Sehemu ya kivutio ya Jiouzhaigou inajulikana duniani kwa mandhari yake nzuri ya kimaumbile. Sehemu hiyo iko kusini magharibi mwa China. Mwaka 1992 iliwekwa kwenye orodha ya kumbukumbu za urithi wa dunia, na mwaka 1997 iliorodheshwa katika "hifadhi ya viumbe ya dunia".
Sehemu ya kivutio ya Jiouzhaigou iko mkoani Sichuan, kilomita 450 kutoka mji mkuu wa mkoa huo, Chengdu, jumla ya eneo lake ni kilomita za mraba 620, asilimia 52 ya sehemu hiyo ni misitu ya kiasili.
Sehemu hiyo sio kubwa lakini ina maziwa mengi na maji ni safi, wenyeji wa huko wanayaita maziwa hayo kwa jina la "watoto wa bahari". Kati ya maziwa hayo kuna ziwa moja linaloitwa "Ziwa la Kifaru", Ziwa hilo ni kubwa kuliko maziwa yote.
Ziwa la Kifaru lina urefu wa kilomita 2 na kina cha maji mita 18, na urefu wake juu ya usawa wa bahari ni mita 2,400. Kuhusu ziwa hilo wenyeji wa huko wa kabila la Watibet wana masimulizi yao. Wanaeleza kuwa, hapo kale alikuwako sufii mmoja mzee wa dini ya Buddha aliyekuwa mahututi alifika huko kwa kupanda kifaru, alipofika kwenye ziwa hilo bila makusudi alikunywa maji ya ziwa hilo ikawa kioja kwani ugonjwa wake ulipona kiajabu. Basi tokea hapo sufii huyo aling'ang'ania kukaa huko akihofia ugonjwa ungemrudia tena asipotumia maji ya ziwa hilo. Mwishowe aliingia ziwani akiwa mgongoni mwa kifaru ili akae hapo daima. Baadaye wenyeji walilipatia ziwa hilo jina la Ziwa la Kifaru. Kando ya ziwa kuna majabali mawili yanayoegemeana, wenyeji wanaeleza, hapo awali majabali hayo yalikuwa wapenzi wawili.
Katika sehemu ya Jiouzhaigou kuna maporomoko 14 yaliyotapakaa kila mahali, kileleni, magengeni, mabondeni na misituni. Kati ya maporomoko hayo poromoko linalovutia zaidi ni la Norilang. Poromoko hilo lina urefu wa mita zaidi ya 20 na upana zaidi ya mita 300, ni poromoko lenye upana mkubwa kabisa duniani.
Licha ya maporomoko ya maji, pia kuna milima yenye mandhari ya ajabu, milimani kuna misitu minene ya asili, maua na majani yenye rangi yanachangia uzuri wa huko, theluji na mawingu pamoja na ukungu unaoelea milimani yanawafanya watu kuona kama wako katika dunia nyingine. Miongoni mwa milima, kuna milima miwili inayokabiliana, mmoja unaitwa mlima Dage, mwingine unaitwa mlima Semuo, weneyeji wanaiabudu sana.
Inasemekana kwamba katika enzi ya kale, Kaka Dage na Dada Semuo walikuwa wachumba wawili. Mwaka mmoja mfalme wa theluji aliharibu misitu na maziwa. Wachumba hao wawili waliamua kwenda mlimani kutafuta kito cha kijani kinachoweza kurudisha mazingira ya awali. Mfalme wa theluji kisiri siri alimnywesha maji ya kupoteza fahamu ili amwoe binti yake. Lakini dada Semuo alilia sana na machozi yalimamsha mpenzi wake, jambo hilo pia lilimhurumisha binti wa mfalme. Mfalme wa theluji alitaka kulipiza kisasi, wapenzi hao wawili walimeza kito wakageuka kuwa milima miwili ya kumzuia mfalme wa theluji asiharibu tena mazingira ya awali. Tokea hapo wapenzi hao wawili wanalinda eneo la Jiouzhaigou liwe mandhari nzuri duniani daima.
Mwanakamati wa Kamati ya Urithi wa Dunia nchini China alisema, katika sehemu ya Jiouzhaigou kuna viumbe wa aina nyingi. Mandhari yake ni ya ajabu na ya kuvutia, kuna aina 140 za ndege na wanyamapori wengi walioko hatarini kutoweka, ikiwa ni pamoja na panda.
1 2 3
|