
Kuhusu suala la Iraq, Misri inashikilia msimamo wake wa kikanuni na wenye unyumbufu. Kwenye mazungumzo kati yake na waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq, Bw. Nazef alisema kuwa, Misri haitapeleka jeshi nchini Iraq, lakini inaweza kutoa mafunzo ya usalama kwa watu wa Iraq, msimamo huo wa Misri ulisifiwa na upande wa Iraq.
Zaidi ya hayo, kuhusu tatizo la Darfur nchini Sudan, Misri haikufuatana na msimamo wa nchi za maghairbi wa kuiwekea Sudan vikwazo vya kiuchumi, badala yake inasisitiza kuipa serikali ya Sudan muda zaidi, na kupendekeza kutatua suala la Darfur kwa kupitia mazungumzo ya kisiasa. Msimamo huo wa Misri umekaribishwa na serikali ya Sudan.
Idhaa ya Kiswahili 2004-08-04
|