Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-09-01 16:40:44    
Tanzania yatilia maanani kuwaendeleza vijana

cri

    Mwandishi wetu wa habari alibahatika kufanya mahojiano na mkuu wa ujumbe kutoka Tanzania, mkurugenzi wa maendeleo ya vijana katika wizara ya kazi, maendeleo ya vijana na michezo ya Tanzania Bi. Joyce Shaidi kuhusu hali ya vijana nchini Tanzania.

    Swali: Bi. Joyce shaidi, kwanza unaweza kutueleza hali ya vijana nchini Tanzania?

    Jibu: Vijana wa Tanzania wenye uwezo wa kufanya kazi ni zaidi ya asilimia sitini, kwa hivyo ni idadi kubwa ya nguvu kazi ya Taifa, lakini tatizo kubwa linalowakabili vijana ni tatizo la ajira. Kuna vijana wengi ambao wamepata elimu katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi, sekondari, vyuo na hata chuo kikuu, ambapo wengi wanaingia katika soko la ajira, lakini wengi pia wanapenda kupata ajira rasmi. Wanaoingia kwenye ajira binafsi ni kwa sababu nafasi za ajira rasmi ni chache ikilinganishwa na nafasi za kujiajiri wao wenyewe.

    Swali: Serikali ya Tanzania ina mpango gani wa kuwawezesha vijana wa Tanzania kujiendeleza?

    Jibu: Serikali kwanza ina sera, sera ya maendeleo ya vijana inayolenga kumwendeleza kijana katika maeneo makubwa ambayo yanahusu maswala ya kiuchumi, kuongeza ajira kwa vijana, na ajira sio kuajiriwa tu ofisini, bali pia kumwezesha kujiajiri wenyewe. Kwa hiyo ni nia ya serikali kuhakikisha kwamba vijana wanapata elimu ili kujengewa uwezo wa kuweza kushiriki katika ajira isiyo rasmi. Tanzania ni nchi yenye ardhi kubwa, lakini imejionyesha kwamba vijana wengi hawapendi kushiriki katika kilimo, kwahiyo ni nia ya serikali kuwahamasisha vijana ili waweze kutambua rasilimali walizonazo ikiwa ni pamoja na ardhi ili waweze kujiajiri wenyewe katika sekta mbalimbali, hasa hasa katika sekta ya kilimo.

    Swali: Ugonjwa wa ukimwi unaleta athari mbaya katika nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania, na vijana wengi wa duniani wameathirika zaidi. Je serikali ya Tanzania ina mpango gani wa kuwahamasisha vijana wa Tanzania kupambana na ukimwi?

    Jibu: Asante sana, swala la ukimwi ni swala ambalo serikali ya Tanzania imelipa kipaumbele, sasa hivi tuna sera ya Taifa kuhusu ukimwi ambayo inatoa maelekezo kwa sekta zote ili kuhakikisha kwamba inakuwa na mipango ya kudhibiti ukimwi. Vilevile kuna mkakati wa Taifa wa kudhibiti ukimwi, katika mkakati huu wa Taifa wa kudhibiti ukimwi, sekta zinazohusiana na maswala ya vijana, kwa mfano Wizara ya elimu, Wizara ya kazi, maendeleo ya vijana na michezo zimepewa kipaumbele kuhakikisha kwamba zinakuwa na mipango inayohusu vijana. Kwahiyo elimu ya ukimwi hutolewa kwa vijana ndani ya shule kupitia wizara ya elimu, na vijana nje ya shule kupitia Wizara ya kazi, maendeleo ya vijana na michezo. Vilevile taasisi za vijana zimehamasishwa kuanzisha vikundi mbalimbali vya vijana ambavyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mashirika mbalimbali kuhakikisha kwamba, vijana wanapata elimu kuhusu afya ya uzazi, ambayo inatoa stadi za maisha kwa vijana ili waweze kujikinga kwa mbinu mbalimbali. Kwa hiyo kuna msisitizo katika maeneo ya kujikinga kuhakikisha kwamba vijana hawaambukizwi na vilevile kuna msisitizo katika kuwajali wale ambao wameathirika ili kuhakikisha hakuna unyenyepa yaani aliyeathirika asidharauliwe au asibugudhiiwe kwa sababu tu ameathirika. Kwa hiyo katika juhudi hizo serikali inasisitiza sana ushiriki wa vijana kwasababu wao ndio walioathirika sana na wao kama hawatapata ukimwi ni wazi kwamba Taifa lijalo litakuwa na vijana ambao hawana ukimwi.

Swali : Unaweza kutueleza kuhusu hali ya upatikanaji wa ajira kwa vijana wa Tanzania wa kike na wa kiume?

Jibu: Kimsingi serikali ya Tanzania haibagui kijana kwa kufuatana na jinsia yake, kwa hiyo elimu hutolewa bila kujali wewe ni kijana wa kike. Tatizo linalojitokeza ni kwamba vijana wa kike mara nyingi wanaathirika kwa kuachwa nyuma kwasababu ya mila mbalimbali na desturi ambazo zipo katika makabila mbalimbali. Kwa mfano, kijana wa kike anaweza kulazimishwa kuolewa mapema. Anapoolewa mapema ni kwamba anashindwa kuendelea kielimu na anaposhindwa kuendelea mbele ni kwamba anapunguza nafasi yake ya kupata nafasi nzuri katika ajira kwahiyo serkali inahamasisha kila taasisi kuhakikisha kwamba jamii inawashirikisha vijana wa jinsia zote kushirki katika mipango mbalimbali ya elimu, kwa sababu elimu ndio msingi.

    Swali : Na kuhusu ushirikiano kati ya vijana wa Tanzania na China unaonaje?

    Jibu: Kusema kweli serikali ya Tanzania imeweza kufaidi matunda ya serikali ya China katika kuwasaidia vijana kwa muda mrefu sana, nakumbuka mimi mwenyewe nilikuwa bado kijana nikiwa elimu ya sekondari siku nyingi tu lakini mmoja wa rafiki yangu ambaye tulikuwa wote shuleni aliweza kukaribishwa China katika programu hizi na ushirikiano. Kwa hiyo tuna ushirikiano katika maswala ya elimu, kama nilivyosema kwamba elimu ndio msingi wa kumuongoza kijana kwa hiyo vijana wengi wa Tanzania wamepata elimu nzuri tu kwa kupitia msaada wa serikali ya china. Na kwa misingi hiyo kwa sababu wameweza kupata elimu vilevile wameweza kupata ajira. Kwa mfano: Sasa hivi kuna miradi mbalimbali ambayo ipo nchini Tanzania inaendeshwa na serikali ya China kusaidia serikali ya Tanzania kwa hiyo kuwepo kwa miradi ile kumetoa nafasi za ajira kwa vijana ambao wamepata elimu, na ila tu ningependa kusisitiza kwamba tunahitaji nguvu zaidi kwa maana kwamba katika eneo la kilimo kama nilivyozungumza kwamba vijana wengi wa Tanzania bado hawana utaalamu sana katika maswala ya kilimo, kwasababu najua wachina wanao utaalamu mzuri wa kilimo, kwahiyo hilo ni eneo zuri tunaweza tukalikuza zaidi katika kushirikiana na serikali ya China ili kuhahakisha vijana wa Tanzania wanakuwa wakulima wazuri na kuweza kutambua masoko mbalimbali ya bidhaa za kilimo duniani.

    Swali: Una matumaini gani kuhusu ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Tanzania?

Jibu: Matumaini najua ni mazuri tu, kwasababu kama nilivyozungumza, ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na China ni wa muda mrefu sana tangu tukiwa vijana, kwa hiyo nina imani kwamba utazidi kuwa mzuri na imejionyesha wazi hata kiongozi wetu wa taifa Mheshimiwa Rais Mkapa alikuwa hapa China mwaka huu, ni moja ya njia hizo za kukuza mahusiano kwahiyo nina imani kwamba ushirikiano utazidi kukua.

Idhaa ya kiswahili 2004-09-01