Saa nne asubuhi, tarehe 23, mwezi Agosti, katika idara ya usimamizi wa shughuli za uhamiaji nchini China ya idara ya usalama wa umma ya Shanghai, wageni zaidi ya 10 walisimama kwenye foleni mbele ya madirisha ya kushughulikia "kadi ya kijani" na kusubiri kushughulikia maombi ya kibali cha ukazi wa kudumu, yaani "kadi ya kijani". Walikuwa na vitambulisho na picha mbalimbali, wakiuliza kwa makini maofisa wa idara hiyo na kujaza fomu kufuatana na maelezo ya maofisa hao. Hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza kushughulikia maombi ya "kadi ya kijani" baada ya wizara ya usalama wa umma na wizara ya mambo ya nje ya China kutangaza tarehe 20 kuwa China inaanza kutekeleza utaratibu wa "kadi ya kijani".
Kufuatana na Utaratibu wa kuthibitisha na kupitisha maombi ya ukazi wa kudumu kwa wageni nchini China, wageni wanaotaka kuomba "kadi ya kijani" ya China lazima wawe waliotoa mchango mkubwa kwa China. Kwa mfano, Bw. Gehade Maihefa ni meneja mkuu wa kampuni ya chuma na chuma cha pua cha Krupp mjini Shanghai. M-Austria huyo mwenye umri wa miaka 49 pia ni naibu mwenyekiti wa shirikisho la makampuni yenye mitaji ya nje mjini Shanghai, na aliwahi kupata tuzo ya mchango muhimu kwa maendeleo ya eneo jipya la Pudong na tuzo ya maua ya magnolia ya Shanghai, pia ni mkazi wa heshima wa Shanghai. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, zamani alipaswa kubadilisha kibali cha ukazi kila baada ya miezi 6, na safari hii "kadi ya kijani" atakayopata itabadilishwa kila baada ya miaka 10 kama ilivyo kwa kitambulisho cha wakazi wa China.
Miongoni mwa wageni hao, wageni kadhaa ni Wamarekani wenye asili ya kichina. Historia ya ofisa mkuu mtendaji wa kampuni ya mtandao ya Shengda ya Shanghai Bw. Tang Jun ni ya kufurahisha. Mwaka 1993, Bw. Tang Jun alipata "kadi ya kijani" ya Marekani, na mwaka 1998 alipata uraia wa Marekani. Baada ya kufanya kazi mjini Shanghai kwa miaka 7, aliona kuwa, kutumia kibali cha ukazi wa wageni kuna usumbufu mkubwa. Alipaswa kuomba visa kwanza akitaka kuingia au kutoka China, alipaswa kubadilisha kibali cha ukazi mara kwa mara, na akitaka kwenda miji mingine au kubadilisha kazi anapaswa kushughulikia utaratibu wa kuandikishwa. Mke na watoto wake wawili bado wako Marekani, anatumai wao wote watakuwa na "kadi ya kijani" ya China. Alipotaja tofauti kati ya "kadi ya kijani" ya Marekani na ya China alisema kuwa, ukitaka kupata kadi hiyo nchini Marekani, unatakiwa kuwa na kazi na pato la kudumu, lakini China ambayo si nchi ya wahamiaji, unatakiwa kutoa mchango kwanza kwa jamii.
Mkuu wa idara ya usimamizi wa shughuli za kuingia na kutoka China ya Shanghai Bw. Ma Zhendong alisema kuwa, kabla ya kutekeleza utaratibu wa "kadi ya kijani", mjini Shanghai kwa jumla wageni zaidi ya 130 walipata kibali cha ukazi wa kudumu, na wengi wao ni watoto wa wageni wazee wenye asili ya kichina; baada ya kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, wageni 6 tu walipata kibali hicho, miongoni mwao hayati Mmarekani Bi. Gen Lishu aliyewahi kushiriki katika mapinduzi ya China, wengine watano waliwahi kutoa mchango maalum kwa Shanghai. Baada ya kutekeleza utaratibu wa "kadi ya kijani", wageni ambao maombi yao ya ukazi yataidhinishwa na kupewa haki ya ukazi wa kudumu.
Idhaa ya Kiswahili 2004-08-27
|