Familia ni mahali muhimu pa kuwatunza watoto, mazingira mazuri au la ya familia yanakuwa na athari kubwa kwa watoto. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya kijamii, mawazo ya wachina kuhusu thamani ya vitu na njia yao ya kimaisha yamebadilika, na mbinu za kuwaelimisha watoto nyumbani pia zimebadilika. Katika kipindi hiki cha leo, tutazungumzia kuhusu elimu ya nyumbani.
Xie Muyi mwenye umri wa miaka 15 mwaka huu anaishi katika mji wa Shenzhen, kusini mwa China. Yeye ni mchangamfu na mwenye moyo mkunjufu, kutokana na tabia yake nzuri, anapendwa na kukaribishwa na watoto wa rika lake. Muda si mrefu uliopita, alifaulu mtihani wa kuingia katika sekondari iliyo nzuri kabisa mjini Shenzhen. Mama yake anafanya kazi katika kampuni ya teknolojia ya mawasiliano na habari (IT), baba yake ni mwalimu wa chuo kikuu, badala ya kumsimamia kwa makini, wazazi wake wanaheshimu fikra na mawazo yake na kumfanya kama mtu mzima.
Xie Muyi alisema: Wazazi wangu hawanioni kama mtoto, bali hunifanya kama mtu mzima na mwenye akili, wanashauriana nami kwa subira mambo yote yanayonihusu. Hata kama nikifanya makosa, wazazi wangu hujaribu kunifahamisha nimefanya makosa gani. Kama nikiwa na maoni mazuri hupokelewa na wazazi wangu.
Hali ya kawaida ya familia ya Xie Muyi ndiyo imempa mazingira mazuri ya kukua na kuwa na tabia nzuri.
Familia nyingi nchini China zinatilia maanani kuwaelimisha watoto nyumbani, lakini wazazi wengi huwa wanajifanya wenye uwezo mkubwa, wanapenda kufanya maamuzi yote kwa ajili ya watoto wao, na hawapendi kuwasiliana na kuelewana na watoto wao ipasavyo. Hivi sasa wazazi wengi wamefahamu dosari ya kufanya hivyo, kama mama wa Xie Muyi Bi. Yang Bo alivyosema:
"Kila mtoto ana mawazo yake mwenyewe, tunapaswa kuwaheshimu na kuwapa nafasi ya kujiendeleza. Watoto wa kizazi kipya wana ujuzi mwingi hata kuweza kutuzidi sisi. Nyumbani kwangu, napenda kushauriana na kujadiliana na mtoto wangu kuhusu shughuli zote za nyumbani hata za kazini, nafikiri kwa kufanya hivyo naweza kumpa nafasi ya kuifahamu jamii ."
Nchini China, idadi ya wazazi kama Bi. Yang Bo inaongezeka siku hadi siku. Mwandishi wetu wa habari alimtembelea mhandisi mmoja anayeitwa Zhao Gang. Bwana Zhao ana binti mwenye umri wa miaka 11, anasoma shule ya msingi. Tofauti na wazazi wengine, Bw. Zhao hajali sana matokeo ya masomo ya binti yake, bali anatumai kuwa binti yake atakua vizuri kiakili na kisaikolojia.
Bw. Zhao alisema: "Mimi sifuatilii sana matokeo yake ya masomo, nafikiri jambo muhimu zaidi ni awe na roho nzuri . Natumai kuwa, mtoto wangu atakuwa na tabia nzuri, kuweza kusikilizana na watu wengine kwa furaha na kwa urahisi, na kuweza kuelewa shughuli yoyote kwa maamuzi sahihi. Zamani tulizingatia zaidi elimu kwa mtoto, lakini kwa kweli, hisia na tabia ya mtoto pia ni muhimu sana, kama mtoto hawezi kujumuika vizuri na jamii, na kuweza kufuata maendeleo ya jamii, itakuwa ni shida yake baadaye."
Tangu China itekeleze sera ya uzazi wa mpango kuanzia miaka ya 70 ya karne iliyopita, familia nyingi mijini zina mtoto mmoja tu, ni hali ya kawaida kwa watu wazima kadhaa kumhudumia mtoto mmoja, kama vile wazazi, babu na bibi, matokeo yake ni kuwa, watoto wengi wanadhoofishwa uwezo wao na hawawezi kujitegemea kimaisha. Baadhi ya wazazi ili kuandaa uwezo wa watoto wao wa kuishi kwa kujitegemea, huwashirikisha katika shughuli za aina mbalimbali za kijamii, hata kuwapeleka watoto ng'ambo kwa kujiendeleza zaidi.
Katika miaka ya hivi karibuni, jumuiya za kienyeji nchini China zimefanya kazi nyingi katika hali ya kuwaelimisha watoto na wazazi kwa ujumla, hasa kuhusu idadi inayoongezeka siku hadi siku ya watu wanaohamahama waishio mijini. Kutokana na maendeleo ya kiuchumi nchini China, wakulima wengi wanamiminika mijini kutafuta ajira, na suala la kuwapatia elimu watoto wao limekuwa suala la kufuatiliwa na jamii. Ili kuwafahamisha wazazi hao kuhusu jinsi ya kuwaelimisha watoto wao nyumbani, mtaa wa mashariki wa mji wa Beijing unazingatia kuanzisha shule ya wazazi kwa wale wanaohamahama kutoka vijijini, mkuu wa shule hiyo Bi. Liu Hong alisema :
"Tunajua kwamba, baadhi ya wazazi wa watu wanaohamahama kutoka vijijini wanahitaji kufahamishwa jinsi ya kuwaelimisha watoto wao nyumbani. Baadhi yao wanauza mboga, wengine wanafanya kazi za vibarua, hawana nafasi ya kushiriki semina zinazohusika, pia hawana wakati wa kusoma vitabu vinavyohusika. Hivyo tunafikiri kuanzisha shule hiyo ya wazazi ili kuinua sifa ya wazazi hawa."
Bi. Tan Lining kutoka sehemu ya kaskazini mashariki ya China anaishi yeye na mtoto wake, anapenda kujiunga na shule ya wazazi, alisema kuwa, mtoto wake amehitimu masomo ya shule ya msingi, ataingia sekondari ya chini mwaka huu, yuko katika kipindi cha kupevuka, kwa sababu Bi. Tan alishindwa kujua mawazo ya mtoto wake, hawawezi kuelewana vizuri, hivyo anatumai kujifunza kuhusu jinsi ya kuelewana na mtoto wake .
Watoto ni matumaini ya wazazi na ya jamii nzima. Kama tukiweza kuwapa mazingira mazuri ya kukua, ndiyo tutapata jamii yenye matumaini.
Idhaa ya kiswahili 2004-08-05
|