Sauti kubwa za kushangilia zilisikika mara kwa mara wiki iliyopita kwenye jumba la maonesho la taifa la Ghana huko Accra, mji mkuu wa nchi hiyo, kwani wacheza ngoma hodari na wanasarakasi kutoka China walikuwa wanafanya maonesho mazuri.
Tamasha la kwanza la wiki moja ya sanaa za kichina ilifanyika nchini Ghana kuanzia tarehe mosi mwezi Agosti. Maonesho manne ya kichina ya nyimbo, dansi na sarakasi yaliyoandaliwa na wizara ya utamaduni ya China yaliwavutia waghana wengi. Wakati huo huo, maonesho ya picha kuhusu hali ya China na sanaa za ushonaji pia yamewafungua macho. Tamasha la sanaa za China lililofanyika nchini Ghana.
Watu wengi walikusanyika mbele ya picha zinazoonesha mji wa Shanghai, wakishangaa sana mabadiliko makubwa yaliyotokea katika mji huo wa China. Vitu vizuri vya ushonaji vilivyotengenezwa na wasanii wa China pia vilisifiwa sana na waghana.
Ghana ni nchi ya kiafrika yenye historia ndefu ya utamaduni wa kale. Baada ya kupata uhuru, serikali ya Ghana siku zote imekuwa ikitilia maanani kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jadi, ili kuwafanya wananchi kuwa na fahari ya taifa lao na kushirikiana vizuri. Baada ya jitihada za miongo kadhaa, muziki, dansi, drama, uchoraji, nakshi na ubunifu wa sanaa zinazotumika katika maisha ya watu zinajulikana barani Afrika. Ikiwa nchi iliyoanzisha uhusiano wa kibalozi na China mapema zaidi kati ya nchi zilizoko eneo la kusini mwa Sahara, sanaa za kichina si kitu cha kigeni kwa wananchi wa Ghana. Tangu nchi hizo mbili zilipoanzisha uhusiano wa kibalozi, uhusiano wa siasa kati ya nchi hizo mbili unaendelea vizuri, wakati ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara unapata matokeo mapya, na mawasiliano ya utamaduni yanazidi kuboreshwa.
Waziri wa utalii wa Ghana kwa niaba ya rais John Agyekum Kufuor wa nchi hiyo alihudhuria sherehe ya ufunguzi wa tamasha la sanaa za kichina. Rais Kufuor alisema kupitia waziri huyo kwamba, watu wa nchi mbalimbali wanapaswa kufahamu na kuelewa tamaduni tofauti, ili kuelewana. Kufanyika kwa tamasha la sanaa za kichina kunawawezesha watu wa Ghana kujionea tofauti na mambo yaliyo sawa kati ya tamaduni za China na Ghana.
Mwenyekiti wa kamati ya utamaduni ya taifa ya Ghana alisema alipokutana na ujumbe wa utamaduni wa China alisema kuwa, ziara ya waziri mkuu wa zamani wa China hayati Chou Enlai nchini Ghana miaka arobaini iliyopita ilikuwa kumbukumbu nzuri kwa wananchi wa Ghana, hali hiyo inaonyesha urafiki mkubwa kati ya watu wa Ghana na China. Alisema wananchi wa Ghana hawatasahau daima misaada iliyotolewa na inayotolewa na serikali ya China bila ya masharti yoyote.
Mawasiliano ya utamaduni ni daraja la maelewano kwa watu wa nchi mbalimbali. Tangu miongo kadhaa iliyopita, China inaendelea kukuza mawasiliano na ushirikiano wa utamaduni na nchi za Afrika kwa msingi wa usawa, urafiki na kunufaishana, juhudi hizo zimetoa mchango mkubwa katika kuzidisha urafiki na kuhimiza ushirikiano katika sekta nyingine kati ya pande hizo mbili.
Ghana ni kituo cha tatu cha Shughuli za "Utamaduni wa China barani Afrika". Shughuli hizo zilifanyika kuanzia mwezi Julai hadi katikati ya mwezi Agosti, na hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya China kufanya shughuli kubwa za mawasiliano ya utamaduni Barani Afrika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Shughuli hizo zinajulisha utamaduni wa aina mbalimbali wa China kwa watu wa Afrika, na kupitia shughuli hizo, wanaelewa zaidi hali ya China. Mbali na hayo, shughuli hizo pia zinakuza ushirikiano wa utamaduni kati ya China na Afrika.
Shughuli za "Utamaduni wa China barani Afrika" zilifunguliwa tarehe 13 mwezi Julai nchini Afrika Kusini, na zitafungwa tarehe 13 mwezi Agosti. Katika muda wa mwezi mmoja, tamasha la sanaa za kichina limefanyika kwenye nchi tatu za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Cameroon na Ghana, wakati huo huo, wasanii wachina wa muziki, ngoma, sarakasi na Kongfu watafanya maonesho ya michezo ya sanaa katika nchi 11 za Afrika.
Tarehe 13 mwezi Julai, mjumbe wa taifa wa China bibi Chen Zhili alihudhuria sherehe ya ufunguzi wa shughuli za "Utamaduni wa China barani Afrika" zilizofanyika nchini Afrika Kusini. Hali hiyo inaonesha kuwa, viongozi wa China wanatilia maanani sana kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya China na Afrika, pia imeonesha jinsi China inavyojitahidi kutekeleza mipango iliyofikiwa kwenye mkutano wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika.
|