Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-08-26 20:08:08    
Mtindo mpya wa wazee kuishi katika sehemu nyingine

cri
    Hii ni mara ya pili kwa profesa Shi Zhengzong anayeishi Hefei, mji mkuu wa Anhui, kwenda kukwepa joto kali katika mji wa Dalian. Katika majira ya joto ya mwaka huu, mzee huyo alikwenda kukaa katika nyumba ya wazee inayojulikana kwa jina la Tongtai mjini Dalian akiandamana na wazee wengine karibu 20 kutoka mkoa wa Anhui.

    Kutalii Dalian kupitia shirika la utalii kutoka mji wa Hefei kwa siku tano, kila mtu atalipa Yuan 1,500, lakini kukaa katika nyumba ya wazee huko Dalian anatakiwa kulipa Yuan 2,000, ingawa analipa Yuan 500 zaidi, lakini siku anazokaa huko Dalian ni 30. Kutumia njia hiyo ya kutalii na kukaa katika sehemu nyingine, kumekuwa mtindo mpya wa maisha ya wazee wa siku hizi. Kufanya hivyo, si kama tu kunapunguza gharama, bali pia wanaweza kutimiza azma yao ya miaka mingi ya kutalii sehemu mbalimbali nchini.

    Nyumba ya wazee ya Tongtai mjini Dalian ilianzishwa mwezi Agosti mwaka jana, katika muda wa mwaka mmoja uliopita, nyumba hiyo ilipokea wazee zaidi ya 360 kutoka sehemu nyingine nchini na nchi za nje. Meneja wa nyumba hiyo, Bw. Jia Gang alisema kuwa mtindo huo unaunganisha utalii, kupumuzika kwa muda na kuishi maisha ya uzeeni. Njia hiyo si kama tu imebadilisha wazo la kijadi la kuishi maisha ya uzeeni kwa wazee, bali pia limechangamsha wazee kwa maisha mapya yenye shughuli nyingi za utamaduni, pamoja na kuchangia ongezeko la uchumi wa taifa.

    Kiongozi wa kitengo cha utafiti wa sayansi wa wazee cha taasisi ya sayansi ya jamii ya China, Profesa Xiong Bijun anaona kuwa wazee wamepata nafasi nzuri ya kujistarehesha kuliko watu wengine, wanatarajia kujiburudisha na kujichangamsha kwa njia ya utalii ili kuimarisha afya zao. Kuendeleza huduma hiyo kwa wazee, kunaweza kuwasaidia wazee wanaokaa sehemu ya kaskazini kwenda sehemu ya kusini zenye joto kukwepa baridi kali katika majira ya baridi, njia ambayo licha ya kuwawezesha kukwepa baridi kali ya sehemu ya kaskazini, bali pia inaweza kuwasaidia wazee wanaokaa sehemu ya kusini kwenda sehemu ya kaskazini kukwepa joto kali katika majira ya joto.

    Wataalamu wanaona kuwa sasa kumekuwa na uwezekano kwa wazee kuishi sehemu nyingine uzeeni. Kwanza ni kutokana na mabadiliko ya mawazo ya watu, wazee wengi wanaona kuwa ni heri waende kutembelea sehemu nyingine, bado wakiwa na afya nzuri; pili kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha, baadhi ya wazee wenyewe au watoto wao wamekuwa na nguvu ya kiuchumi ya kumudu gharama ya kuishi katika sehemu nyingine kwa wazee wao; tatu kwa kuwa hivi sasa mashirika ya kutunza wazee yameanzishwa katika sehemu mbalimbali, ambazo kiwango cha utoaji huduma pamoja na zana zake zimefikia kiwango cha kuridhisha, na kuweza kutoa huduma nzuri kwa wazee kuendana na mahitaji yao tofauti.

    Habari zinasema kuwa hivi sasa, katika sehemu zilizoendelea kiuchumi, ikiwa ni pamoja na miji ya Shanghai na Shenzhen, idadi ya wazee wanaoishi sehemu nyingine uzeeni, inaongezeka mwaka hadi mwaka. Baadhi ya wazee wenye hali nzuri kiuchumi, wanahama hama kama ndege katika majira ya mwaka. Licha ya hayo kuna baadhi ya wazee wanaokwenda kwa pamoja kuishi katika sehemu zenye mandhari nzuri, ambazo ni pamoja na mji wa kale Xian na mji wa Guilin.

    Profesa Xiong alisema kuwa maswala yanayopaswa kutatuliwa kwa wazee kuishi katika sehemu nyingine ni pamoja na tiba, chakula, malazi, mawasiliano na burudani. Kwa mfano, nyumba za wazee zinapaswa kuwa na madaktari, wauguzi, zana za tiba, kantini, vyombo vya jikoni na kuwa na super market iliyo karibu, mawasiliano mepesi, waweze kwenda kutembelea wao wenyewe, mazingira mwafaka na kuweza kufanya mazoezi ya mwili na matembezi.

Idhaa ya Kiswahili 2004-08-26